Kim Jong Un: Je, kiongozi wa Korea Kaskazini anajiandaa kuingia vitani?

Chanzo cha picha, KCNA
Wiki iliyopita, wafuatiliaji wawili wa Korea ya Kaskazini walisema wana imani kiongozi wa taifa hilo lililotengwa Kim Jong Un anajiandaa kwa vita.
'Kim Jong Un ametupilia mbali lengo la kupatanisha na kuunganisha tena Korea Kusini na Kaskazini,' wanasema na kuongea, 'badala yake, anaitazama Kaskazini na Kusini kama nchi mbili huru zinazopigana.'
"Tunaamini kama babu yake 1950, Kim Jong Un amefanya uamuzi wa kimkakati wa kuingia vitani," ameandika Robert L Carlin, mchambuzi wa zamani wa CIA na Siegfried S Hecker, mwanasayansi wa nyuklia ambaye ametembelea Kaskazini mara kadhaa katika makala kwenye tovuti ya 38 North.
Kauli hiyo iliamsha kengele huko Washington na Seoul, na mjadala mkubwa huko Korea Kaskazini. Wachambuzi wengi, hata hivyo, hawakubaliani na maoni ha ya vita.
Wataalamu wengine

Chanzo cha picha, KCNA
BBC ilizungumza na wataalamu saba kutoka Asia, Ulaya na Amerika Kaskazini - hakuna hata mmoja ambaye aliunga mkono wazo hilo.
"Kuhatarisha utawala wake wote kwa mzozo unaoweza kusababisha maafa sio tabia ya Wakorea Kaskazini," anasema Christopher Green, mfuatiliaji wa Korea kutoka Crisis Group lenye makao yake Uholanzi.
Yeye na wengine wanaona mara nyingi Kim hufanya mambo ili kuileta Magharibi kwenye meza ya mazungumzo.
Hata hivyo, wanakubaliana na hoja kwamba – sio jambo la kupuuza utawala wake umezidi kuwa hatari. Ingawa wanabisha, vita si jambo linaloweza kutokea. Lakini anaweza kuendeleza majaribio yake.
Ni nini kimesababisha hofu ya vita?

Chanzo cha picha, Getty images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wataalamu wanaomfuatilia Kim Jong Un wa Korea Kaskazini wamezoea vitisho vyake vya nyuklia, lakini wengine wanasema jumbe za hivi punde kutoka Pyongyang ni za tofauti.
Siku sita baada ya tamko lake la Mkesha wa Mwaka Mpya kwamba "ni kweli vita vinaweza kuzuka wakati wowote kwenye peninsula ya Korea," jeshi lake lilifyatua mizinga ya kuvuka mpaka.
Korea Kaskazini pia imedai kufanya jaribio la kombora jipya lenye nguvu zaidi, na ndege zake zisizo na rubani za chini ya maji, ambazo zinaweza kubeba silaha za nyuklia, mwanzoni mwa Januari.
Pia, tangazo lake la kuachana rasmi na mpango wa kuungana na Korea Kusini. Kuungana tena na Kusini ni jambo la msingi kama sehemu ya itikadi ya Kaskazini tangu kuanzishwa kwa taifa hilo.
Pamoja na kufunga njia za diplomasia na matangazo ya redio ya kuvuka mpaka, ametangaza atabomoa ‘mnara wa muungano.’ Jengo la ghorofa tisa nje kidogo ya Pyongyang.
Mnara huo unaonyesha wanawake wawili waliovalia mavazi ya kitamaduni ya Kikorea, uilijengwa mwaka 2001 kuashiria juhudi za baba yake na babu kuelekea lengo la kuungana tena.
Picha za satelaiti zilizotolewa na Planet Labs, Jumanne zinaonyesha mnara huo tayari umeharibiwa, ingawa hakuna uthibitisho rasmi wa hilo.
Kim Il Sung ndiye aliyeingia vitani mwaka wa 1950, lakini pia ndiye aliyeweka wazo kwamba wakati fulani Wakorea Kaskazini waungane na jamaa zao wa kusini tena.
Uchokozi wa Kim

Carlin na Dk Hecker, wachambuzi waliotabiri vita, wamefasiri yote haya kama ishara Kim Jong Un anajiandaa kufanya vita.
Seong-Hyon Lee, kutoka wakfu wa George HW Bush wa uhusiano wa Marekani na China, hakubaliana na tafsiri hiyo.
Anadokeza kuwa nchi hiyo inatazamiwa kufungua shughuli za kitalii mwezi ujao, na pia imeuza makombora yake kwa Urusi – mambo hayo yanaenda kinyume na mpango wa vita.
"Vita vinaweza kuua watu wengi Kusini, lakini utakuwa mwisho wa Kim Jong Un na utawala wake," anasema Peter Ward, mtafiti kutoka chuo kikuu cha Kookmin University, Seoul.
Mwaka 2010, Kaskazini ilipiga kisiwa cha Yeonpyeong na kuua wanajeshi wanne wa Korea Kusini. Uchokozi kama huo unaweza kufanywa tena ili kuijaribu Korea Kusini.
Utawala huo unaendelea kuteseka kutokana na vikwazo vya kiuchumi na 2024 ni mwaka wa uchaguzi kwa maadui zake - kura ya urais wa Marekani na kura ya wabunge wa Korea Kusini.
"Mengi ya yale tunayoyaona ni matokeo ya imani ya Korea Kaskazini katika uwezo wake na msimamo wake kwa kuungwa mkono na Urusi, na kwa kiwango kidogo, msaada wa China," anasema mchambuzi Ankit Panda, kutoka taasisi ya Carnegie Endowment for International Peace.
Malengo ya ndani

Chanzo cha picha, Reuters
Na wengine wanasema tabia ya Kim Jong Un inalenga kuleta utulivu kwa utawala wake.
Anasema Profesa Leif-Eric Easley kutoka Chuo Kikuu cha Ewha huko Seoulm, "Wakorea Kaskazini wanazidi kufahamu mapungufu ya nchi yao ya Kikomunisti ikilinganishwa na Kusini. Kwani kuna ripoti za njaa Korea Kaskazini.”
"Kwa kweli hataki vita – hiyo ni kamari kubwa ambapo hawezi kupata chochote na atapoteza kila kitu," anasema Sokeel Park, kutoka Liberty nchini Korea Kaskazini, NGO inayosaidia wakimbizi wa Korea Kaskazini.
“Vitisho vyake badala yake vinalenga kuimarisha sera yake mpya ya Kaskazini na Kusini, ili hatimaye kuimarisha mamlaka yake nyumbani,” anasema.
Ingawa ni muhimu kwa Korea Kusini, Marekani na washirika kujiandaa kwa lolote baya. Kadhalika, wanapaswa pia kufanya uchunguzi wa kina wa hali ya ndani ya Korea Kaskazini, wachambuzi wanasema.
“Mwisho wa siku, njia bora ya kujua kile ambacho kiongozi wa Kaskazini anakifikiria ni kujihusisha naye,” anasema Dkt. Lee.
"Jumuiya ya kimataifa haitoiona Marekani kuongea na Kim Jong Un kama kusalimu amri kwa vitisho vya Kim Jong Un. Bali itaonekana kama njia ya kufikia lengo," anasema.
"Mtu anapaswa kukutana na kiongozi wa taifa adui ikibidi ili kupunguza mawazo potofu na kuzuia vita."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












