Lebanon: 'Waajiri wangu walinifungia nyumbani na kuondoka Israel ilivyoanza kudondosha mabomu'

Wafanya kazi wengi wa ndani ambao ni raia wa kigeni hawana pa kwenda kutafuta usaidizi
Maelezo ya picha, Wafanya kazi wengi wa ndani ambao ni raia wa kigeni hawana pa kwenda kutafuta usaidizi
    • Author, Manal Khalil & Ethar Shalaby
    • Nafasi, BBC News Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati shambulio la anga la Israeli lilipopiga nyumba ya mwajiri wake kusini mwa Lebanon, Andaku (si jina lake halisi) alijikuta peke yake, akiwa amejifungia ndani.

Mwanamke huyo Mkenya mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akifanya kazi nchini Lebanon kama kijakazi kwa muda wa miezi minane iliyopita, lakini anasema mwezi uliopita umekuwa mgumu zaidi huku jeshi la Israel likizidisha mashambulizi dhidi ya kile ambacho kimesema ni malengo ya Hezbollah kote nchi.

“Kulikuwa na milipuko mingi ya mabomu. Waajiri wangu walinifungia ndani ya nyumba na kuondoka ili kuokoa maisha yao wenyewe," aliambia BBC Idhaa ya Kiarabu.

Sauti za milipuko zimemwacha Andaku na kiwewe. Amepoteza kumbukumbu ya siku ngapi aliachwa peke yake ndani ya nyumba kabla ya waajiri wake kurudi.

“Waliporudi walinitupa nje. Hawakuwahi kunilipa na sikuwa na pa kwenda,” anasema, akiongeza kuwa alikuwa na bahati ya kuwa na pesa za kutosha kupata basi kwenda mji mkuu, Beirut.

Si Andaku sio pekee aliyejipata katika hali kama hiyo.

Ijumaa iliyopita, maafisa wa Umoja wa Mataifa walisema makazi mengi ya karibu 900 yaliyopangwa na serikali ya Lebanon yamejaa kufuatia kuongezeka kwa mzozo wa Israel na Hezbollah, na kuelezea wasiwasi wao kuhusu maelfu ya wafanyikazi wa nyumbani wengi wao wakiwa wanawake nchini humo.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, kuna wafanyakazi wahamiaji 170,000 nchini Lebanon. Wengi wao ni wanawake kutoka Kenya, Ethiopia, Sudan, Sri Lanka, Bangladesh na Ufilipino.

"Tunapokea ripoti zinazoongezeka za wafanyikazi wa nyumbani kutelekezwa na waajiri wao wa Lebanon, ama kuachwa mitaani au majumbani mwao huku waajiri wao wakikimbia," Mathieu Luciano, mkuu wa ofisi ya IOM nchini Lebanon, aliambia mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva.

Takriban wafanyakazi wahamiaji 170,000 wanaishi nchini Lebanon, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM)
Maelezo ya picha, Takriban wafanyakazi wahamiaji 170,000 wanaishi nchini Lebanon, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM)
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wafanyakazi wengi wa nyumbani wahamiaji wanahamia Lebanon ili kusaidia familia zao.

Wastani wa mshahara wa kila mwezi kwa wafanyikazi wa ndani wa Kiafrika unakadiriwa kuwa karibu dola 250, huku wale wanaotoka Asia wakilipwa hadi dola 450.

Wafanyakazi wa ndani wahamiaji wanapaswa kutii mfumo wa Kafala (ufadhili) nchini Lebanon, ambao hauwahakikishii haki zinazolindwa kwa wafanyakazi wahamiaji, na unaruhusu waajiri kuwanyang'anya pasi zao za usafiri na kuwanyima mishahara yao. Wanapata kazi kupitia mashirika ya ndani.

"Kukosekana kwa ulinzi wa kisheria ndani ya mfumo wa Kafala, pamoja na harakati zenye vikwazo, inamaanisha wengi wanaweza kunaswa katika mazingira ya unyonyaji. Hii imesababisha matukio ya unyanyasaji, kutengwa, na kiwewe cha kisaikolojia miongoni mwa wafanyakazi wahamiaji,” anasema msemaji wa IOM Joe Lowry.

"Zaidi ya hayo, tumepokea visa vya wahamiaji kufungiwa ndani ya nyumba za raia wa Lebanon ambao wanakimbia, kuangalia mali zao," anaongeza.

Hakuna mahali pa kwenda

Mina (pia sio jina lake halisi) anatoka Uganda na amekuwa mfanyakazi wa ndani nchini Lebanon kwa mwaka mmoja na miezi minne.

Anaiambia BBC kuwa alidhulumiwa na familia aliyokuwa akifanyia kazi na kuamua kutoroka na kurejea katika shirika lake.

Akitumaini angepokea msaada, Mina alisema alishtuka kujua kwamba alilazimika kufanya kazi kwa familia nyingine kwa mkataba wa miaka miwili kabla ya kurejea nyumbani.

“Niliporudi kwa [wakala], niliwaambia nimefanya kazi ya kutosha kuweza kulipia tikiti yangu na kurudi nyumbani. Walichukua pesa zangu na kuniomba nifanye kazi katika nyumba nyingine kwa miaka miwili ili niweze kusafiri nyumbani,” kijana huyo wa miaka 26 anasema.

Kuishi na sauti zinazoendelea za milipuko kulisababisha afya ya akili ya Mina kuathiriwa. Hakuwa na uwezo wa kufanya kazi zake za ndani ipasavyo, kwa hiyo akamwomba mwajiri wake mpya aondoke.

Alikuwa akifanya kazi kwa familia huko Baalbek, jiji lililo katika Bonde la Bekaa kaskazini-mashariki mwa Lebanon.

“[Familia] ilikuwa imenipiga, ikanisukuma na kunitupa nje... Kulikuwa na mabomu mengi sana wakati huo. Nilipoondoka, sikuwa na pa kwenda,” anasema.

Mfanyakazi mwingine wa ndani kutoka Kenya, Fanaka, 24, anasema wakala wake ungemtuma kufanya kazi katika nyumba tofauti kila baada ya miezi miwili na kwamba alikuwa akiumwa na kichwa mfululizo.

"Nimekuwa nikijaribu kufanya kazi vyema kadri ya uwezo wngu lakini hakuna mtu anayezaliwa mkamilifu," anasema.

Moshi ukifuka katikati ya uhasama unaoendelea kati ya Hezbollah na vikosi vya Israel, kama inavyoonekana kutoka Tiro, kusini mwa Lebanon, Oktoba 7, 2024.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mashambulizi ya anga ya Israel yamepiga mji wa kusini wa Tiro na maeneo yanliyo karibu

Wanawake hao wanasema walikabiliwa na changamoto nyingi walipokuwa wakiishi mitaani, kwani makazi mengi yalikataa kuwapokea, wakidai yametengwa kwa ajili ya Walebanon waliokimbia makazi yao na sio wageni.

Wote watatu walifanikiwa kufika Caritas Lebanon, shirika lisilo la kiserikali ambalo limekuwa likitoa msaada na ulinzi kwa wafanyikazi wahamiaji tangu 1994.

Katika rekodi za sauti zilizotumwa kwa BBC, wafanyikazi wahamiaji kutoka Sierra Leone walisema baadhi ya waliobaki wamekwama katika mitaa ya Beirut na walikuwa wakihitaji sana chakula.

Wengine waliambia vyombo vya habari vya ndani kwamba walizuilliwa kuingia kwenye makazi yaliyopangwa na serikali shuleni kwa sababu hawakuwa Walebanon.

BBC iliwasiliana na viongozi wa eneo hilo, ambao walikanusha kuwepo kwa aina yoyote ya ubaguzi.

Vyanzo kutoka wizara ya elimu viliiambia BBC: "Hakuna vituo maalum ambavyo vimetengwa kwa ajili ya wafanyakazi wa ndani kutoka mataifa ya kigeni, lakini wakati huo huo, hawajazuiliwa kuingia."

Inafahamika kuwa baadhi ya wafanyikazi wanakwepa makazi rasmi, wakihofia athari kutokana na kutokamilika kwa nyaraka zao za kisheria.

Hessen Sayah Korban, mkuu wa idara ya ulinzi katika Caritas Lebanon, anasema Shirika Lake lisilo la kiserikali kwa sasa linawahifadhi wafanyakazi 70 wa ndani ambao ni wahamiaji, wengi wao ni akina mama walio na watoto.

Anasema ufadhili zaidi unahitajika ili kuweza kutoa makazi kwa hadi wafanyakazi 250 wa ndani ambao wametelekezwa na waajiri wao au hawana makazi na wanyang'anywa nyaraka zao rasmi.

“Tunajaribu kuwapa msaada wowote unaohitajika; iwe ni wa kisheria, kiakili au kimwili.”

Anaongeza kuwa wafanyakazi wengi wa nyumbani wanahitaji msaada wa afya ya akili kwa sababu wameumia.

Tangu mwanzoni mwa Oktoba, IOM imepokea zaidi ya maombi 700 mapya kutoka kwa watu wanaotafuta usaidizi wa kurejea katika nchi zao za asili.

Bi Korban anasema Caritas, pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, inawasaidia wafanyakazi wa nyumbani waliotelekezwa wanaotaka kuondoka kwa kuratibu na IOM, balozi na balozi mbalimbali, na huduma za usalama za Lebanon.

Maelezo zaidi:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi