Wapalestina wanaokimbia Jabalia wanasema miili imetapakaa mitaani

F

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jeshi la Israel lilisema Jumanne kwamba maelfu ya wakaazi wa Jabalia wamehamishwa katika muda wa saa 24 zilizopita.
    • Author, David Gritten
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Wapalestina wanaokimbia mashambulizi ya ardhini ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kaskazini mwa Gaza wametoa maelezo ya kuhuzunisha kuhusu hali ilivyo huko.

Mwanaume mmoja aliambia BBC, aliona maiti zimetapakaa baada ya kuamriwa kuondoka eneo hilo na wanajeshi wa Israel. Mwanamke mwingine amesema baadhi ya watu waliondoka kwa hofu kubwa na kuwaacha watoto wao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina lilitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda ili kuwezesha njia salama kwa familia ambazo bado zinataka kutoroka, huku hospitali mbili za ndani zikionya kwamba hazina vifaa.

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake wanaendelea na operesheni dhidi ya wapiganaji wa Hamas huku wakiwaondoa raia kwa usalama.

Zaidi ya watu 400 wanaripotiwa kuuawa na maelfu wameyakimbia makazi yao tangu jeshi lilipoanzisha mashambulizi ya tatu katika eneo la Jabalia tarehe 6 Oktoba, likisema linawatokemeza wapiganaji wa Hamas waliojipanga tena huko.

Operesheni hiyo imekuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken akielekea Israel kujaribu kufufua mchakato wa kidiplomasia uliokwama juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia huru mateka kutoka Gaza – baada ya mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel ya kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar wiki iliyopita.

Blinken alisisitiza haja ya Israel kuchukua hatua za ziada ili kuongeza mtiririko wa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.

Pia unaweza kusoma

Ushuhuda wa Waliokimbia

Kipindi cha BBC Arabic cha Gaza Today kiliwahoji watu kadhaa waliokimbia makazi yao katika kambi ya Jabalia na kutafuta hifadhi katika kitongoji cha karibu cha Rimal cha Gaza City.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwanaume anayeitwa Saleh anasema "alikwama kwa siku 16" akiishi na familia yake katika Shule ya Msingi ya Wavulana ya Abu Hussein.

Madaktari na wafanyikazi wa uokoaji wanasema zaidi ya watu 20 waliuawa katika shambulio la anga la Israel katika eneo hilo wiki iliyopita. Jeshi la Israel limewataja wapiganaji 18 wa Hamas na Palestina Islamic Jihad siku ya Jumanne kuwa miongoni mwa waliofariki.

"Tulipokea ujumbe kupitia droni za Israel, zikitusihi tuhame, kwa hiyo tukaanza kutembea chini ya uangalizi wa wanajeshi wa Israel, ambao walitutaka tuelekee kusini au magharibi mwa Gaza. Nilikuwa na nyanya yangu, alikuwa hawawezi kutembea, kama wengine wengi."

Mwanaume mwingine, Mohammed al-Danani, anasema alikuwa katika shule hiyo hiyo na "alishuhudia miili ya mashahidi barabarani.”

Engy Abdel Aal anasema alikuwa katika eneo la Bwawa la Abu Rashid wakati droni zikitangaza amri ya watu kuelekea mji wa Beit Lahia, kaskazini mwa kambi hiyo.

"Hali ilikuwa ngumu sana, hakuna mtu aliyejua pa kwenda. Watu wengine walilazimika kukimbia bila watoto wao, na kuwaacha shuleni huku wakitoroka na wengine."

Hali Ilivyokuwa

df

Chanzo cha picha, REUTES

Maelezo ya picha, Watu waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza siku ya Jumatatu

Siku ya Jumanne Jeshi la Israel lilitangaza kuwa wanajeshi wake "wanaendelea na mapigano katika eneo la Jabalia, huku wakiwahamisha raia kutoka eneo la mapigano."

“Maelfu ya raia wamehamishwa. Makumi ya magaidi wamekamatwa kutoka miongoni mwa raia,” lilisema Jeshi kwenye chapisho la X - likijumuisha video inayoonyesha umati wa watu wakitembea katika mitaa iliyoharibiwa.

Jeshi pia lilisema wanajeshi "waliwauwa magaidi 10 ambao walikuwa tishio katika shambulio moja la anga, bila kutoa maelezo yoyote.

Wakati huohuo Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilichapisha video ambayo inasema inaonyesha gari la wagonjwa likisafirisha miili ya watu watano, wakiwemo watoto, waliouawa kwa kushambuliwa na makombora katika mji wa Jabalia siku ya Jumatatu.

Video nyingine iliyorikodiwa siku hiyo hiyo inamwonyesha mhudumu wa afya Nevin al-Dawasah akijaribu kuwasaidia wanaume, wanawake na watoto waliofariki na kujeruhiwa kwenye kambi ya Shule ya Maandalizi ya Wavulana ya Jabalia.

Baada ya kutoroka eneo hilo siku ya Jumanne, Bi Dawasah aliliambia shirika la habari la AFP, “wakati watu wakitii agizo la kuhama na ghafla kulizuka makombora."

"Tulikuwa na mashahidi na waliojeruhiwa na hapakuwa na njia salama kwa ambulensi kuja," anasema.

Jeshi la Israel bado halijazungumzia taarifa hizo.

Wito wa Umoja wa Mataifa

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa), Philippe Lazzarini, anasema wafanyakazi wake kaskazini mwa Gaza wanaripoti kuwa hawakuweza kupata chakula, maji au huduma za matibabu.

"Harufu ya maiti ipo kila mahali kwani miili imeachwa imelala barabarani au chini ya vifusi," aliandika kwenye X. "Watu wanangojea tu kufa. Wanajihisi kutelekezwa, kutengwa, na hawa tumaini."

Bw Lazzarini alitoa wito wa "kusitishwa mapigano mara moja, hata ikiwa kwa saa chache, ili kuwezesha njia salama za kibinadamu kwa familia zinazotaka kuondoka eneo hilo na kufika maeneo salama."

Msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema serikali ya Israel inaendelea kukataa ombi la Ofisi yake ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), kusaidia kuwaokoa raia waliokwama chini ya vifusi na kuwasilisha vifaa vinavyohitajika katika hospitali.

Mkurugenzi wa hospitali ya Indonesia, mojawapo ya hospitali za mwisho zinazofanya kazi karibu na Jabalia, aliambia BBC, wanajeshi wa Israel walisimama nje ya lango na kulikuwa na milio ya risasi mara kwa mara katika eneo hilo.

"Hilo limezua hali ya hofu na kuchanganyikiwa kwa wagonjwa na wafanyakazi wa matibabu," anasema Dk Marwan al-Sultan. "Pia tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta, vifaa vya matibabu, wafanyakazi, chakula na maji."

“Aidha, kukatika kwa umeme kunaendelea kulazimu hospitali kutegemea vyanzo vya nishati mbadala vinavyodumu kwa saa nane hadi 10 pekee. Na hilo linahatarisha usalama wa wagonjwa.”

Dk Sultan pia alikanusha ripoti kwamba kumetokea moto katika hospitali hiyo siku ya Jumatatu, akisema kumetokea moto ndani ya shule iliyo karibu.

Jeshi la Israel limesema linahakikisha hospitali zinafanya kazi wakati wa mashambulizi hayo.

Pia linasema tangu wiki iliyopita zaidi ya malori 230 ya kubeba chakula, maji, vifaa vya matibabu na malazi yamepelekwa kaskazini mwa Gaza kupitia kivuko cha Erez Magharibi, baada ya kipindi cha wiki mbili ambacho UN ilisema hakukupelekwa mahitaji.

Israel ilianzisha operesheni ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 42,710 wameuawa huko Gaza tangu operesheni hiyo kuanza, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah