Je, Israel inataka Mashariki ya Kati ya aina gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Alaa Ragaie
- Nafasi, BBC News Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Maneno 'Mashariki ya Kati Mpya' yametumiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Na maafisa wa Israel wameonekana wakiwa wameshikilia ramani za Israel katika majukwaa ya kimataifa na ramani hizo hazina maeneo ya Palestina.
Katika hotuba yake ya hivi karibuni kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri Mkuu wa Israel aliwasilisha ramani mbili, ya kwanza ikiwa na maeneo yenye rangi ya kijani kwa nchi ambazo zina makubaliano ya amani na Israel au ziko katika mazungumzo ya kurekebisha uhusiano wao na Israel; hizo ni Misri, Sudan, UAE, Saudi Arabia, Bahrain na Jordan.
Ramani ya pili ilijumuisha maeneo yaliyotiwa rangi nyeusi, ambayo Netanyahu aliyaita "yamelaaniwa," yakijumuisha Iran na washirika wake: Syria, Iraqi na Yemeni, pamoja na Lebanon.
Katika hotuba ya hivi karibuni ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alionya kuhusu kile alichokiita "malengo yenye chuki ya Israel," akisema, "Watatamani ardhi ya nchi yetu kati ya Tigris na Eufrate na watangaze wazi kupitia ramani zao, hawataridhika na Gaza."
Yezid Sayigh, kutoka kituo cha utafiti wa sera za Carnegie Middle East, haamini kwamba malengo hayo ni dalili nzuri kwa ajenda za Netanyahu.
"Mashariki ya Kati mpya ambayo Netanyahu anajaribu kuitafuta ni kuiwezesha Israel kukoloni maeneo mengine ya Palestina," anasema Sayegh.
Israel haifichi azma yake ya kuendeleza mradi wake wa makaazi, hasa katika Ukingo wa Magharibi, na imetangaza waziwazi nia yake ya kuongeza idadi ya makaazi, licha ya ukosoaji wa kimataifa.
"Kuna mawaziri katika serikali ya mrengo wa kulia ya Israel ambao hawaamini katika suluhu ya mataifa mawili, na sasa uwepo wa taifa la Palestina uko mbali zaidi tangu mapatano ya Oslo mwaka 1993, lakini sidhani kama Marekani itaweza kuunga mkono ramani hizi za Israel - ambazo hazijumuishi maeneo ya Palestina," anasema David Schenker, kutoka Taasisi ya uchambuzi wa sera ya Washington.
"Mtazamo wa Israel kuhusu Mashariki ya Kati mpya ni eneo lisilo na vitisho vya Iran," anasema Schenker.
Mashariki ya Kati bila 'tishio la Iran'

Chanzo cha picha, Getty Images
Akizungumza na BBC, Miri Eisen, mtaalamu wa masuala ya usalama na afisa mstaafu wa ujasusi wa Israel, alisema: “Israel haitafuti kuanzisha Mashariki ya Kati mpya, lakini inataka kuhakikisha utawala wa mullah nchini Iran hautawali kanda hii.”
"Maneno ya Netanyahu yanalenga kukomesha mpango wa nyuklia wa Iran na kurejesha heshima yake baada ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023 ambayo yamemletea aibu duniani," anasema Sayigh.
Mauaji ya Katibu Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah, yanaonekana kama hatua ya mabadiliko katika vita hivyo.
Iran ilirusha safu ya makombora ya balestiki dhidi ya Israel, kwa kutumia aina mbalimbali za silaha ambazo zimezitia hofu nchi za Magharibi kwa muda mrefu, kujibu mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh katika ardhi yake, huku Israel ikiapa kujibu mashambulizi ya Iran.
Suluhisho la kijeshi halitoshi

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Marekani inatoa msaada mkubwa kwa Israel na imezidisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo kutokana na kuongezeka kwa mivutano.
Lakini uungaji mkono huu umewekewa masharti kwa Israel kutovuka mstari mwekundu ambao Washington inarudia katika hotuba zake rasmi, ambazo ni kulenga mradi wa nyuklia wa Iran na suluhisho la mataifa mawili.
Eisen alisema: "Hatua ya kijeshi ya Israel zinazuia Iran kupeleka itikadi na silaha kwa washirika wake, na inalenga kudhoofisha uwezo wa Iran wa kijeshi."
David Schenker, anaamini Israel inaweza kuwa imepiga hatua katika kulemaza 'wawakilishi' wa Iran katika eneo hilo, lakini haiwezi kuunda utaratibu mpya bila ya kuungwa mkono na mataifa ya Kiarabu.
"Hamas inaweza kurudi tena ikiwa hakuna mamlaka ya Palestina na juhudi za nchi za Kiarabu katika diplomasia ya kimataifa, na vile vile Hezbollah bila juhudi za jamii ya Lebanon."
Eisen anaamini Israel inataka kuimarisha ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi na hata wa kiteknolojia na washirika ambao wana mtazamo sawa juu ya "tishio la Iran."
Katika miaka ya hivi karibuni, Washington imekuwa ikiongoza mpango wa kuboresha uhusiano kati ya Israel na majirani zake, ikitoa vishawishi vya kiuchumi na kijeshi na kuendeleza fikra kwamba Israel si tishio kwa Waarabu bali, ni mshirika wa kistratijia katika kukabiliana na Iran.
Morocco, Imarati na Bahrain zimetia saini Makubaliano ya Abraham Accords, lakini uhusiano umekwama tangu shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023 na vita vya Israel-Gaza.
Israel imekuwa ikitaka kuboresha uhusiano na Saudi Arabia ambayo inapinga kuongezeka ushawishi wa Iran yenye Washia wengi katika eneo hilo na inahofia ushawishi wake katika Mashariki ya Kati.
Hata hivyo Saudi Arabia imetangaza rasmi katika makala ya gazeti la Financial Times kwamba nchi hiyo haitaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel hadi pale taifa la Palestina litakapoanzishwa.
Ushirikiano wa kiuchumi

Chanzo cha picha, Reuters
Mikataba na makubaliano yaliyotangazwa kabla ya tarehe 7 Oktoba 2023 yalijumuisha uwekezaji katika ulinzi, usalama wa mtandao, na nishati.
Vita vya tangu tarehe 7 Oktoba 2023 vinaweza kupunguza kasi ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Israel na washirika wake wapya kutoka nchi za Kiarabu, lakini taarifa rasmi kutoka Israel zilifichua kuwa biashara kati ya Israel na nchi tano za Kiarabu iliongezeka katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, ikiongozwa na UAE, Misri, Bahrain na Morocco.
Gazeti la Israel la Maariv lilifichua makubaliano yaliyotiwa saini kati ya UAE na Israel kuanzisha njia ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili, kupitia Saudi Arabia na Jordan, na Misri pia. Gesi ya Israel pia ni chanzo kikuu cha baadhi ya gridi za umeme za Misri.
"Israel lazima iunganishe diplomasia, ushirikiano wa kiuchumi na ulinzi na hatua za kijeshi ili kuunda utaratibu mpya wa kikanda," anasema Schenker.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah








