Korea Kaskazini inajenga 'ukuta' wa mpakani , picha za satelaiti zaonyesha

- Author, Jake Horton
- Nafasi, BBC Verify
- Author, Yi Ma
- Nafasi, BBC Verify
- Author, Daniele Palumbo
- Nafasi, BBC Verify
Korea Kaskazini inajenga sehemu za kile kinachoonekana kuwa ukuta katika maeneo kadhaa karibu na mpaka wake na Korea Kusini, picha mpya za satelaiti zinaonyesha.
Picha zilizochambuliwa na BBC Verify pia zinaonyesha kuwa ardhi ndani ya Eneo lisilo na Kijeshi (DMZ) imeondolewa, jambo ambalo wataalamu wanasema linaweza kuwa ukiukaji wa mapatano ya muda mrefu na Korea Kusini.
DMZ ni eneo linalotenganisha nchi hizo mbili la kilomita 4 (maili 2.5) kati ya Korea Kaskazini na Kusini, ambao bado wako vitani bila kusaini mkataba wa amani. DMZ imegawanyika mara mbili, huku kila upande ukidhibitiwa na mataifa husika.
Shughuli hii ya hivi karibuni ni "isiyo ya kawaida", kulingana na wataalam, na inakuja wakati wa kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili.
"Kwa wakati huu tunaweza kukisia tu kwamba Korea Kaskazini inatazamia kuimarisha uwepo wake wa kijeshi na ngome kwenye mpaka," anasema Shreyas Reddy, mwandishi wa habari katika tovuti maalum ya NK News, iliyoko Seoul.

BBC Verify iliagiza picha za setilaiti zaubora wa juu za kipande cha mpaka cha kilomita 7 kama sehemu ya mradi wa kuangalia mabadiliko ambayo Korea Kaskazini ilikuwa ikifanya katika eneo hilo.
Picha hizi zinaonekana kuonyesha angalau sehemu tatu ambapo vizuizi vimewekwa karibu na DMZ, vinavyochukua jumla ya kilomita 1 karibu na mwisho wa mashariki wa mpaka.
Inawezekana kwamba kumekuwa na ujenzi wa kizuizi zaidi kando ya sehemu zingine za mpaka.
Tarehe kamili ya ujenzi ulipoanza haijulikani kwa sababu ya ukosefu wa picha za awali za ubora wa juu katika eneo hilo. Walakini, miundo hii haikuonekana kwenye picha iliyopigwa mnamo Novemba 2023.
"Tathmini yangu ya kibinafsi ni kwamba hii ni mara ya kwanza wamewahi kujenga kizuizi kwa maana ya kutenganisha maeneo kutoka kwa kila mmoja," Dk Uk Yang, mtaalam wa kijeshi na ulinzi katika Taasisi ya Asan ya Seoul ya Mafunzo ya Sera aliiambia BBC.

"Hapo nyuma katika miaka ya 1990, Korea Kaskazini ilikuwa imeweka ukuta wa kuzuia mizinga ili kuzuia kusonga mbele kwa mizinga iwapo vita vitazuka. Lakini hivi majuzi, Korea Kaskazini imekuwa ikiweka kuta zenye urefu wa m 2-3, na hazifanani na kuta za kuzuia tanki,” Dk Yang anasema.
"Umbo la kuta zinaonyesha kuwa sio tu vizuizi [kwa mizinga], lakini vinakusudiwa kugawanya eneo," anaongeza Dk Yang, ambaye alipitia picha za satelaiti.
Pia kuna ushahidi wa kufyekwa kwa ardhi ndani ya upande wa Korea Kaskazini wa DMZ.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Picha ya hivi punde ya setilaiti ya mwisho wa mashariki wa mpaka inaonyesha kile kinachoonekana kuwa barabara mpya ya kufikia eneo hilo
Katika kuchora mpaka halisi wa kaskazini wa DMZ katika ramani iliyo hapo juu, tumepitisha utafiti wa BBC kuhusu uchoraji wa ramani. Hii ni kwa sababu kuna tofauti kidogo katika ramani zinazopatikana za mpaka. Hata hivyo, matoleo yote ambayo tumepata yanaonyesha kuondolewa kwa msitu katika ardhi kunakofanyika ndani ya DMZ.
Afisa kutoka kwa Uongozi wa pamoja wa Jeshi la Korea Kusini (JCS) alisema katika mahojiano mafupi ya hivi majuzi kwamba jeshi limetambua shughuli inayoendelea kuhusiana na "uimarishaji wa barabara za kimbinu, uwekaji wa migodi na kusafisha maeneo yaliyoharibiwa".
"Usafishaji wa ardhi unaweza kunuiwa kwa nyanja za kijeshi na zisizo za kijeshi", anasema Prof Kil Joo Ban, profesa wa usalama wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Korea.
"Inaruhusu vituo vya uchunguzi kuanzishwa kwa urahisi," anasema "kwa Korea Kaskazini kufuatilia shughuli za kijeshi nchini Korea Kusini" na kuona "waasi wanaojaribu kuvuka mpaka hadi Korea Kusini."

Chanzo cha picha, Getty
"Si kawaida kujenga vizuizi katika DMZ na inaweza kuwa ukiukaji wa uwekaji silaha bila mashauriano ya awali," kulingana na Prof Victor Cha, makamu mkuu wa rais wa Asia na Korea katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.
Vita vya Korea vilimalizika mwaka wa 1953 kwa kusitisha mapigano, ambapo pande zote mbili ziliahidi "kutotekeleza kitendo chochote cha uadui ndani, kutoka, au dhidi ya eneo lisilo la kijeshi." Lakini hakukuwa na suluhu la mwisho la amani.
Ingawa kuungana tena kumeonekana kutowezekana kwa miaka mingi, hili lilikuwa daima lengo lililotajwa la viongozi wa Korea Kaskazini hadi mwanzoni mwa 2024, wakati Kim Jong Un alitangaza kwamba nchi yake haitafuata tena azma hiyo.
Baadhi ya wataalam walitaja matamshi hayo kuwa "hayajawahi kushuhudiwa" na waliona mabadiliko makubwa ya sera wakati Bw Kim alipoitaja Korea Kusini kama "adui mkuu" mwanzoni mwa mwaka huu.
Tangu wakati huo, Korea Kaskazini pia imeanza kuondoa alama zinazowakilisha umoja wa nchi hizo mbili - kama vile kubomoa makaburi na kufuta taarifa za nchi hizo kuunganishwa tena kwenye tovuti za serikali.
"Korea Kaskazini haihitaji vizuizi zaidi kuzuia shambulio kutoka Kusini lakini kwa kuweka vizuizi hivi vya mpaka, Kaskazini inaashiria kwamba haitaki kuunganishwa tena," anasema Dk Ramon Pacheco Pardo, mkuu wa Mafunzo ya Ulaya na Kimataifa. Chuo cha Kings London.
Wataalamu wengine pia wanasema hii inalingana na hatua pana za Bw Kim.
"Korea Kaskazini hata haiigizi hata kutaka kufanya mazungumzo na Marekani au Korea Kusini, na imepinga majaribio ya hivi majuzi ya Japan ya kushiriki mazungumzo," anasema Dk Edward Howell, mtafiti wa Peninsula ya Korea huko Oxford.
"Kwa uhusiano mzuri wa Korea Kaskazini na Urusi, hatupaswi kushangaa ikiwa uhasama kati ya Korea hizo mbili utaongezeka mwaka huu."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












