Sayari ya buluu inayochemka kwa nyuzi joto 1,000 na kunuka kama yai bovu

Chanzo cha picha, ROBERTO MOLAR CANDANOSA/JOHNS HOPKINS UNIVERSITY
Sayari hii iliyo nje ya Mfumo wa Jua ilikuwa tayari inajulikana kwa hali ya hewa yake mbaya ya jua kali. Lakini sifa yake nyingine iliyogundulika hivi karibuni, ni kutoa harufu mbaya kama mayai yaliyooza.
Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani walitumia taarifa kutoka Darubini ya Anga ya juu ya James Webb ili kuchunguza sayari inayojulikana kama HD 189733 b, yenye ukubwa wa Jupiter.
Angahewa ya sayari hii ina hidrojeni sulfidi, molekuli ambayo husababisha harufu kali kwa mayai yaliyooza na gesi tumboni kwa binaadamu.
"Ikiwa pua yako inaweza kuishi kwenye nyuzi joto 1,000 ° C, anga yake inanuka kama mayai yaliyooza," anasema Dk. Guangwei Fu, mwanaastrofizikia wa Johns Hopkins ambaye aliongoza utafiti huo.
HD 189733 b ni miaka 64 tu ya mwanga kutoka duniani na ndiyo sayari ya karibu zaidi ambayo wanaanga wanaweza kuiona wakipita mbele ya nyota yake.
“Wanasayansi wanafanya uchunguzi wa sayari hiyo tangu ilipogunduliwa mwaka 2005,” anasema Dkt. Fu.
Sayari hiyo iko karibu mara 13 karibu na nyota yake, kuliko Mercury ilivyo karibu na Jua na inachukua takribani siku mbili tu za dunia kukamilisha mzunguko mmoja.
Ina joto kali la takribani nyuzi joto 1,000 °C, fuwele zinazong’aa na upepo wa zaidi ya kilomita 8,000 kwa saa.
"Hatutafuti maisha"

Chanzo cha picha, ROBERTO MOLAR CANDANOSA/JOHNS HOPKINS UNIVERSITY
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ugunduzi wa hidrojeni sulfidi kwenye HD 189733 ni mojawapo ya ugunduzi wa kwanza wa hidrojeni sulfidi kwenye sayari ya nje.
Ingawa gesi hiyo ni mojawapo ya gesi zinazoonyesha kwamba sayari za mbali zinaweza kuwa na viumbe, watafiti hawatafuti uhai kwenye sayari hii kwa sababu ya joto kali, kama Jupita, ilivyo na joto sana.
"Hatutafuti uhai kwenye sayari hii kwa sababu ina joto sana, lakini kupata hii gesi ni hatua kubwa kuelewa jinsi sayari tofauti tofauti zinavyoundwa," anasema Fu.
Mbali na kugundua gesi hiyo, wanasayansi wanatafiti gesi nyingine katika sayari hiyo: oksijini, maji, kaboni dioksidi na kaboni monoksidi.
"Sulfuri ni muhimu kwa ajili ya kujenga molekuli, kama vile kaboni, nitrojeni, oksijeni na fosfeti, wanasayansi wanahitaji kuichunguza zaidi ili kuelewa jinsi sayari zinavyoundwa na zinatengenezwa na nini," anasema Fu alisema.
Sayari kubwa zenye barafu, kama vile Neptune na Uranus, zina chuma kingi zaidi, kuliko chuma kipatikanacho kwenye sayari kubwa kama vile Jupita na Zohali, sayari kubwa zaidi katika mfumo wa jua.
Uwepo wa chuma unaonyesha kwamba Neptune na Uranus zilikusanya barafu nyingi, miamba na vitu vingine vizito vinavyohusiana na gesi kama vile hidrojeni na heliamu wakati wa kipindi cha awali.
“Wanasayansi wanataka kubaini ikiwa vitu hivyo pia vipo kwenye sayari ya HD 189733, anaeleza Fu.
"Sayari hii iko karibu sana na dunia na imechunguzwa sana," anaongeza mwanasayansi huyo.
Darubini ya mapinduzi

Chanzo cha picha, NASA, ESA, CSA, NORTHROP GRUMMAN
Darubini ya James Webb imefungua dirisha jipya la uchanguzi wa kemikali kwenye sayari za mbali, kusaidia wanaanga kujifunza zaidi kuhusu asili ya sayari hizo.
"Ni kweli imeleta mapinduzi katika nyanja ya unajimu. Imefanya kile tulichokitarajia na imevuka matarajio yetu katika nyanja hii," anasema Dk Fu.
Katika miezi ijayo, timu ya Fu inapanga kutumia data kutoka darubini ya angani kufuatilia salfa katika sayari nyingi zaidi.
Utafiti huo wa Dkt. Fu na timu yake ulichapishwa katika jarida la Nature.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












