China ndio yenye nguvu katika urafiki unaokuwa wa Putin na Kim

K

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Kim Jong Un na Vladimir Putin
    • Author, Laura Bicker
    • Nafasi, BBC

Kukumbatiana na kukaribishwa na heshima ya askari waliopanda farasi, ndio picha kubwa ya Kim Jong Un na Vladimir Putin - haya yalifanywa ili kuzitia wasiwasi nchi za Magharibi.

Ziara ya kwanza ya Putin mjini Pyongyang tangu 2000 ilikuwa fursa kwa Urusi na Korea Kaskazini kuonesha urafiki wao. Na walifanya hivyo, huku Kim akitangaza "uungaji mkono" kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ukweli ni kwamba viongozi hao wawili wanaamini wanahitajiana - Putin anahitaji sana silaha ili kuendeleza vita na Korea Kaskazini inahitaji pesa.

Hata hivyo, nguvu halisi katika eneo hilo haiko Pyongyang. Iko Beijing, China, mshirika muhimu wa biashara na ushawishi kwa serikali hizi mbili zilizoekewa vikwazo.

Na hata kama Putin anasifu "urafiki wake’’ na Kim, lazima ajue kuwa una kikomo. Na kikomo hicho ni Rais wa China Xi Jinping.

Beijing inatazama

cx

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Rais wa China Xi Jinping

Kuna baadhi ya ishara kwamba Rais wa China, Xi hakubaliani na urafiki unaoshamiri kati ya washirika wake wawili.

Ripoti zinaonyesha Beijing ilimtaka Rais Putin kutotembelea Pyongyang mara baada ya kukutana na Rais Xi mwezi Mei. Inaonekana maafisa wa China hawakupenda ziara ya Putin Korea Kaskazini.

Xi tayari yuko chini ya shinikizo kubwa kutoka Marekani na Ulaya kukata uungaji mkono wake kwa Moscow na kuacha kuiuzia vifaa vinavyosaidia vita vyake nchini Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Na hawezi kupuuza maonyo haya. Kama vile ulimwengu unavyohitaji soko la China, Beijing pia inahitaji watalii wa kigeni na uwekezaji ili kukuza uchumi na kushikilia nafasi yake kama uchumi wa pili kwa ukubwa duniani.

Sasa China inaruhusu safari bila viza kwa wageni kutoka sehemu za Ulaya na pia kutoka Thailand na Australia. Na dubu wake mara nyingi hupelekwa kwenye mbuga za wanyama za nchi za kigeni.

Mitazamo ni muhimu kwa China, ambayo inataka kuchukua jukumu kubwa la kimataifa na kutoa changamoto kwa Marekani. Hakika China haitaki kutengwa au kukabiliana na shinikizo jipya kutoka Magharibi. Wakati huo huo, bado inasimamia uhusiano wake na Moscow.

Ingawa Xi hajalaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, hadi sasa ameshindwa kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Urusi. Na wakati wa mkutano wa Mei, hotuba yake ya tahadhari ilikuwa tofauti na pongezi za Putin kuhusu Xi.

Kufikia sasa, China pia imetoa ulinzi wa kisiasa kwa juhudi za Kim kuendeleza silaha zake za nyuklia, kwa kuzuia vikwazo vinavyoongozwa na Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Xi si shabiki wa Kim Jong Un

Majaribio ya silaha ya Pyongyang yameziwezesha Japan na Korea Kusini kuweka kando historia yao chungu na kutia saini makubaliano ya ulinzi na Marekani.

Wakati mvutano unapoongezeka, meli nyingi za kivita za Marekani hujitokeza katika maji ya Pasifiki, na kusababisha hofu ya Xi ya "Nato ya Mashariki ya Asia."

Andrei Lankov, mkurugenzi wa NK News, anasema ana shaka: "Sitarajii Urusi kuipatia Korea Kaskazini kiwango kikubwa cha teknolojia ya kijeshi."

Anaamini, Urusi haipati mengi kutoka Korea Kaskazini na pengine italeta matatizo yanayoweza kutokea siku zijazo" ikiwa itafanya hivyo.

Na Putin anaweza kutambua haifai kuikasirisha China, ambayo inanunua mafuta na gesi ya Urusi, na inasalia kuwa mshirika muhimu katika ulimwengu ambao umemtenga.

Pyongyang inahitaji China zaidi. Ni nchi pekee ambayo Kim anatembelea. Robo hadi nusu ya mafuta ya Korea Kaskazini yanatoka Urusi, lakini 80% ya biashara yake iko na China. Mchambuzi mmoja alielezea uhusiano wa China na Korea Kaskazini kama taa inayoendelea kuwaka.

Hata ikiwa Putin na Kim wanajaribu kuonekana kama washirika, uhusiano wao na China ni muhimu zaidi kuliko kile wanachoshirikiana.

China ni muhimu zaidi

o

Chanzo cha picha, [Gavriil Grigorov/Sputnik kupitia AFP]

Maelezo ya picha, Korea Kaskazini ilimkaribisha Putin kwa shangwe, na umati wa watu ulikusanyika katika uwanja wa Kim Il Sung kumshangilia rais wa Urusi

Mapambano ya wazi ya Putin na Kim dhidi ya "mabeberu wa Magharibi," yanaweza kukuwa, hata kuboresha ushirikiano wao kwa kiwango cha "muungano."

Mkataba wa Ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, uliotangazwa kwenye mkutano kati ya Putin na Kim, sio hakikisho kwamba Pyongyang inaweza kuendelea kusambaza silaha.

Wachambuzi wanaamini Urusi na Korea Kaskazini hutumia mifumo tofauti ya kijeshi, huku mifumo ya Kaskazini ikiwa ya ubora wa chini na inazeeka.

Urusi na Korea Kaskazini hazikuweka kipaumbele uhusiano wao kwa miongo kadhaa. Alipokuwa na urafiki na nchi za Magharibi, Putin aliiwekea vikwazo Pyongyang mara mbili na kujiunga na Marekani, China, Korea Kusini na Japan ili kuishawishi Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Wakati Kim Jong Un alipojitosa kwenye mikutano ya kilele ya kidiplomasia 2018, alikutana na Vladimir Putin mara moja tu.

Kim alitumiana "barua" na Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump kabla ya mikutano yao mitatu - mtu ambaye aliwahi kumwita "kikongwe" ghafla akawa "mtu muhimu."

Pia alifanya mikutano mitatu na Xi, kiongozi wa kwanza wa kimataifa kuwahi kukutana naye.

Gazeti la serikali ya Korea Kaskazini liliangazia masilahi ya pamoja ya Urusi na Kaskazini na kupingana na Magharibi.

Kim alimsifia Xi, ambaye alitangaza kuwa ni ndugu wa karibu, huku akisifu uchumi wa China. Na kusema familia yake inajifunza Mandarin.

Kwa hakika Putin hangethubutu kumweka Rais Xi akingoja kwa saa nyingi na kuchelewa kufika kama alivyofanya kwa Kim.

Mbele ya China, wote wako chini. Na bila China, tawala zao zitapata tabu.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla