'Sisi si wanajeshi - kwa nini wanatushambulia?'

dfc

Chanzo cha picha, Goktay Koraltan

Maelezo ya picha, Mohammed, 29, aliungua vibaya baada ya shambulio la Israel katika kijiji chake kusini mwa Lebanon
    • Author, Orla Guerin
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati shambulio la anga lilipotokea, Mohammed alikuwa akiwagawia chakula cha moto majirani zake watu wazima – amekuwa akifanya hivyo yeye na marafiki zake tangu Israel ilipovamia Lebanon tarehe 1 Oktoba.

Ni mhandisi wa ujenzi, 29, alikuwa amesimama umbali wa mita 5 (16ft) kutoka mlipuko ulipotokea, ambao uliharibu nyumba katika kijiji anachoishi kusini mwa Lebanon.

Tabaka ya juu ya ngozi iliungua kwenye paji lake la uso na mashavu, na kuacha uso wake mbichi na rangi ya waridi. Mikono yake pia iliungua moto. Tumbo lake lina majeraha ya moto ya kiwango cha tatu. Wiki mbili baadaye, anasimulia hadithi yake.

"Kulikuwa na kiza, moshi kila mahali," anasema kwa sauti ya chini. "Ilichukua kama dakika moja. Kisha nikaanza kutambua kilicho karibu nami. Niligundua marafiki zangu wawili walikuwa bado hai lakini wanavuja damu nyingi. Ilichukua dakika tano watu kututoa nje.”

Mohammed anasimulia mambo ya kutisha akiwa katika kitanda katika hospitali ya serikali ya Nabih Berri, ambayo iko kwenye kilele cha mlima huko Nabatieh. Ni mojawapo ya miji mikubwa zaidi kusini, na kilomita 11 tu kutoka mpaka na Israel. Kabla ya vita watu wapatao 80,000 waliishia hapa.

Mohammed anasema hapakuwa na onyo kabla ya shambulio hilo - "si kwetu, si kwa majirani zetu, si kwa mtu ndani ya nyumba iliyoshambuliwa."

Mtu ambaye aliuawa katika shambulio hilo alikuwa polisi, anasema

“Sisi si wanajeshi,” anasema, “sisi si magaidi. Kwa nini tunashambuliwa? Maneno ambayo yanasemwa na na kila raia.

Mohammed atarudi nyumbani kijijini kwake, Arab Salim, atakapotolewa, ingawa bado mashambulizi yanaendelea. “Sina mahali pengine pa kwenda,” anasema. “Kama ningeweza [kuondoka] ningefanya hivyo.”

Pia unaweza kusoma

Kijiji cha Arab Salim

l

Chanzo cha picha, Goktay Koraltan

Maelezo ya picha, Dr Wazni inabidi atafute mafuta ili jenereta za hospitali ziendelee kufanya kazi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati tunapoitembelea hospitali hivyo, shambulizi jingine la anga, linawafanya wafanyakazi kukimbilia kwenye roshani, kuangalia wapi pameshambuliwa. Wanaona moshi wa kijivu unaofuka kutoka eneo la umbali wa kilomita 4.

Muda mfupi baadaye, chini ya ghorofa katika chumba cha dharura, kilio cha king'ora kinaonya juu ya majeruhi wanaowasili - kutoka katika shambulio hilo la anga. Lilipiga kijiji cha Mohammed, Arab Salim.

Mwanamke anaingizwa ndani ya machela huku damu zikimtoka. Anafuatwa na mumewe, ambaye anagonga ukuta kwa kufadhaika kabla ya kuanguka kwa mshtuko.

Ndani ya dakika chache mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Hassan Wazni, anawaambia wafanyakazi kuwa mshipa mkuu unaosafirisha damu kati ya moyo na mwili umepasuka na lazima apelekwe kituo maalumu cha mishipa katika hospitali kaskazini.

Hospitali hii hupokea majeruhi 20-30 kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel kwa siku. Wengi ni raia, lakini hakuna mtu anayegeuzwa. "Tunachukua wagonjwa wote, na wote waliojeruhiwa, na mashahidi wote wanaokuja," anasema. "Hatubagui."

Dkt. Wazni hajaondoka hospitalini hapa tangu vita vianze. Nyuma ya meza yake katika ofisi yake, anafungua pakiti ya sigara. "Nadhani ni sawa kuvunja sheria fulani katika vita," anasema kwa tabasamu la kuomba msamaha.

Anatatizika kulipa mishahara na kuja na lita 1,200 za mafuta kwa siku kuendesha jenereta za hospitali. "Hatupati chochote kutoka serikalini," anasema.

Hospitali hii ina vitanda 170, Nabih Berri ndio hospitali kuu ya umma katika mji huu, lakini sasa ina wafanyikazi wa mifupa tu, na wagonjwa 25. Wagonjwa na majeruhi wanaoletwa hapa wanahamishwa haraka hadi hospitali ya maeneo salama zaidi Kaskazini.

Wafanyakazi wanasema kumekuwa na "mashambulizi mengi" karibu na Nabih Berri.

Soko la Urithi

k

Chanzo cha picha, Goktay Koraltan

Maelezo ya picha, Mfanyakazi wa ulinzi wa raia Hussein Jaber anasema droni za Israel zinapaa juu ya mji wa Nabatieh kila wakati

Jengo la manispaa hiyo lililipuliwa wiki mbili zilizopita na kusababisha kifo cha Meya Ahmad Kahil na wengine 16. Wakati huo alikuwa kwenye mkutano wa kuratibu usambazaji wa misaada. Tunapopita karibu na magofu, vifusi na mabakia yanaonekana na ambulensi iliyoharibika.

Shambulio hilo kubwa liliangusha majengo kadhaa ya jirani - mtaa wa jiji hilo umepoteza mandhari yake.

Pia soko la zama za Ottoman – nalo liliharibiwa siku hiyo hiyo. Karne za historia zilivunjwa na kuwa vifusi, urithi ukageuka kuwa vumbi.

Soko hilo la zamani, lilipendwa na Hussein Jaber, 30, naye anatoa huduma za dharura. Yeye na wenzake, baadhi yao wakiwa wakujitolea, wanatupeleka huko kwa ziara fupi. Wanaendesha kwa kasi – katika barabara pekee ya kusafiri huko Nabatieh.

"Tulizaliwa na kukulia hapa," Hussein anasema. “Tumekuwa hapa tangu tukiwa watoto. Soko hili lina maana kubwa sana kwetu. Inasikitisha sana kuona liko hivi. Linahifadhi kumbukumbu za siku za nyuma na siku nzuri za watu wa jiji hili.”

Kama Dk Wazni, Hussein na wenzake wamebaki kuhudumia watu, licha ya hatari. Zaidi ya watoa huduma za awali 110 na wahudumu wa kwanza wameuawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon katika mwaka uliopita, kulingana na takwimu za serikali ya Lebanon - wengi wao katika mwezi uliopita.

Baadhi ya mashambulizi ni "dhahiri ni uhalifu wa kivita,’ kulingana na kundi la kimataifa la haki za binaadamu, Human Rights Watch.

Hussein alipoteza mfanyakazi mwenzake na rafiki mwezi huu, katika shambulio la anga la mita 50 kutoka kituo chao cha ulinzi wa raia, ambapo wanalala. Aliyekufa, ni Naji Fahes, alikuwa na umri wa miaka 50 na alikuwa na watoto wawili.

"Alikuwa na shauku na nguvu na alipenda kusaidia wengine," Hussein ananiambia. "Ingawa alikuwa mzee kuliko sisi, yeye ndiye alikuwa akikimbia kwenda kuokoa, kuwa pamoja na watu."

Wakati shambulio la anga lilipotokea, Naji Fahes alikuwa amesimama nje ya kituo, tayari kutoa msaada.

Wakati Hussein akizungumza tunaona ndege isiyo na rubani ya Israeli inazunguka angani, kisha inashuka zaidi. "Nadhani iko juu yetu moja kwa moja sasa. Pengine inatutazama,” anasema.

Majibu ya IDF

k

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Shambulio la anga la tarehe 16 Oktoba liliharibu soko la Nabatieh, pamoja na majengo ya manispaa

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilituambia "linafanya mashambulizi tu dhidi ya kundi la kigaidi la Hezbollah, sio dhidi ya wakazi wa Lebanon."

Israel inasema mapambano yake ni "dhidi ya kundi la kigaidi la Hezbollah, lililojiweka ndani ya maeneo ya raia na miundombinu."

Israel inasema "inachukua hatua nyingi kupunguza madhara dhidi ya raia ikiwa ni pamoja na kutoa onyo la mapema," ingawa onyo halikutolewa katika shambulio la anga lililomjeruhi Mohammed, au shambulio lililomuua meya.

Saa tano na nusu katika jiji hili lililokuwa na shughuli nyingi tuliona watu wawili tu nje, wakitembea kwa miguu. Wote wawili walikimbia, hawakutaka kuzungumza nasi.

Wakati wa ziara yetu ndege isiyo na rubani ilikuwa ikitangaza ujumbe kutoka jeshi la Israel - kuwaagiza watu kuondoka mara moja.

Inakadiriwa kuwa kuna watu mia kadhaa tu waliosalia ambao hawataki au hawawezi kuhamia kwingine. Hasa ni wazee na maskini, na wataishi au kufa pamoja na jiji lao.

Na Hussein na timu yake watakuwa hapa, kuja kuwasaidia. "Tutakaa hapa, na tutaendelea. Tutakuwa karibu na raia. Hakuna kitakachotuzuia.”

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi