'Mimi ni mfungwa wa kivita' - Yaliyojiri Maduro alipofikishwa mahakamani

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Madeline Halpert
- Nafasi, Mahakamani New York
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Milio ya pingu za miguu ilisikika muda mfupi kabla ya kiongozi wa Venezuela Nicolás Maduro kuingia kwenye mlango wa mahakama ya Jiji la New York kwa mara ya kwanza.
Aligeuka na kuwaambia waandishi wa habari na watu wengine waliokuwa ukifuatilia tukio hilo kwamba "amekamatwa".
Dakika chache baada ya kuingia mahakamani, Jaji Alvin Hellerstein alimtaka Maduro kujitambulisha ili kesi ianze.
"Mimi ni, bwana, Nicolás Maduro. Mimi ni rais wa Jamhuri ya Venezuela na nimetekwa nyara tangu Januari 3," aliiambia mahakama kwa utulivu akitumia lugha ya Kihispania kabla ya mkalimani kutafsiria mahakama alichosema. "Nilikamatwa nyumbani kwangu huko Caracas, Venezuela."
Jaji mwenye umri wa miaka 92 alimkatiza na kumwambia Maduro kwamba kutakuwa na "wakati na mahali pa kuangazia haya yote".
Maduro na mke wake, Cilia Flores, walikana mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya umiliki na silaha, katika kikao hicho cha mahakama ambacho kilidumu kwa dakika 40 hivi Jumatatu mchana.
"Sina hatia. Mimi ni mtu na heshima zangu," Maduro alisema, huku Flores akiongeza kuwa "hakuwa na hatia kabisa".
Maduro aliye na umri wa miaka 63 na mke wake walifikishwa katika jela ya New York baada ya kukamtwa na vikosi vya Marekanikwenye makaazi yake nchini Venezuela siku ya Jumamosi, katika operesheni yakushtukiza ya usiku wa manane iliyoshuhudia pia mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi.
Wakiwa wamevalia mashati ya jela ya rangia ya bluu na machungwa na suruali ya kaki, wawili hao walivalia vipokea sauti vya masikioni ili kusikiliza tafsiri ya Kihispania wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, huku wakili akiwa ameketi kati yao. Maduro alinakili maelezo ya kina kwenye karatasi ya rangi ya njano ambayo alimwomba hakimu athibitishe kwamba angeweza kubaki naye baada ya kesi kusikilizwa.

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati Maduro alipoingia katika chumba cha mahakama - mahali pale pale ambapo Sean "Diddy" Combs alishitakiwa miezi michache iliyopita - aligeuka na kutikisa kichwa kama ishara ya kuwasalimu watu kadhaa waliokuwa wamehudhuria kesi.
Alidumisha utulivu bila kuonyesha hisia wakati wa kesi, hadi mwishoni, wakati mtu aliyekuwa akifuatilia kutoka kwenye eneo la umma ghafla aliposema kwa sauti Maduro "atalipia" uhalifu wake.
"Mimi ni rais na mfungwa wa vita," alimjibu kwa sauti mtu huyo kwa Kihispania. Baadaye mwanamume huyo alitolewa nje ya chumba hicho huku akitokwa na machozi.
Kesi hiyo ilikuwa ya hisia kwa wengine waliokuwa mahakamani. Mwandishi wa habari Maibort Petit, kutoka Venezuela ambaye ameangazia utawala wa Maduro, alisema mashambulizi ya makombora ya Marekani wakati wa kukamatwa kwa Maduro yaliharibu nyumba ya familia yake karibu na Fuerte Tiuna huko Caracas.
Alisema ilikuwa jambo la kusisimua kumuona kiongozi wake wa zamani akisindikizwa mahakamani akiwa amevalia vazi la gereza na akiongozwa na walinzi wa Marekani.
Mke wa Maduro, Flores, alikuwa mtulivu zaidi, akiwa na bandeji karibu na macho yake na paji la uso kutokana na majeraha ambayo mawakili wake walisema alipata wakati wa kukamatwa kwao wikendi.
Aliongea kwa upole huku nywele zake ndefu zikiwa zimefungwa kwenye fundo huku mawakili wake wakiomba apewe matibabu yanayofaa, ikiwa ni pamoja na kupigwa picha ya mbavu huenda imechibuka na kuvunjika.
Maduro na mkewe hawakuomba dhamana wakati wa kesi hiyo, lakini wanaweza kufanya hivyo baadaye, kumaanisha kuwa wataendelea kuzuiliwa nchini humo.
Marekani imemshutumu Maduro kwa ugaidi na ulanguzi wa mihadarati, njama ya kuingiza dawa za kulevya aina ya cocaine, njama ya kumiliki bunduki na vifaa vya uharibifu.
Maduro alishtakiwa pamoja na mkewe, mwanawe na wengine kadhaa. Kesi hiyo imepangiwa kusikilizwa tena Machi 17.

















