Uchambuzi: Kwanini Trump amemchagua Makamu wa Rais wa Maduro badala ya mshindi wa Nobel

.

Chanzo cha picha, REUTERS/Leonardo Fernandez Viloria TPX IMAGES OF THE DAY

    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, Diplomatic correspondent
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Maswali mengi yameibuka tangu matukio makubwa ya wikendi yajiofanyika jijini Caracas - kuna moja ambalo limesalia midomoni mwa watu na linamhusu mwanamke ambaye sasa anaongoza kile ambacho maafisa wa Marekani wanakiita "mamlaka mpito ya Venezuela."

Mbona Delcy?

Ni kitu gani kumhusu Delcy Rodríguez, naibu wa rais wa kiongozi wa kiimla Nicolas Maduro, ambacho kimevuti utawala wa Trumpa?

Na kwa nini Washington imeamua mwanamapinduzi aliyejidhihirisha kuwa "Chavista" kusalia madarakani, badala ya kumuunga mkono kiongozi wa upinzani, María Corina Machado, ambaye vuguvugu lake la upinzani linaaminika kuwa lilishinda uchaguzi wa urais wa 2024?

Jibu, kulingana na balozi mmoja wa zamani wa Marekani nchini Venezuela, ni rahisi.

"Wameamua kuchukua mkondo huo kwa ajili ya utulivu badala ya demokrasia," anasema Charles Shapiro, ambaye aliwahi kuwa balozi wa George W Bush nchini Venezuela kuanzia 2002-04.

"Wameweka utawala wa kidikteta bila dikteta. Wafuasi bado wapo."

"Nadhani ni hatari kama kuzimu."

Lakini njia mbadala, unaohusisha kuondoa kabisa serikali iliyopo madarakani na kuunga mkono vuguvugu la upinzani la Machado, ungeleta hatari nyingine, ikiwa ni pamoja na migogoro inayoweza kutokea miongoni mwa viongozi wa upinzani na kutengwa kwa Wavenezuela - pengine kama 30% - ambao walimpigia kura Maduro.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika mkutano na waadhidi wa habari Jumaosi asubuhi, Rais Trump aliwashutua waangalizi wengi kwa kumpuuza mshidi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Machado akisema hana sifa ya "kuheshimiwa" ndani ya Venezuela, huku akimtaja Rodríguez kama "mnyenyekevu."

"Nilishangaasana kusikia kauli ya Rais Trump dhidi ya María Corina Machado," Kevin Whitaker, naibu mkuu wa zamani wa ujumbe katika ubalozi wa Marekani mjini Caracas, anasema.

"Vuguvugu lake lilichaguliwa kwa wingi... kwa hivyo ukihoji uwezo wa Machado kwa kwa kigezo cha sifa, kwa kweli, umepuuza vuguvugu zima."

Kasi iliyotumika kumuondoa Maduro na kumuweka Rodríguez inawafanya baadhi ya waangalizi kuhisi kuwa makamu wa rais wa zamani huenda alikuwa katika mpango huo.

"Inatoa taswira ya kwamba tulimtaka Maduro tu lakini makamu wa rais amenusurika," afisa wa zamani wa CIA Lindsay Moran anasema.

"Ni dhahiri kwamba kulikuwa na vyanzo vya ngazi ya juu vilivyotoa taarifa. Kwa mtazamo wangu vyanzo hivyo vilikuwa katika ofisi ya Makamu wa Rais, la sivyo Makamu wa rais mwenyewe alihusika."

Lakini Phil Gunson, mchambuzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la kufuatilia Migogoro ICG mwenye makao yake mjini Caracas, anasema nadharia ya usaliti haina msingi ikichunguzwa kwa makini, ikizingatiwa kwamba uwezo mkubwa bado uko kwa waziri wa ulinzi wa Venezuela, Jenerali Vladimir Padrino Lopez, na waziri wa mambo ya ndani mwenye msimamo mkali, Diosdado Cabello, wote washirika waaminifu wa Maduro.

"Kwa nini amsaliti Maduro, na kujiweka katika hali ya hatari ndani ya nchi dhidi ya watu ambao wanadhibiti silaha," Gunson anauliza.

Badala yake, uamuzi wa kumuunga mkono Rodríguez ulifuatiwa na onyo kwamba kumweka madarakani Machado kunaweza kusababisha ukosefu wa utulivu.

Mnamo Oktoba, ripoti ya ICG ilionya kwamba "Washington inapaswa kuwa makini linapokuja suala la mabadiliko ya serikali."

"Hofu ya ghasia kuzuka katika hali yoyote ya baada ya Maduro hazipaswi kupuuzwa," ripoti hiyo ilihimiza, ikisema baadhi ya vikosi vya usalama vinaweza kuanzisha vita vya kuvizia dhidi ya mamlaka mpya.

"Tulikuwa tukiwatahadharisha watu katika utawala, kwa hatua hii haitafanya kazi," Gunson anasema. "Kutakuwa na machafuko makali, itakuwa kosa lako na huna budi kukubali lawama."

Siku ya Jumatatu, jarida la Wall Street Journal liliripoti kuwepo kwa tathmini ya kijasusi ya Marekani iliyoainishwa na kufikia hitimisho sawa na kubainisha kuwa wanachama wa utawala wa Maduro, akiwemo Rodríguez, walikuwa katika nafasi nzuri ya kuongoza serikali ya muda.

Ikulu ya White House haijatoa kauli yoyote hadharani kuhusu ripoti hiyo, lakini iliweka wazi kuwa inapanga kufanya kazi na Rodríguez siku zijazo.

"Inakinzana na uhalisia unaokabili utawala wa Trump, anasema Henry Ziemer, mtafiti wa masuala ya Amerika Kusini katika Kituo cha Washington cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.

Lakini changamoto, anasema, ndiyo kwanza zimeanza.

"Kuchukuliwa kwa Maduro ilikuwa sehemu rahisi. Ujenzi wa Venezuela, miundo mbinu wa ya mafuta, kukabiliana na dawa za kulevya na kuimarisha demokrasia…itachukua muda zaidi kutimiza.

Kwa sasa, Rodríguez anaonekana kuwa mtu ambaye utawala wa Trump unahisi kuwa unaweza kumdhibiti.

"Amefanya mageuzi kidogo ya kiuchumi," Gunson anasema. "Anafahamu hitaji la kupanuliwa kwa uchumi na hapingi wazo la kuejesha mtaji wa kigeni."

Ziemer anakubali kwamba Rodríguez anaweza asipate ugumu wa kufanya zabuni ya Washington linapokuja suala la kupokea makampuni ya mafuta ya Marekani, kutoa ushirikiano mkubwa katika kukabiliana na madawa ya kulevya na hata kupunguza uhusiano wa Venezuela na Cuba, China na Urusi, hasa kama itasaidia kuondolewa kwa hatua kwa hatua ya vikwazo vya Marekani.

"Nadhani anaweza kufanya hivyo," anasema.

"Lakini ikiwa Marekani intaka maendeleo ya kweli kuelekea mabadiliko ya kidemokrasia, hiyo itakuwa ngumu zaidi."

Kwa sasa, hili halionekani kuwa ya juu katika orodha ya vipaumbele vya Washington.

Katika hotuba yake kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alizungumzia mpango wa hatua tatu kwa Venezuela, kuanzia kwa utulivu wa nchi hiyo na uuzaji wa mapipa milioni 30-50 ya mafuta chini ya usimamizi wa Marekani.

Mpango huo ungesababisha kile Rubio alichokiita "mchakato wa upatanisho", ikiwa ni pamoja na msamaha kwa vikosi vya upinzani, kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa na kujenga upya mashirika ya kiraia.

"Awamu ya tatu, bila shaka, itakuwa ya mpito," alisema, bila kufafanua.

Ibara ya 233 ya katiba ya Venezuela inataka uchaguzi mpya ufanyike ndani ya siku 30 baada ya rais "kutoweza kabisa kuhudumu," jambo ambalo linaweza kutimia kwa kuwa Maduro anazuiliwa katika jela ya New York, akisubiri kuhukumiwa.

Lakini katika mahojiano na kituo cha habari cha NBC News siku ya Jumatatu, Rais Trump alisema uchaguzi haupo kwenye mipango ya hivi karibuni. "Lazima tuweke nchi sawa kwanza," alisema. "Huwezi kuwa na uchaguzi."

Gunson anasema uamuzi wa Washington wa kutofuatilia mabadiliko ya utawala katika muda mfupi unaweza kuwa na maana, lakini kukosekana kwa matarajio ya muda mfupi au mrefu kunakatisha tamaa.

"Trump anaweza kunufaika kutoka na hili, lakini Wavenezuela hawatapata lolote," anasema. "Wanavenezuela wa kawaida wataendelea kukaza buti kama kawaida."

Huku utawala wa Trump ukizungumzia matarajio ya makampuni ya kimataifa ya mafuta kuwekeza tena katika miundombinu mibovu ya petroli ya Venezuela, Gunson anasema kiuhalisia hili linaweza kuwa mchakato mgumu zaidi.

"Hakuna mtu atakayeingia hapa na mabilioni ya dola zinazohitajika...kuanza mchakato wa kurejesha miundo mbinu hiyo ikiwa serikali ni haramu na hakuna utawala wa sheria," anasema.

Wakati kiongozi wa zamani wa Venezuela Hugo Chávez alipomteua Nicolás Maduro kuwa mrithi wake, muda mfupi kabla ya kifo chake mwaka wa 2013, hatua hiyo ilielezwa kama "dedazo" ya Chavez, neno la Kihispania linalomaanisha "kunyoosha kidole," upako wa kibinafsi ambao unapuuza mchakato wa kawaida wa kidemokrasia.

Balozi Shapiro anaona Delcy Rodríguez pia ameingia madarakani vivyo hivyo.

"Hii ni dedazo ya Trump," anasema.