Siasa za Tanzania: Kujitoa uchaguzi serikali za mitaa ni mwisho wa uvumilivu wa chama cha siasa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo
Maelezo ya picha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo alisema kuwa mamlaka ya uchaguzi imetoa nafasi ya wazi kwa wote bila pingamizi
    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Jumla ya vyama vinane vimejitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho, Novemba 24, nchini Tanzania ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya nchi hiyo kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu.

Uchaguzi huo hufanyika chini ya Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba ya Tanzania kuwa ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kuwa ndiyo msingi wa mamlaka yote iliyonayo serikali hupata kutoka kwa wananchi.

Vyama vilivyotangaza kujitoa kushiriki kinyang'nyiro cha uchaguzi huo ni Chadema, UMD, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD, ACT-Wazalendo, CUF na Chauma.

Uamuzi wao umetokana na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya umma na kukilaumu chama tawala CCM kuwa chanzo cha kuvurugika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu nchini.

Licha ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jaffo, mwenye dhamana ya uchaguzi huo kutoa matamko mawili yenye nia ya kuviomba vyama vya upinzani kulegeza misimamo yao na kuwataka wagombea walioteuliwa kuendelea na uchaguzi huo, lakini hapakuwa na mafanikio yoyote.

Vyama vya kisisasa vyakosolewa

Katika taarifa yake iliyokaririwa na vyombo vya habari nchini, Waziri Jaffo alivikosoa pia vyama vya siasa kwa kile alichokiita kushindwa kuwalekeza wagombea wao namna nzuri ya kujaza fomu za kuomba kuteuliwa katka nafasi wanazogombea kwenye mitaa,vitongoji na na vijiji.

"Inaonesha vyama vya siasa vilishindwa kuwasimamia wagombea wao wakati wa kujaza fomu hizo, kwa maana makosa mengine yalionekana ni kama ya mtu alijaza ili kushindwa mapema." Hilo alilitoa wakati anazungumzia suala la vyama vya siasa kujitoa kwenye uchaguzi huo, lakini vyama vilivyojitoa vilisimama kidete na kupinga mchakato mzima wa uchaguzi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na vyombo vya habari mwanzoni mwa mwezi Novemba alibainisha kuwa chama chake kimeshuhudia wagombea wake wote katika Mkoa wa Mwanza wakielezwa kukosa sifa. Mbowe alisema takribani wagombea 1,000 walienguliwa na wasimamizi wa uchaguzi huo.

Freeman Mbowe
Maelezo ya picha, Freeman Mbowe kiongozi wa chama cha upinzani Chadema

Mbowe alisema wagombea waliochukua fomu na kurudisha ni asilimia 60 kati ya 85. Asilimia 25 ya wagombea wa Chadema walioteuliwa na chama walinyimwa fomu. Katika mkoa wa Dar es salaam Chadema walikuwa na wagombea 570, waliopitishwa 24.

Vilevile katika vijiji 12,319 Chadema walisimamisha wagombea asilimia 78 sawa na wagombea 50,218 katika vitongoji,mitaa na vijiji.

Aidha, chama cha ACT-Wazalendo chenyewe kilishuhudia wagombea wake zaidi ya 200 wakiondolewa kwenye kinyang'anyiro hicho na baadhi yao wakiambiwa chama chao hakijasaliwa msajili wa vyama vya siasa.

Malalamiko mengine yaliyotolewa yaliyotolewa na vyama vya upinzani, ni wagombea wao kufanyiwa hujuma wakati wa kurudisha fomu, wasimamizi wa uchaguzi kuzikimbia ofisi.

Mkoa wa Dar es salaam unatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa katika mitaa miwili pekee, baada ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa baada ya kuenguliwa wagombea wa vyama vya upinzani.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole aliviambia vyombo vya habari kuwa malalamiko ya vyama vya upinzani yametokana na uzembe wa viongozi wao

"Usipowekeza katika elimu kwa wagombea wako hayo ni makosa ya kawaida, ndio maana CCM iliweka mawakili na wanasheria 1250 ili kushirikiana na wagombea wa chama hiki katika ujazaji wa fomu za mchakato wa uchaguzi huu," Polepole alikaririwa na gazeti la kila siku la Mwananchi.

wapinzani

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa chama upinzani cha CHADEMA

Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo amemwambia wmandishi wa makala haya, "Ni uamuzi sahihi (kujitoa kwenye uchaguzi wa serikali za Mitaa mwaka 2019) kwa sababu tayari wagombea wa upinzani walikuwa wameenguliwa katika maeneo mengi bila sababu za msingi,".

Uchaguzi huo una maana gani kwa Watanzania?

Sheria ya serikali za mitaa iliundwa mwaka 1982 chini ya Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sheria Na.7 ya Mwaka 1982 (Sura ya 287 ya Sheria za Nchi Marejeo ya Mwaka 2002) na Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sheria Na.7 ya Mwaka 1982 (Sura ya 288 ya Sheria za Nchi Marejeo ya Mwaka 2002);

Serikali za Mitaa nchini zimeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 (1) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Madhumuni na kazi za Serikali za Mitaa yameainishwa chini ya Ibara ya 146 ya Katiba, ambapo ni vyombo vya haki na vyenye mamlaka ya kushiriki na kushirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma katika sehemu zao ili kuchochea maendeleo.

Ifahamike uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ni matakwa ya kikatiba na demokrasia, ambayo wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu ya masuala ya umma.

Kwa mujibu wa Ibara ya 146(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali za Mitaa zitakuwa na majukumu ya kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi, kuimarisha demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Je demokrasia imedidimia?

Tangu kuingia uongozi wa serikali ya awamu ya tano mwaka 2015 kumeshuhudiwa hekaheka za kisiasa ambazo zimeendelea kuwapoteza wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Fursa ya uchaguzi wa serikali za mitaa ilitarajiwa kuwa eneo ambalo vyama vya upinzani vingetumia kujiimarisha na kuwa huru kufanya siasa, lakini wamejikuta wakipata pigo kwa wagombea wao kuenguliwa.

Wabunge na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wanakabiliwa na kesi mahakamani.

Septemba 12 mwkaa huu, mahakama iliwapata na kesi ya kujibu maafisa tisa wa ngazi ya juu wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa Freeman Mbowe.

Naye Kiongozi Mkuu wa chama ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amekuwa akikumbana na rungu la vyo bo vya dola baada ya mikutano yake kuzuiwa mara kwa mara, huku Katibu wake, Ado Shaibu akiwa na rekodi za kukamatwa na Polisi wakati wa kuandaa mikutano ya kiongozi wake mkuu na wanahabari.

Hali hiyo inajenga dhana kana kwamba wanasiasa wa upande wa upinzani si watu wema na kwamba hawana sifa ya kuheshimiwa kama viongozi wengine wa taasisi nchini, na kuimarisha fikra kuwa viongozi wanaotakiwa kuthaminiwa ni wale wlaioko kwenye chama tawala cha CCM pekee.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa fursa za viongozi wa kuchaguliwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uchaguzi zimekuwa zikikumbana na rungu la vyombo vya dola huku vikitoa sababu mbalimbali. Na sasa kamata kamata ya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani inaonekana kuwa jambo la kawaida, lakini lenye madhara makubwa kwa jamii na kisiasa.