Vita vya Gaza: Matukio ya kutisha baada ya shambulio la Israel huko Jabalia

- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ukiwa nje ya Gaza, ni vigumu kufahamu ukubwa wa mateso wanayopitia raia wa huko. Siku ya Jumatatu tarehe 21 Oktoba, video iliibuka kutoka Jabalia baada ya mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Gaza.
Kama ilivyo kwa waandishi wengi wa habari ambao wanalazimika kuripoti vita kutoka nje ya Gaza kwa sababu Israel haiwaruhusu kuingia.
Nami hutazama video nyingi zinazoibuka mtandaoni, matukio ya kutisha ya watu waliojeruhiwa, wanaokufa na walio hospitalini, za wanaume kwenye vifusi wakiokoa walionusurika na kufukua miili, na raia waliolazimishwa kuhama wakipita kwenye vifusi vinene na magofu.
Shule ya Msingi ya Wavulana ya Jabalia ilishambuliwa asubuhi, tarehe 21 Oktoba. Haikuwa tena mahali pa kujifunzia, iligeuzwa kuwa makazi ya raia waliokimbia makazi yao, kama vile shule nyingi za Gaza zinazoendeshwa na UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina.
Katika video hiyo, mhudumu wa afya anayeitwa Nevine al Dawawi, anakimbia akipita raia waliokufa na wanaokufa, akitumia simu yake kurikodi kile kinachoendelea.
Tulifanikiwa kumpata Nevine katika Jiji la Gaza. Aliweza kutusimulia yeye mwenyewe kile kilichotokea Jumatatu asubuhi.
'Hakuna mahali salama Gaza'

Chanzo cha picha, Getty Images
Makala hii ina maelezo ya kusikitisha kuanzia hapa!
Nevine alitusimulia juu ya mwanamke ambaye watoto wake waliuawa anayeitwa Lina Ibrahim Abu Namos. Waandishi wa habari wanaofanya kazi na BBC walimpata katika hospitali ya Kamal Adwan huko Jabalia ambako amelazwa akiwa na majeraha. Watoto wawili kati ya saba wa Lina waliuawa, binti yake mkubwa na mwanawe pekee wa kiume.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mumewe hakuwa nao wakati shambulio hilo lilipotokea, alikuwa akitibiwa majeraha katika shambulio la awali.
"Nilimwona binti yangu akifa, kwa macho yangu mwenyewe. Alikuwa anakufa mbele yangu. Sikuweza kuzuia asife, na alikuwa mtoto wangu mkubwa.”
Nevine, mhudumu wa afya, alieleza kuwa walizingirwa shuleni kwa siku 16 au 17. Juu yao kulikuwa na sauti ya droni ndogo zilizotumiwa na Jeshi la Israel, IDF.
Droni hizo ni kwa ajili ya ufuatiliaji na ujasusi, kutoa amri kupitia vipaza sauti, pia hurusha mabomu au kuwafyatulia risasi kwa Wapalestina wanaotaka kuwaua.
"Tulikuwa tunaishi kwa hofu kubwa. Shule iliposhambuliwa, watu waliuawa na kujeruhiwa. Hapakuwa na kitu cha kula wala kunywa pale. Gari la maji lililipuliwa na Israel.
Siku tatu zilizopita, droni ilishuka shuleni saa tatu asubuhi, na kututaka tuondoke saa nne. Kipaza sauti cha droni kilisema tulilazimika kuhama shule kwa sababu tulikuwa katika eneo hatari la mapigano.”
“Hatukuwa na muda wa kubeba vitu vyetu. Ilitupa saa moja tu. Lakini baada ya dakika 10, ndege za Israel zililipua shule hiyo. Yalikuwa mauaji makubwa na zaidi ya watu 30 walijeruhiwa na zaidi ya 10 waliuawa.”
Alituonesha video ya wasichana wakiwa wamekatika vipande vipande. Pia inaonyesha wanaume ambao matumbo yao yametoka nje.
Mvulana mwenye umri wa miaka 10 matumbo yake yametoka nje. Mama yake aliuawa, alijeruhiwa moyoni.
"Baadhi ya wanawake waliokuwa wamejipa hifadhi pia walijeruhiwa na wengine kuuawa. Msafishaji shuleni alikatwa vipande vipande. Msichana wa miaka 12 alilipuliwa mguu,” anasema mtoa huduma huyo.
Siku moja kabla ya shambulizi la shule hiyo, huku mashambulizi ya Israel yakizidi, Tor Wennesland - mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini Jerusalem - alitoa taarifa kali.
“Matukio ya kutisha yanatokea katika eneo la kaskazini, mashambulizi yasiyoisha ya Israel na mzozo wa kibinadamu unazidi kuwa mbaya."
"Hakuna mahali salama Gaza. Nalaani kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya raia. Vita hivi lazima viishe, mateka wanaoshikiliwa na Hamas waachiliwe, kuhamishwa kwa Wapalestina kukome, na raia lazima walindwe popote walipo. Misaada ya kibinadamu lazima ipelekwe bila vikwazo."
Israel inasisitiza inajilinda, na inadai majeshi yake yanaheshimu sheria za vita. Lakini kuhusu Gaza na Lebanon inasema raia wanauawa kwa sababu makundi yenye silaha yanawatumia kama ngao za binadamu.
Ni shambulio halali?

Tunamuuza mhudumu wa afya, Nevine al Dawawi. IDF inadai Hamas inawatumia raia kama ngao za binadamu, ni kweli?
"Hapana, Hamas waikutumia raia kama ngao za binadamu. Walikuwa wakitulinda na kusimama pamoja nasi.”
Kwa wengi nchini Israel, kauli yake kwamba Hamas walikuwa katika eneo hilo itachukuliwa kama sababu ya shambulio baya la IDF dhidi ya raia la siku ya Jumatatu tarehe 21 Oktoba.
Lakini mawakili wa uhalifu wa kivita watauliza ikiwa shambulio hilo ni halali. Sheria za vita zinasema raia lazima walindwe, na mashambulizi dhidi yao yanapaswa kuwa sawa na uzito wa tishio linalokikumba kikosi kinachoshambulia.
Iwapo makamanda wakuu wa Hamas wangekuwepo hapo, au mkusanyiko mkubwa wa wapiganaji wanaojiandaa kushambulia, pengine shambulio hilo lingeweza kuhesabiwa la halali na wanasheria wenyewe wa Jeshi la Ulinzi la Israel.
Lakini kama Hamas, ambayo vikosi vyake vya mapigano vimesambaratishwa ndani ya mwaka mmoja wa mashambulizi ya Israel, uwepo wa wapiganaji wachache wenyeji bunduki katika eneo hilo, huenda shambulio hilo linakiuka sheria.
Ushahidi unaongezeka kwamba Israel imefanya matukio huko Gaza ambayo haitaki waandishi wa habari wayaone, ndiyo maana hawaruhusu tuingie katika eneo hilo, isipokuwa katika ziara za nadra zinazodhibitiwa na jeshi.
Matokeo yake, waandishi wa habari wanategemea video na taarifa zinazotoka kwa Wapalestina ndani ya Gaza, wakiwemo waandishi wa habari, na kutoka kwa wanadiplomasia wa kimataifa, madaktari na wafanyakazi wa misaada ambao wanaruhusiwa kuingia Gaza, na wahudumu kama Nevine.
Akiwa hospitali, Lina Ibrahim Abu Namos anasema: "Mimi naogopa sana, sili wala sinywi, tumehamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hakuna kilichobaki kwangu na mabinti zangu, hakuna mahali salama, mimi ni mmoja tu wa watu wengi ambao hawana pa kwenda, hakuna usalama, nimechoka.”
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












