Kutoka kupeana mikono hadi uadui: Hali ni mbaya kiasi gani Korea Kaskazini

Kim Jong-un anazifanyia majaribio silaha za kisasa za Korea Kaskazini, huku Korea Kusini ikijiandaa kumwapisha rais mpya, mwenye msimamo mkali. Baada ya miaka mingi ya mkwamo, kufuatia kushindwa kwa mazungumzo ya nyuklia, mvutano kwenye eneo la peninsula ya Korea unaongezeka.
"Nilifikiria kupata shoka, lakini niliamua itakuwa ngumu sana kubeba, kwa hivyo niliamua kuchukua kisu."
Akiwa ameketi kwenye baa yenye mwanga hafifu, usiku mmoja hivi, Jenn anasimulia mpango wake wa kina wa kutoroka. Kama raia wa Korea Kusini, anayeishi katika jiji la Seoul, anajua ni nini hasa anapaswa kufanya ikiwa Korea Kaskazini ingeshambulia.
Kwanza ni kuwa na silaha, kisha pikipiki mbili: moja yake, nyingine ya kaka yake. Wazazi wao wangewafuatwa kwa nyuma. Kwa njia hii wangeweza kuvuka mto wa jiji hilo haraka, kabla ya Wakorea Kaskazini kushambulia madaraja kwa mabomu, na kwa matumaini kufika pwani kabla ya bandari kuharibiwa.
Jioni moja yeye na kaka yake waliketi na kuchora ramani ya njia yao, wakikubaliana kufunga riboni kwenye miti ikiwa wangetenganishwa.
Hii ilikuwa miaka mitano iliyopita. Wakati huo, Korea Kaskazini ilikuwa ikijaribu kwa hasira makombora yake ambayo kwa nadharia yalionekana ni majaribio ya silaha za nyuklia kwa Marekani, na Rais wake wa wakati huo Donald Trump alitishia kujibu "mapigo".

Chanzo cha picha, Getty Images
Jenn anakubali kwamba alikuwa na wasiwasi zaidi kuliko watu wengi. Lakini hata hivyo, hii ilikuwa hali ya watu wengi wa karibu zaidi wa Korea Kusini waliona kuwa wameingia tena vitani tangu mapigano na Korea Kaskazini yalipomalizika karibu miaka 70 iliyopita.
Kisha jambo la ajabu likatokea. Rais mpya mteule wa Korea Kusini wakati huo, Moon Jae-in, alimshawishi Bw Trump kukutana na Kim Jong-un. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais aliyeko madarakani wa Marekani kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini. Msururu wa mikutano ya kilele ya kihistoria ilifuata, na kuzua matumaini kwamba Kaskazini inaweza kukubali tu kuachana na silaha zake za nyuklia, na amani itatawala katika Korea zote mbili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini Rais Moon anapoondoka madarakani, matumaini ya mwaka huo yanazidi kudorora. Wakati makubaliano ya nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini yalipovunjika mwaka 2019, mazungumzo kati ya Korea pia yalidorora.
Kumekuwa na mkwamo tangu wakati huo. Wakati huo huo Korea Kaskazini imeendelea kutengeneza silaha zake za maangamizi makubwa na kwa mara nyingine inazifanyia majaribio kwa masafa ya kutisha. Wakati huu tu, kwasababu ya vita vya Ukraine inamaanisha macho ya ulimwengu yameelekezwa mahali pengine.
Alipoulizwa ikiwa serikali imeshindwa, Prof Moon Chung-in anajitetea. "Hapana, sidhani! Kulikuwa na vita?" Anasababu kwamba kwa miaka mitano serikali ya Moon ililinda amani katika wakati ambao ulikuwa mbaya katika uhusiano kati ya Korea.
Rais Moon alijaribu kila awezalo kuwashawishi Wakorea Kaskazini warudi kwenye mazungumzo, lakini kwa kufanya hivyo ameshutumiwa kwa kumridhisha mmoja wa madikteta katili zaidi duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Nilipoona picha zao wakiwa wamekumbatiana wakicheka, nilitetemeka," anakumbuka Hanna Song, mwenye ofisi yake katikati mwa jiji la Seoul.
Shirika lake, Kituo cha Hifadhidata cha Haki za Kibinadamu cha Korea Kaskazini, kimekuwa kikifuatilia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Korea Kaskazini kwa zaidi ya miongo miwili. Miaka michache iliyopita haikuwa rahisi.
Haki za binadamu zinasiginwa chini ya Kim Jong-un, Hanna anaelezea. Anasema kuwa katika juhudi za kumzuia kiongozi wa Korea Kaskazini asijisikie vibaya, Rais Moon "alimfagilia njia".

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini kukumbatiana na kupeana mikono kumekwisha. Korea Kusini imemchagua Rais mpya, mmwenye msimamo mkali, mwendesha mashtaka wa zamani asiye na uzoefu wa kisiasa. Katika mahojiano ya hivi majuzi, Yoon Suk-yeol alielezea Korea Kaskazini kama "adui mkubwa" wa Korea Kusini na ameahidi kuchukua mtazamo mgumu kwa kuongeza nguvu za kijeshi.
Amesema atazungumza tu na jirani yake, ikiwa Korea Kaskazini itaonyesha nia ya dhati kuondoa au kuachana na silaha za nyuklia. Lakini wataalamu wengi sasa wanakubali kwamba Korea Kaskazini haina nia yoyote ya kuachana na silaha zake za nyuklia. Ilikuwa imefikia hitimisho hili muda mrefu kabla ya vita vya Ukrainia kuangazia hatari za kuacha silaha kama hizo, ingawa hii haijasaidia.
Hii inaonyesha mkakati wa Bw Yoon "kutokuwa na fursa ya kutekelezeka" kwa mujibu wa Chris Green, mshauri wa International Crisis Group, shirika linalojishughulisha na kuzuia vita.
Wakati wa kampeni zake, Bw Yoon alifikia hatuya ya kusema angeanzisha mashambulizi ya mapema dhidi ya Korea Kaskazini, ili kuharibu silaha zake, ikiwa kungekuwa na dalili kwamba Kaskazini iko karibu kufanya mashambulizi. Mwezi uliopita Korea Kaskazini ilifanya maonyesho ya makombora yake barabarani, katika jaribio lake la hivi punde la kuonyesha nguvu zake. Kim Jong-un, akiwa amevalia sare nyeupe za kijeshi, alitoa onyo kali: jeshi lolote la uhasama ambalo liliitishia Korea Kaskazini, "litasambaratishwa". Hii ilitafsiriwa, angalau kwa kiasi fulani, kama onyo kwa rais mpya wa Korea Kusini.

Chanzo cha picha, MOON CHUNG-IN
Lakini Chris Green bado anaamini kuwa lengo kuu la Korea Kaskazini ni kujinusuru. "Kama ingetumia silaha ya nyuklia, kwa hali yoyote ile, ingeashiria mwisho wa utawala, na Korea Kaskazini inajua hilo," anaeleza. Bw Green anatabiri majaribio ya silaha kw apande zote mbili yataleta mzozo zaidi.
Kuna wasiwasi huko Seoul kuhusu kile kinachokuja, kama Korea Kaskazini inajaribu nguvu na mipaka ya serikali mpya na kujaribu kuunga mkono ajenda ya kimataifa. "Ninajizatiti," Luteni Jenerali wa zamani wa Korea Kusini alikiri.
Ulimwengu unaweza kuwa unatazama mahali kwingine, lakini kwa Korea Kaskazini ni ngumu kuipuuza.














