Netanyahu aionya Lebanon na ‘uharibifu kama wa Gaza'

Chanzo cha picha, REUTERS
- Author, David Gritten
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Waziri Mkuu wa Israel ametoa wito wa moja kwa moja kuwataka watu wa Lebanon kuindoa Hezbollah na kuepuka "uharibifu na mateso kama huko Gaza."
Ombi la Benjamin Netanyahu la siku ya Jumanne lilikuja wakati Israel ikipanua uvamizi wake wa ardhini dhidi ya Hezbollah kwa kutuma maelfu ya wanajeshi katika eneo jipya kusini-magharibi mwa Lebanon.
Netanyahu pia alidai kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF), limemuua mrithi wa kiongozi wa zamani wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, lakini IDF baadaye ilisema haiwezi kuthibitisha kifo cha Hashem Safieddine.
Siku ya jana wapiganaji wa Hezbollah waliendelea kurusha makombora kuelekea mji wa bandari wa Israel wa Haifa kwa siku ya tatu mfululizo, na kuwajeruhi watu 12.
Wakati wa hotuba ya video iliyotolewa kwa watu wa Lebanon, Netanyahu anasema: "Muna fursa ya kuiokoa Lebanon kabla haijaanguka kwenye hali mbaya ya vita vya muda mrefu ambavyo vitasababisha uharibifu na mateso kama tunavyoona huko Gaza.
"Nawaambia, watu wa Lebanon: Komboeni nchi yenu kutoka kwa Hezbollah ili vita hivi viweze kumalizika."
Hezbollah imeendelea kuleta upinzani licha ya wiki tatu za mashambulizi makali ya Israel ambayo maafisa wa Lebanon wanasema yameua zaidi ya watu 1,400 na wengine milioni 1.2 kuwa wakimbizi.
Mapema Jumanne naibu wa zamani wa Hassan Nasrallah, Naim Qassem, alisisitiza kuwa Hezbollah imeshinda mashambulizi makali ya hivi karibuni ya Israel na uwezo wake bado ni imara.”
Israel imefanya mashambulizi baada ya takribani mwaka mzima wa mapigano ya mpakani yaliyosababishwa na vita huko Gaza, ikisema inataka kuhakikisha usalama kwa maelfu ya wakaazi wa maeneo ya mpakani mwa Israel waliofurushwa na mashambulio ya roketi na ndege zisizo na rubani za Hezbollah.
Mashambulizi yameongezeka kwa kasi tangu Hezbollah ilipoanza kurusha maroketi kaskazini mwa Israel ili kuwaunga mkono Wapalestina tarehe 8 Oktoba 2023, siku moja baada ya shambulio baya la mshirika wake Hamas katika eneo la kusini mwa Israel.
Uvamizi wa Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku ya Jumanne asubuhi, IDF ilitangaza kwamba askari wa akiba walianza "operesheni kusini-magharibi mwa Lebanon.”
Kuna vikosi vitatu vya jeshi katika maeneo ya kati na mashariki mwa Lebanon tangu uvamizi huo kuanza tarehe 30 Septemba - inaripotiwa idadi ya wanajeshi waliotumwa ni zaidi ya 15,000.
IDF inasema wanajeshi wamechukua udhibiti wa kile walichokiita eneo la mapigano la Hezbollah katika kijiji cha mpakani cha Maroun al-Ras na kuchapisha picha zinazoonyesha kile inachosema ni eneo la kurushia roketi kwenye shamba la mizeituni, pamoja na silaha na vifaa ndani ya jengo la makazi.
Picha za droni zimeonyesha uharibifu mkubwa katika kijiji cha karibu cha Yaroun, ambacho kilikuwa shabaha ya kwanza ya uvamizi huo.
Wakati huo huo, mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Lebanon na mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa alionya kwamba athari za kibinadamu za mzozo huo "ni janga kubwa."
Serikali ya Lebanon imesema takribani watu milioni 1.2 wamekimbia makazi yao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Watu 180,000 wako katika vituo vilivyoidhinishwa vya waliokimbia makazi yao.
Zaidi ya watu 400,000 wamekimbilia Syria iliyokumbwa na vita, wakiwemo wakimbizi zaidi ya 200,000 wa Syria - hali ambayo mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi alieleza ni ya “kusikitisha."
Shirika la Mpango wa Chakula la Dunia linasema kuna “wasiwasi kuhusu uwezo wa Lebanon wa kuendelea kujilisha” kwa sababu maelfu ya hekta za mashamba ya kilimo yamechomwa moto au kutelekezwa.
IDF pia ilisema ndege zake zilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Hezbollah katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, ambapo kundi hilo lina ngome zake, na maeneo mengine ya Lebanon siku ya Jumanne.
Pia imetangaza kuwa mashambulizi katika mji mkuu siku ya Jumatatu, umemuua kamanda wa makao makuu ya Hezbollah, Suhail Husseini.
Hezbollah haikutoa kauli yoyote kuhusu madai hayo. Lakini iwapo itathibitishwa, itakuwa ni pigo la hivi punde zaidi katika mfululizo wa mapigo makali ambayo Israel imetoa kwa kundi hilo, huku Hassan Nasrallah na wengi wa makamanda wake wa kijeshi wakiwa wameuawa katika mashambulizi kama hayo ya hivi karibuni.
Bado Hezbollah iko imara?

Chanzo cha picha, AFP
Hashem Safieddine, afisa wa ngazi ya juu wa Hezbollah anayetarajiwa kumrithi binamu yake Nasrallah kama kiongozi, hajasikika hadharani tangu shambulizi la anga la Israel liliporipotiwa kumlenga huko Beirut siku ya Alhamisi iliyopita.
Msemaji wa IDF, Daniel Hagari alisema siku ya Jumanne jioni kwamba wanajeshi hawajaweza kuthibitisha madai ya Netanyahu na waziri wa ulinzi wa Israel kwamba Safieddine aliuawa katika shambulio hilo, na kuongeza kuwa IDF inachunguza matokeo ya operesheni hiyo.
Naibu kiongozi wa Hezbollah alisema katika hotuba ya runinga kutoka eneo lisilojulikana siku ya Jumanne kwamba kamandi na udhibiti wa Hezbollah ni "imara" na hakuna "nafasi tupu," akitoa mfano wa mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel katika siku za hivi karibuni.
"Tunawaumiza na tutaendelea. Miji mingi bado tunaweza kuishambulia kwa safu za makombora. Tunawahakikishia kuwa uwezo wetu uko vizuri," alisema Naim Qassem.
Lakini, kwa mara ya kwanza, hakutaja kusitishwa vita huko Gaza kama sharti la Hezbollah kuacha kuishambulia Israel – kama ilivyokuwa ikisema huko nyuma.
"Tunaunga mkono juhudi za kisiasa ambazo (Spika wa Bunge la Lebanon) Nabih Berri anafanya kuelekea kusitisha mapigano," Qassem alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni.
"Mara baada ya usitishaji mapigano kufikiwa, diplomasia itafuata."
Haikuwa wazi ikiwa hii inamaanisha mabadiliko katika msimamo wa Hezbollah.
Hotuba hiyo iliambatana na mashambulizi ya zaidi ya roketi 100 kuelekea Haifa Bay, pamoja na mikoa ya Chini, Kati na Juu ya Galilaya.
IDF ilisema roketi nyingi zilinaswa. Hakukuwa na majeruhi makubwa.
Siku ya Jumapili usiku, kulitokea shambulio la moja kwa moja huko Haifa - shambulio ambalo halikuwahi kutokea tangu Israel na Hezbollah kupigana vita mara ya mwisho mwaka 2006.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












