Golikipa wa West Ham, 15, afariki baada ya kuugua saratani

Chanzo cha picha, West Ham United
Golikipa wa shule ya michezo ya West Ham amefariki akiwa na umri wa miaka 15 baada ya kuugua saratani.
Oscar Fairs kutoka Benfleet, Essex, aligundulika kuwa na aina ya uvimbe usio wa kawaida kwenye ubongo wenye ukubwa wa 7cm (2.8in) unaofahamika kama ependynoma, mwezi Agosti 2023.
Alifanyiwa upasuaji mara saba, raundi moja ya matibabu ya mionzi yanayofahamika kama chemotheraphy na radiotherapy, lakini aliambiwa kuwa kitu pekee anachoweza kufanya ni kupata matibabu ya kupunguza maumivu na msongo wa mawazo unaotokana na kuugua maradhi makubwa.
Mkurugenzi wa klabu hiyo ya michezo Mark Noble amesema kuwa “alikuwa na maisha mazuri kwa siku za baadaye, na inasikitisha sana kuwa ameondoka kwa familia na marafiki zake katika umri mdogo.”
Salam za pole kutoka kwa vilabu vingi na wachezaji wengi wa mpira zimekuwa zikitolewa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo kipa wa Real Madrid Thibaut Courtois na nyota wa Liverpool aliyestaafu, Jamie Carragher.
Ukurasa wa kusaidia familia kukusanya £100,000 kwaajili ya gharama za matibabu nchini Ufaransa umefunguliwa.
Kulingana na familia yake, Wachezaji wa timu ya West Ham wamechangia £27,000, huku mwenyekiti wao David Sullivan akichangia £10,000 na mchezaji wa Arsenal na mchezaji wa zamani wa West Ham Declan Rice wakitoa £5,000.
Ratiba zote za shule hiyo ya michezo za mwishoni mwa wiki zimeahirishwa ikiwa kama ishara ya heshima kwa marehemu.















