Mvutano wa Korea Kaskazini: Kwa nini Kim Jong-un anaongeza hali ya wasiwasi?

Chanzo cha picha, KCNA
Kumekua na vipindi vya wasiwasi Korea Kaskazini vinavyokuja na kuondoka, lakini hali katika peninsula ya Korea hivi sasa ndiyo tete zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka mitano na inaonekana huenda ikawa mbaya zaidi.
Katika kipindi cha mwezi uliopita Kaskazini imerusha kombora katika anga ya Japan, na kuwalazimisha wakaazi kutafuta makazi; kitendo kinachotajwa ni cha uadui na uchochezi.
Imerusha makombora mengine kadhaa ya balestiki, imerusha ndege za kivita karibu na mpaka wake na Korea Kusini na kurusha mamia ya makombora ya mizinga baharini, ambayo yametua katika eneo la kinga la kijeshi, iliyoundwa na Korea mbili mnamo 2018 kulinda amani.
Nchi hizo mbili kiufundi bado ziko vitani. Siku ya Jumatatu meli ya kibiashara ya Korea Kaskazini ilivuka mpaka wa bahari ya nchi hizo, na kusababisha pande zote mbili kufyatua risasi za tahadhari. Korea Kusini inasema uvamizi huo ulikuwa wa makusudi.
Kwa hivyo, Kim Jong-un anafanya hivi kwanini? Kuna sababu tatu ambazo Korea Kaskazini inaelekea kurusha makombora -mosi, kufanya majaribio na kuboresha teknolojia ya silaha, kutuma ujumbe wa kisiasa kwa ulimwengu (hasa Marekani), na kuwavutia watu wake nyumbani na kuimarisha uaminifu kwa serikali.
Inaweza kuwa vigumu kubainisha ni sababu ipi hasa kati ya hizi itamaliza vitendo vya Pyongyang, lakini wakati huu Bw Kim amekuwa wazi.
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti mara kadhaa kwamba uzinduzi na mazoezi ya hivi karibuni ni kujibu mazoezi ya kijeshi yanayoendeshwa na Marekani, Korea Kusini na Japan.
Korea Kaskazini imewalaumu maadui zake kwa kuzidisha mvutano na kusema kuzinduliwa kwa makombora ni onyo la wazi wanapaswa kuacha.

Chanzo cha picha, KCNA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Washington, Seoul na Tokyo zimekuwa zikifanya mazoezi makubwa ya kijeshi, tofauti na kwa pamoja, kwa muda wa miezi miwili iliyopita, ili kuonyesha wako tayari kwa shambulio la nyuklia la Korea Kaskazini.
Hakuna shaka kwamba haya yamemkasirisha Bw Kim, ambaye kila mara amekuwa akiona mazoezi kama hayo kama maadui wake wanaofanya mazoezi ya uvamizi. Sababu ya Korea Kaskazini kuanza kutengeneza silaha za nyuklia hapo awali ilikuwa ni kujilinda na uvamizi.
Lakini kuna sababu isiyo wazi sana anaweza kuwa anaongeza shinikizo kwa sasa. Anaweza kuwa anatayarisha mazingira ya jaribio la uchochezi zaidi - kulipuliwa kwa silaha ya nyuklia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano, au hata shambulio la kiwango kidogo dhidi ya Korea Kusini.
Mwaka jana aliweka mpango wa miaka mitano, akielezea silaha zote mpya alizopanga kutengeneza. Ilijumuisha mabomu madogo ya nyuklia kwenye uwanja wa vita na makombora ya masafa mafupi ya kubebeka.
Majaribio ya hivi majuzi ni ushahidi kwamba Bw Kim hafanyii kazi orodha hii ya matamanio ya silaha pekee, lakini pia anawafunza wanajeshi wake kuzitumia.
Sasa Bw Kim anahitaji kuzingatiwa. Anahitaji ulimwengu kutambua maendeleo ambayo amefanya.
Vikwazo havijaizuia Korea Kaskazini kutengeneza silaha, kama ilivyopanga, lakini vinaathiri uchumi wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ulimwengu umejielekeza zaidi katika vita vya Ukraine, na kuongezeka kwa mamlaka ya China. Msimamo wa Rais Biden ni kwamba vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini vinaweza tu kupunguzwa pale itakapokubali kuachana na silaha zake zote za nyuklia.
Wakati huo huo, Washington na Seoul zimekubaliana kuimarisha ulinzi wao katika eneo la Peninsula kwa kufanya mazoezi ya kijeshi ambayo Pyongyang inachukia sana, na kujibu chokochoko zake kwa nguvu.
Kufuatia duru ya hivi punde zaidi ya kurusha makombora na mazoezi ya Kaskazini, Korea Kusini ilituma ndege za kivita na kurusha mizinga yake.
Iwapo Bw Kim anataka Marekani ifanye mazungumzo juu ya masharti yanayompendeza zaidi, lazima athibitishe jinsi nchi yake imekuwa hatari.
Mwezi uliopita alitangaza Korea Kaskazini kuwa taifa la silaha za nyuklia, msimamo ambao alisema hauwezi kutenguliwa.
Je, uwezo wa nyuklia wa Korea Kaskazini ni upi?

Chanzo cha picha, KCNC
Tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu jinsi inavyoonekana kuwa na uthubutu, alisema Kim Jong-dae, mshauri wa zamani katika Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini. Alidokeza jinsi siku za nyuma Korea Kaskazini ilisubiri hadi vikosi vya Marekani vimalize mazoezi yao ya kijeshi kabla ya kulipiza kisasi. Safari hii walirusha mizinga baharini huku mazoezi yakiendelea.
"Hatujawahi kuona ujasiri na uchokozi huu hapo awali, ni tofauti. Ni Kaskazini inayofanya kama taifa la nyuklia," alisema.
Serikali za Marekani na Korea Kusini zinaamini kuwa maandalizi ya jaribio la saba la silaha za nyuklia kwa Korea Kaskazini yamekamilika na Kaskazini inasubiri wakati mwafaka wa kisiasa kuchukua hatua.
Mkutano wa Chama cha Kikomunisti cha China sasa umekwisha na uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani unakaribia. Wakati huohuo Korea Kusini iko katikati ya duru nyingine ya michezo ya vita, huku Marekani ikipangwa kujiunga nayo. Haya yanaweza kumpa Kim Jong-un kisingizio ambacho amekuwa akikisubiri.














