Wapalestina na Waisraeli wana matumaini huku makubaliano ya kusitisha mapigano yakikaribia

- Author, David Gritten, Paul Adams & Tom Bateman
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wapalestina na Waisraeli wameelezea matumaini yao kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko yanakaribia baada ya miezi 15 ya vita vibaya.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar alisema siku ya Jumanne kwamba hakuna tena masuala makubwa yanayozuia makubaliano kati ya Israel na Hamas na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Doha yako mwishoni ili kufikia makubaliano.
Afisa wa serikali ya Israel amesema mazungumzo hayo yamepiga hatua ya kweli na kuingia katika kipindi muhimu huku Hamas ikisema imeridhishwa na hali ya mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema mpango huo "uko mwishoni" kukamilika.
Wakazi wa Gaza

Chanzo cha picha, Asmaa Tayeh
"Siwezi kuamini kwamba bado niko hai kushuhudia hilo," anasema Sanabel mwenye umri wa miaka 17 katika ujumbe uliotumwa kutoka Gaza City. "Tumekuwa tukingojea hilo tangu mwezi wa kwanza wa mwaka [uliopita]."
Sanabel, anayeishi na familia yake katika nyumba yao iliyoharibiwa, amekiambia kipindi cha OS cha BBC, kila mtu kaskazini mwa Gaza "ana furaha na matumaini ya kuona marafiki zao, kuona familia zao ambazo zimehamishwa kusini mwa Gaza."
"Katika saa za mwisho za vita hivi, sitaki kupoteza mmoja wa wanafamilia yangu. Nataka mapigano yasitishwe kwa muda mrefu - yaani kwa maisha yetu yote."
Asmaa Tayeh, mhitimu anayeishi na familia yake katika nyumba ya babu yake katika kitongoji cha Magharibi mwa Gaza cha al-Nasr, pia amesema watu kwa mara nyingine tena wana matumaini.
Asmaa anatoka Jabalia, kambi kubwa zaidi ya wakimbizi mjini Gaza, ambayo wakazi wake wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel.
Wakati jeshi la Israel lilipoanzisha mashambulizi mapya ya ardhini huko Jabalia mwezi Oktoba, familia ya Asmaa ililazimika kukimbia kwa mara nyingine tena.
Mapigano makali yamezuka huko Jabalia tangu wakati huo. Mwezi Desemba, Asmaa alisema eneo lote "limeharibiwa."
Jamaa wa Mateka

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jamaa za mateka wa Israel walioshikiliwa Gaza tangu Oktoba 2023 pia wamezungumza na BBC kuhusu habari juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Sharon Lifshitz, ambaye baba yake mzee ni miongoni mwa mateka waliosalia Gaza, anasema: "Najaribu kuwa na matumaini. Najaribu kufikiria kuwa makubaliano yatatokea na mateka wote watarudi."
Sharon Lifshitz ni msanii na mtengenezaji wa filamu raia wa Uingereza na Israel ambaye hajui alipo baba yake Oded mwenye umri wa miaka 84.
"Kwetu sisi, tunajua kutakuwa na huzuni nyingi sana. Tunajua wachache kati ya [mateka] hawapo hai tena. Tunatamani walio hai warudi ili waweze kurejea katika familia zao," alikiambia kipindi cha Today.
Anasema mama yake, Yocheved - ambaye pia alitekwa nyara katika shambulio la Oktoba 7, aliachiliwa wiki kadhaa baadaye.
Eyal Kalderon - binamu wa Ofer Kalderon mwenye umri wa miaka 54, ambaye watoto wake wawili walikuwa miongoni mwa mateka 105 walioachiliwa mwezi Novemba - amesema katika ujumbe alioutuma kwa BBC OS: "Tunatumai mpango huo utakamilika hivi karibuni na tutafikia wakati ambapo tunamkumbatia Ofer, na watoto wake wanne wanamkumbatia."
"Tunataka mpango huu ujumuishe mateka wote, mateka wote 98. Tunataka hivyo. Tunatumai kuwaona wote katika ardhi ya Israel."
Lee Siegel - kaka wa Keith Siegel, 64, ambaye mkewe Aviva pia aliachiliwa mwezi Novemba – anasisitiza kuwa: "Mateka wote lazima warudi nyumbani - wale ambao bado wako hai, ili kujenga upya maisha yao na familia zao; marehemu warudi, kwa ajili ya mazishi yanayofaa katika nchi yao."
Mtoto wa Ruby Chen, aitwaye Itay, aliuawa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 2023 na mwili wake unazuiliwa huko Gaza.
"Waziri Mkuu kwa bahati mbaya anaendelea na mpango ambao haujumuishi mwanangu na mateka wengine, na haijulikani mwili wa mwanangu utapatikana vipi," anasema.
Marekani, Israel na nchi za Kiarabu

Chanzo cha picha, Daniel Lifshitz
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia na baadhi watu wa chama chake, wanaopinga kuachiliwa kwa wafungwa na makubaliano mapana ya kusitisha mapigano.
Sharon Lifshitz anasema Waisraeli wengi wanaunga mkono makubaliano hayo, lakini shinikizo la pamoja kutoka kwa Rais anayeondoka wa Marekani, Joe Biden na Rais mteule Donald Trump hatimaye zimeipa serikali ya Netanyahu "msukumo wa ziada."
Akizungumza siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar amesema ana Imani watu wengi katika serikali ya Israel wataunga mkono makubaliano hayo.
Mpango huo huenda ukashuhudia, vikosi vya usalama vya Gaza vitakuwa pamoja na vikosi vingine kutoka nchi nyingine - uwezekano mkubwa ni kutoka mataifa ya Kiarabu pamoja na "vikosi" vya Palestina.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken amesema, Hamas ilijaribu kuanzisha vita vya kikanda na kukwamisha juhudi zinazoongozwa na Marekani za kuunganisha uhusiano wa Israel na majirani zake wa Kiarabu.
Kwa upande mwingine, amesema Israel imefanya mashambulizi ya kijeshi "kupita lengo la kuuharibu uwezo wa kijeshi wa Hamas na kuua viongozi wake waliohusika na shambulio la Oktoba 7.
Anasema hilo ni kama kujiumiza yenyewe, akiongeza kuwa Marekani imetathmini kuwa Hamas imeajiri karibu idadi sawa ya wanamgambo wapya ambao Israel imewaua.
Israel ilianzisha mashambulizi ya kuiangamiza Hamas kujibu shambulio la kundi hilo la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 46,640 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas. Wengi milioni 2.3 pia wamekimbia makazi yao, kuna uharibifu mkubwa, na kuna uhaba mkubwa wa chakula, mafuta, dawa na makazi.
Israel inasema mateka 94 bado wanazuiliwa na Hamas, ambapo 34 kati yao wanakisiwa kufariki. Pia, kuna Waisraeli wanne waliotekwa nyara kabla ya vita, wawili kati yao wamefariki.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallahn na kuhaririwa na Ambia Hirsi












