Air Tanzania yapigwa marufuku kuruka anga ya Ulaya

Chanzo cha picha, Air Tanzania
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 2
Ndege za Kampuni ya Air Tanzania zimepigwa marufuku kufanya safari katika anga za Umoja wa Ulaya (EU) kufuatia wasiwasi wa kiusalama uliotolewa na Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA).
Hatua hii imefikiwa kwa mashirika ya ndege ambayo hayajafikia viwango vya kimataifa vya usalama.
Kapuni hiyo ya ndege imeongezwa kwenye orodha ya mashirika 129 yaliyopigwa marufuku, ikitajwa kuwa na mapungufu makubwa ya kiusalama yaliyosababisha pia kunyimwa ruhusa ya kufanya kazi kama 'Third County Operator (TCO).
Mashirika mengine yaliyotajwa ni pamoja na Air Zimbabwe, Fly Baghdad, na Iran Aseman Airlines, huku mashirika mawili ya Air Koryo la Korea Kaskazini na Iran Air yakiruhusiwa kufanya safari katika anga za EU kwa kutumia aina maalum ya ndege.
Apostolos Tzitzikostas ambaye ni Kamishna wa masuala ya Usafiri na Utalii wa EU anasema, " Uamuzi wa kuingiza Air Tanzania kwenye Orodha ya Usalama wa Anga ya EU unaonesha dhamira yetu ya dhati ya kuhakikisha viwango vya juu zaidi vya usalama kwa abiria barani Ulaya na duniani kote…
"… tunawahimiza Air Tanzania kuchukua hatua za haraka na za ufanisi kushughulikia masuala haya ya usalama. Nimependekeza msaada kwa mamlaka za Tanzania ili kuboresha utendaji wa usalama wa Air Tanzania na kufikia viwango vya kimataifa vya anga."
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Ulaya, lengo ni kuhakikisha kiwango cha juu kabisa cha usalama wa anga kwa watokao Ulaya na abiria wote duniani kote ikiwa ni sera ya usalama inayopaswa kuzingatiwa.
Kati ya mashirika 129 yaliyopigwa marufuku, 100 yaliidhinishwa katika mataifa 15 ambayo hayana usimamizi mzuri wa mamlaka zao za kitaifa za anga, na mashirika 29, ikiwemo Air Tanzania, yametajwa kwa mapungufu maalum ya kiusalama.
Hata hivyo, Shirika la Ndege la Pakistan International Airlines (PIA) limeondolewa marufuku ya kufanya safari katika anga za EU baada ya kusimamishwa kwa miaka mitatu.
EASA imelisifu shirika hilo pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Pakistan (PCAA) kwa kufanya maboresho makubwa katika utendaji wa usalama.
Je hilo ni pigo kwa Air Tanzania?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Watanzania mitandaoni wamesema kuwa uamuzi huo ni pigo kubwa kwa mpango wa kampuni hiyo kupanua shughuli zake za kimataifa, hasa barani Ulaya.
Air Tanzania, maarufu kama "The Wings of Kilimanjaro," limekuwa likijitahidi kujitanua kama shirika la ndege linaloongoza katika ukanda wa Afrika, likiwa na mipango kabambe ya kupanua huduma zake kimataifa.
Shirika hilo ni mwanachama aliyethibitishwa wa IATA, na linaendesha safari za kimataifa kwenda China, India, UAE, Oman, na Afrika Kusini. Pia linafanya safari kwenda Zambia, Kenya, Visiwa vya Comoro, Zimbabwe, Uganda, Rwanda, Msumbiji, Ethiopia, DRC, Burundi, na lina zaidi ya safari 10 za ndani ya nchi.
Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema kuwa Air Tanzania iko katika hatua za kupanua safari zake kwenda Ulaya na kwamba hakuna vizuizi vinavyokwamisha mchakato huo kwa sasa.
Msigwa alisema, "Tupo katika hatua mbalimbali za kuanza safari za kwenda Ulaya, hakuna vizuizi vinavyoathiri mchakato kwa sasa."












