Nyangumi awashangaza wanasayansi kwa kusafiri kutoka Colombia hadi Tanzania 'kutafuta majike'

Chanzo cha picha, Natalia Botero-Acosta
- Author, Helen Briggs
- Nafasi, Mwandishi wa mazingira, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Nyangumi mwenye nundu amefanya uhamiaji mkubwa na wa kipekee kuwahi kurekodiwa, huenda ukiwa umechochewa na mabadiliko ya tabia nchi, wanasayansi wanasema.
Alionekana katika bahari ya pasifiki karibu na Colombia mwaka 2017, kisha kuzuka tena miaka kadhaa baadaye kisiwani Zanzibar katika bahari hindi - umbali wa kilomita 13,000.
Wataalam wanaamini kuwa safari hii kubwa inaweza kuwa imesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha kupungua kwa hifadhi za chakula au safari ya kutafuta wenza.
Ekaterina Kalashnikova kutoka kwa programu ya mamalia wa baharini Tanzania alisema kwamba tukio hili ni ''la kushangaza na la kipekee hata kwa aina hii ya wanyama wanaohama sana''.
Picha inayofuata hapa chini inaonyesha nyangumi wa nundu aliyepigwa picha mwaka 2022, katika pwani ya Zanzibar.

Chanzo cha picha, Ekaterina Kalashnikova
Dkt.Kalashnikova amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba umbali huu ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa nyangumi aliye na nundu.
Nyangumi mwenye nundu huishi katika bahari zote ulimwenguni.
Husafiri umbali mrefu kila mwaka na wana uhamiaji mrefu zaidi ya mamalia yoyote, wakisafiri kutoka maeneo ya uzalishaji ya kitropiki hadi maeneo ya chakula katika maji baridi.
Lakini safari ya nyangumi huyu dume ilikuwa ya kipekee zaidi ,ikiwa na maeneo mawili mbalimbali ya uzalishaji.
Nadharia moja ni kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanabadilisha wingi wa Krill - aina ya samaki ambao hutumika na nyangumi kama chakula chao hivyobasi kuwalazimu kuhamia bahari to fauti kutafuta chakula hicho.
''Ingawa sababu halisi bado hazijabainika ,lakini uhamiaji wa nyangumi wenye nundu huenda unachochewa na mabadiliko ya tabia nchi , mazingira mabaya ambayo yanatokea kila wakati na mabadiliko ya ya spishi,''anasema Dkt Kalashnikova.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Dume huyu aliyehama alikuwemo katika kundi la nyangumi wenye nundu ambao walinaswa katika picha kutoka kwa meli ya utafiti kwenye pwani ya pasifiki ya Colombia mwaka 2013.
Alitambuliwa tena katika eneo hilo hilo mwaka 2017 - na kando ya Zanzibar mwaka 2022.
Maonyesho haya yanatenganishwa na umbali wa kilomita 13,046 , ikiwa ndio umbali mfupi zaidi ambao nyangumi huyo angeweza kuchukua ,wanasayansi wanasema ,ingawa inawezekana umbali huu ni mrefu zaidi.
Kwa kuwa dunia ni mduara ,njia fupi zaidi kati ya maeneo mawili inatolewa kwa umbali wa mzunguko mkubwa, ambao ni sehemu inayounganisha sehemu mbili kwenye mduara.
Matokeo ya utafiti huu yamejumuisha maelfu ya picha za nyangumi zilizowasilishwa na watafiti , waangalizi wa nyangumi na wanajamii kwa tovuti ya sayansi ya raia ,happywhale.com.
Hifadhi hii hutumia akili mnemba kulinganisha maumbo na mifumo ya mapambo ya mkia wa nyangumi mwenye nundu na hivyo kuorodhesha harakati zao kote duniani.
Utafiti huo umechapishwa katika jarida la sayansi, la Royal Society Open Science.
Pata maelezo zaidi kuhusu nyangumi mwenye nundu katika The Secret's of Antarctica's Giants kwenye BBC iPlayer.

Chanzo cha picha, BBC/Victoria Gill
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Seif Abdalla












