Uchaguzi Tanzania: Uchaguzi wa mitaa uliosusiwa na wapinzani wafanyika huku baadhi ya maeneo wagombea wa CCM wakipita bila kupingwa

Uchaguzi Serikali za mitaa

Chanzo cha picha, Eagan Salla BBC

Maelezo ya picha, Wapigakura wakihakiki majina leo asubuhi (tarehe 24 Novemba)
Muda wa kusoma: Dakika 3

Wakazi wa maeneo jijini Dar es Salaam wamejitokeza kupiga kura, asubuhi ya siku ya Jumapili, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa tangu kuanza kwa zoezi la kupiga kura.

Hata hivyo katika maeneo kadhaa zoezi likionekana kwenda taratibu, huku kwenye maeneo mengine zoezi halikufanyika kabisa kwa kile kilichoelezwa kuwa kulikuwa na mgombea mmoja tu ambaye amepita bila kupingwa.

Mfano katika wilaya moja ya Kinondoni ambayo ilikuwa na mitaa 106 inayowaniwa, mitaa 105 wagombea wa chama cha CCM walipita bila kupingwa katika nafasi zote, isipokuwa mtaa mmoja pekee, kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi wa Manispaa ya Kinondoni mwalimu Kiduna Mageni.

Hata hivyo pamoja na kuwa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani walitangaza kususia uchaguzi huu, lakini wagombea wa baadhi ya vyama hivyo wameendelea kuwania nafasi mbalimbali katika baadhi ya maeneo.

Uchaguzi Serikali za mitaa

Chanzo cha picha, Eagan Salla BBC

Maelezo ya picha, Uchaguzi Serikali za mitaa

Unaweza kutazama mahojiano na msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Kinondoni

Ruka Facebook ujumbe

Haipatikani tena

Tazama zaidi katika FacebookBBC haihusiki na taarifa za kutoka mitandao ya nje.

Mwisho wa Facebook ujumbe

Hali ilivyo katika vituo vya kupigia kura uchaguzi wa serikali za mitaa jijini Dar es salaam:

Uchaguzi Serikali za mitaa

Chanzo cha picha, Eagan Salla BBC

Maelezo ya picha, Maafisa wanaosimamia zoezi wakiwa kwenye vituo vya kupiga kura
Mwanamke akishiriki katika shughuli ya kupiga kura

Jumla ya vyama vinane vilijitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya nchi hiyo kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu.

Uchaguzi huu hufanyika chini ya Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Tanzania kuwa ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kuwa ndiyo msingi wa mamlaka yote iliyonayo serikali hupata kutoka kwa wananchi.

Uchaguzi Serikali za mitaa

Chanzo cha picha, Eagan Salla BBC

Maelezo ya picha, Uchaguzi Serikali za mitaa

Vyama vilivyotangaza kujitoa kushiriki kinyang'nyiro cha uchaguzi huo ni Chadema, UMD, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo, CUF na Chauma.

Uamuzi wao ulitokana na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya umma na kukilaumu chama tawala CCM kuwa chanzo cha kuvurugika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu nchini.

Licha ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo, mwenye dhamana ya uchaguzi huo kutoa matamko mawili yenye nia ya kuviomba vyama vya upinzani kulegeza misimamo yao na kuwataka wagombea walioteuliwa kuendelea na uchaguzi huo, lakini hapakuwa na mafanikio yoyote.

Rais akishiriki katika uchaguzi wa mitaa nchini tanzania

Katika taarifa yake iliyokaririwa na vyombo vya habari nchini, Waziri Jaffo alivikosoa pia vyama vya siasa kwa kile alichokiita kushindwa kuwaelekeza wagombea wao namna nzuri ya kujaza fomu za kuomba kuteuliwa katika nafasi wanazogombea kwenye mitaa, vitongoji na vijiji.

"Inaonesha vyama vya siasa vilishindwa kuwasimamia wagombea wao wakati wa kujaza fomu hizo, kwa maana makosa mengine yalionekana ni kama ya mtu alijaza ili kushindwa mapema." Hilo alilitoa wakati anazungumzia suala la vyama vya siasa kujitoa kwenye uchaguzi huo, lakini vyama vilivyojitoa vilisimama kidete na kupinga mchakato mzima wa uchaguzi.

Uchaguzi Serikali za mitaa

Chanzo cha picha, Eagan Salla BBC

Maelezo ya picha, Uchaguzi Serikali za mitaa

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na vyombo vya habari mwanzoni mwa mwezi Novemba alibainisha kuwa chama chake kimeshuhudia wagombea wake wote katika Mkoa wa Mwanza wakielezwa kukosa sifa. Mbowe alisema takribani wagombea 1,000 walienguliwa na wasimamizi wa uchaguzi huo.