'Tulidhani ndio mwisho wetu’: Mji wa Israel ulioshambuliwa vibaya na Iran

DX

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Alice Cuddy
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Muda mfupi kabla ya kusitishwa kwa mapigano kati ya Iran na Israel, wakaazi wa mji wa Beersheba kusini mwa Israel waliamshwa mapema siku ya Jumanne na mlio wa ving'ora vya tahadhari kwenye simu zao.

"Tahadhari ya hali ya juu," ujumbe ulisomeka, ukionya kuhusu makombora yanayokaribia. Kisha ving'ora vilisikika mitaani.

Kama wengine, Merav Manay na familia yake walielekea kwenye chumba chao cha usalama – chumba kilichojengwa kwa zege na mlango mzito wa chuma ili kuwalinda dhidi ya mashambulizi ya roketi.

Kombora la Iran lilipopiga, walihisi jengo linayumba na walifunika vichwa vyao kwa mikono.

"Lilikuwa na nguvu sana hadi tulidhani ndio mwisho wetu," alisema.

FC

Chanzo cha picha, EPA

Walipotoka kwenye chumba hicho, madirisha ya mbele ya ghorofa yao yalikuwa yamepasuka na vigae viko chini ya sakafu kutokana na mlipuko wa kombora. Lakini wao walibaki salama.

Merav alikaa ndani ya ghorofa hiyo kwa masaa kadhaa, akiogopa kile ambacho angekiona nje.

Kando ya barabara tu, jengo kama lao, lilishambuliwa moja kwa moja na kuporomoka kiasi.

Baada ya shambulio hilo, madaktari wa Israel na wanajeshi walikimbilia Beersheba kuokoa manusura. Wafanyakazi wa kujitolea na wakazi wa eneo hilo pia walitoa msaada.

"Natumai huu ndio mwisho," mwanaume mmoja aliiambia BBC alipokuwa akitazama uharibifu huo.

Israel na Iran

FC

Chanzo cha picha, EPA

Israel na Iran zote zilithibitisha baada ya shambulio la Beersheba kwamba wamekubali kusitisha mapigano, lakini wakashutumiana kwa ukiukwaji.

Wakazi wa Beersheba walipokuwa wakikimbia na mshtuko kutokana uharibifu katika jamii yao, pia walihoji kama mapatano hayo yatadumu.

Siku ya Jumanne alasiri, Oren Cohen, 45, akiwa katika bustani yake iliyoshambuliwa, alisema. "Nilikuwa na wasiwasi kuhusu watoto wangu.”

Oren alikuwa na mke wake na watoto watatu - wenye umri wa miaka minane, 12 na 15 - wakati shambulio lilipopiga.

Alipokuwa akizungumza, kikundi cha wafanyakazi wa kujitolea kilifika kusaidia katika kusafisha.

RD
Maelezo ya picha, Oren Cohen

Hata baada ya kuathirika moja kwa moja, Oren anasema anaunga mkono mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran ambayo yalianzisha vita vya siku 12.

"Nadhani hatukuwa na chaguo lingine," alisema. "Tunafanya kile tunachopaswa kufanya ili kujilinda."

Alisema hajui kama usitishaji mapigano utadumu, lakini anaamini serikali ya Israel inajua jinsi ya kufikia malengo yake.

Wakati Merav akiondoka nyumbani kwake Jumanne kwa mara ya kwanza kwenda kutazama uharibifu katika jamii yake, yeye pia alisema anaamini Israel haikuwa na chaguo ila kuipiga Iran.

"Tulikuwa tayari kwa hili," alisema.