Kwa nini Iran ilipoteza udhibiti wa anga yake "haraka"?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa takriban wiki mbili wakati wa vita kati ya Israel na Iran, anga la Iran lilikuwa likidhibitiwa na Israeli na, wakati mwingine, ndege za kivita za Marekani katika vita hivyo vilivyodumu kwa takriban siku 12.
Wakati mwengine mashirika ya habari ya Iran yalichapisha ripoti ambazo hazikuthibitishwa kuhusu kudunguliwa kwa ndege za kivita za Israel bila ushahidi wowote.
Kwa mtazamo wa kwanza, ilionekana kwamba Iran ilipoteza vita hivyo katika kulinda anga yake, hatua ambayo ina athari kubwa za kijeshi, kisiasa na kiusalama hususan katika vita vya kisasa.
Je, ni nini kilichotokea wakati huo?
Saa 72 baada ya mashambulizi ya Israel kuanza, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitangaza udhibiti kamili wa anga ya Tehran, hatua iliofungua njia kwa mashambulizi makali ya Israel yaliosababisha uharibifu mkubwa katika vituo vya nyuklia vya Iran.
Kwa mujibu wa jeshi la Israel, mapema siku ya Ijumaa ya, Juni 13, ndege 200 za kivita zilitumwa Iran na kushambulia maeneo 100 yaliofufungua anga ya Iran.
Maafisa kadhaa wakuu wa jeshi la Iran waliuawa katika mashambulizi hayo.
Israel ilikuwa imetishia mara kwa mara kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran, huku baadhi ya maafisa wakisema kwamba chaguzi zote zilikuwa zinawezekana na kwamba hakukuwa na pingamizi yoyote.
Mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa Israel Seth Frantzman anasema: "Iran ilipoteza udhibiti wa anga yake kwa sababu ni nchi kubwa yenye mfumo wa ulinzi uliopitwa na wakati, na mifumo yake mipya na ya kisasa zaidi iliripotiwa kuharibiwa katika shambulio la Israel Oktoba mwaka jana."
Mnamo Oktoba 2024, iliripotiwa kuwa Israeli ilikuwa imelenga idadi ya mifumo ya ulinzi ya ardhi hadi angani ya S-300.
Bw. Frantzman anasema Iran ina mifumo mbalimbali ya ulinzi, ikiwa ni pamoja na mifumo ya zamani ya miaka ya 1970, ambayo haifanyi kazi dhidi ya ndege za kivita za kizazi cha tano za Israel.
Je, Iran ilishangaa?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shambulio la Israel dhidi ya Iran lilijiri huku duru nyingine ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani ikipangwa kufanyika. Kwa sababu hii, wengine wanasema shambulio hilo halikutarajiwa.
Hii ni licha ya kwamba maafisa wa kijeshi wa Tel Aviv wanasema walikuwa wakipanga shambulio hilo kwa miaka mingi.
Lakini hata kama Iran ingejitayarisha kwa shambulio hili, mifumo yake ya ulinzi isingeweza kukabiliana na teknolojia ya hali ya juu ya Jeshi la Wanahewa la Israel, shambulio lililoegemea teknolojia ya kisasa zaidi ya silaha zilizotengenezwa na Marekani na Israel.
Mkurugenzi wa Kundi la Ujasusi la Jane's Defence Intelligence, Nick Brown, anasema hata kama Iran ingekuwa tayari kwa shambulio hilo, haingebadili matokeo.
Anasema Iran imekuwa katika hali ya tahadhari kwa miaka mingi, lakini vifaa vya kivita vya kielektroniki vya Israel vilizima rada za Iran na kuizuia Iran kuratibu ulinzi wake.
"Anga ya Tehran ilianguka chini ya udhibiti wa Israeli mapema na kwa gharama ya chini kuliko nilivyotarajia," ni jibu la Michael Eisenhower, mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Kijeshi na Usalama ya Taasisi ya Near East Studies' Military.
Anasema, "Israel ilionyesha kuwa inaweza kuzima ulinzi wa Iran kwa mashambulizi kutoka anga ya Iraq na Syria, na sasa inaruka kwa urahisi juu ya anga ya Iran kwa ndege za siri na zisizo za siri.

Chanzo cha picha, Getty Images
Vita visivyo na usawa wa teknolojia
Iran ni nchi ya 18 kwa ukubwa duniani, takriban mara 75 ya ukubwa wa Israel. Ulinzi wake wa anga lazima uchukue eneo kubwa, na wataalam wa kijeshi wanasema nchi hiyo haina uwezo wa hali ya juu na teknolojia ya kulinda anga yake.
Iran ina idadi ya ndege za kivita za Marekani zilizonunuliwa wakati wa utawala wa Shah, ndege yenye uwezo wa juu zaidi wakati huo ilikuwa F-14 Tomcat, pamoja na ndege za kivita za Urusi.
Katika siku chache zilizopita, jeshi la Israel limetoa picha inazodai kuwa ililenga ndege za kivita za Iran kwenye hangars zao.
Mapema mwaka huu, Iran ilionyesha mfumo wa makombora wa masafa marefu wa S-300 wa urusi wa kutoka ardhini hadi angani na mfumo wa ulinzi wa anga wa Bavar-373 katika gwaride lake la kijeshi ili kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, Michael Eisenstadt wa Taasisi ya Washington ya Masomo ya Near East anasema: "Bavar-373 haionekani kuwa na ufanisi.
Wairani wanapenda kulinganisha Bavar-373 na S-300, lakini ulinganisho huo hauonekani kuwa wa kweli.
Anasema kuwa Israel ilivunja kabisa uwezo wa kiulinzi wa Iran.
Kinyume chake, Israel ina mojawapo ya vikosi vya anga vyenye uwezo wa juu zaidi na vyenye uzoefu duniani. Jeshi la anga la Israel lina vitengo vya ndege za kivita za F-35.
Lockheed Martin anaunda F-35I, iliyopewa jina la "Adair," kwa ajili ya Tel Aviv. Ni ndege ya kivita ya kizazi cha tano iliyo na uwezo maalum wa kukwepa rada.
Israel inasemekana kununua takriban ndege arobaini na tano za "Adair" kutoka kwa Marekani.
Kwa uharibifu wa mfumo wa ulinzi wa Iran, inasemekana kuwa ndege za kivita za Israel F-15 na F-16 pia zilitumika katika operesheni hiyo.
Nick Brown wa Taasisi ya Ulinzi ya Jane anasema kwamba baaada ya Iran kushindwa kuzuia Jeshi la Wanahewa la Israeli kuruka kwa uhuru juu ya ardhi yake, Israel iliendelea kushambulia shabaha zake kwa uhuru na ilivyotaka.
Twitter, yenye uhusiano na Jeshi la Wanahewa la Israel, mara kwa mara ilichapisha picha za mashambulizi ya israel nchini Iran, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kurushia makombora.
Hesabu za Israel na makombora ya Iran
Ikikabiliwa na vikwazo vikali vya kimataifa, Iran kwa miaka mingi imekuwa ikiendeleza mpango wake wa makombora, huku maafisa wakisema walikuwa wakitafuta kupanua uwezo wao wa "kuzuia".
Iran inasemekana kuwa bado ina idadi kubwa ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani, lakini inaonekana kupoteza uwezo wa kuyatumia ipasavyo kufuatia mashambulizi ya Israel.
Ili taifa hilo kuimarisha ulinzi wake , sasa litalazimika kununua mifumo mipya ya anga.
Imetfasiriwa na Seif Abdalla












