Je, mustakabali wa kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utakuwaje?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 8

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, ambaye amejificha kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi saba, anajua kuwa sasa anaweza kuwa shabaha binafsi.

Haiwezekani atakuwa akitembea kwenye uwanja wake wa nyuma ya nyumba au ameketi kwenye roshani yake kwa amani wakati wowote hivi karibuni.

Wakati wa kujadili kile ambacho Marekani inaweza kufanya baadaye kuwasaidia waandamanaji nchini Iran, Rais wa Marekani Donald Trump amemtaja Qassem Soleimani na Abu Bakr al-Baghdadi.

Wa kwanza, mtaalamu wa mikakati ya kijeshi wa Iran katika Mashariki ya Kati, aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad kwa amri ya rais wa Marekani Januari 3, 2020.

Wa pili, kiongozi wa kundi la ISIS, alijilipua na vazi la kujitoa mhanga mnamo Oktoba 27, 2019, wakati majeshi ya Marekani yalipovamia maficho yake kupitia rukhusa ya rais wa Syria katika eneo la kaskazini mwa Syria.

Lakini Ayatollah Khamenei pia hajasahau hatima ya kiongozi wa Hizbullah Hassan Nasrallah.

Aliuawa katika shambulio la anga la Israel mnamo Septemba 27, 2024, alipokuwa akishauriana na wasaidizi wake wa karibu karibu mita 20 ndani ya nyumba ya makazi ya juu mjini Beirut.

.

Chanzo cha picha, Anadolu Agency/Getty Images

Maelezo ya picha, Qassem Soleimani (katikati) aliuawa katika shambulio la Marekani.

Kukamatwa kwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro huko Caracas mnamo Januari mwaka huu kuna uwezekano kuwa hakuko mbali na mawazo ya Ayatollah.

Rais wa Marekani sasa anapima chaguzi zake. Hapo jana, baada ya kuona jumbe za x za kiongozi huyo wa Iran, alisema kwamba anapaswa kufikiria kuhusu uongozi mpya wa Iran.

Ayatullah Khamenei aliandika katika ujumbe katika mtandao wa X kwamba Marekani na utawala wa Donald Trump ndizo zilizohusika na mauaji ya maelfu ya watu nchini Iran katika wiki za hivi karibuni.

Mtu anayechukiwa na Wairan

Kwa miaka mingi, Ayatollah Khamenei, ambaye ana umri wa miaka 86, amekuwa mtu anayechukiwa na Wairani wengi.

Waandamanaji kote nchini wamekuwa wakitaka kupinduliwa kwake kwa miaka mingi. Amekuwa kiongozi mbaya kwa nchi. Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa tawala kandamizi zaidi duniani.

Wakati wa miaka 36 ya Bw. Khamenei madarakani, amekuwa akifuata bila kuchoka sera za chuki dhidi ya Marekani na Magharibi huku akitegemea Urusi na China kuishi.

Amefuata sera ya nyuklia ya upendeleo ambayo haijasababisha chochote ila gharama, vikwazo, na taabu kwa nchi.

Juhudi zake za kupanua ushawishi wake na uwezo wake wa mradi huo katika Mashariki ya Kati zimesababisha eneo hilo kuwaka moto. Miito yake ya kutaka Israeli iangamizwe imesababisha vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Ali Khamenei, ambaye ana umri wa miaka 86, hajaonyesha dalili zozote za kutaka kuachia ngazi kwa hiari.

Bw. Khamenei aliamuru msako mkali dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya hivi majuzi. Amekiri kuwa maelfu ya watu wameuawa katika msako huo.

Kwa kuzimwa kwa mtandao nchini Iran, ni vigumu kupata picha kamili ya ukubwa wa mauaji ya waandamanaji. Jambo lililo wazi ni kwamba, mauaji hayo yametokea sio tu katika miji mikubwa na midogo bali hata vijijini, jambo ambalo ni ishara ya kuenea kwa maandamano dhidi ya utawala wa Ayatullah Khamenei.

Kuondolewa kwake, ikiwa uamuzi huo utafanywa, kunaweza kusababisha machafuko na uvunjaji wa sheria, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba Walinzi wa Mapinduzi watajaribu kujaza pengo lake.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa kuzimwa kwa mtandao nchini Iran, ni vigumu kupata picha kamili ya ukubwa wa mauaji ya waandamanaji.

Kwa mujibu wa Arash Azizi, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Yale na mwandishi wa kitabu "What Iranians Want," baadhi ya watu ndani ya serikali wanaweza hata kukaribisha kuondolewa kwa Ayatollah Khamenei.

Anasema: "Sehemu kubwa ya maafisa wa nchi nchini Iran wako tayari kufanya mabadiliko fulani. Tukimweka kando Khamenei, tukiweka kando baadhi ya sera za msingi na taasisi kuu za Jamhuri ya Kiislamu. Hivyo wanaweza hata kukaribisha mashambulizi ya Marekani kama fursa ya kuharakisha mchakato huu."

'Watawala na watawaliwa'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mohammad Bagher Qalibaf, 64, spika wa sasa wa bunge la Iran, ni mwanachama wa Walinzi wa Mapinduzi mwenye mielekeo ya kimabavu. Ameachana na mavazi yake ya kijeshi na sasa amevaa kiraia.

Ingawa yeye ni muungaji mkono mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Khamenei hajawahi kumuamini kikamilifu. Wengi serikalini wanamwona kama mbwa mwitu zaidi aliyevaa ngozi ya kondoo, akingojea wakati mwafaka wa kushambulia.

Jina la Rais wa zamani Hassan Rouhani linakuja akilini. Amejiweka kama mgombea makini wa makundi ya kidini yenye msimamo wa wastani na wapenda mabadiliko iwapo kiongozi huyo atafariki.

Ali Ansari, mwanzilishi wa Shule ya Mafunzo ya Iran katika Chuo Kikuu cha St. Andrews huko Scotland, anaamini kwamba wanamageuzi kwa kiasi kikubwa wamepoteza umuhimu wao.

"Kimsingi, wapenda mageuzi hawapo kabisa... ni aina fulani ya nguvu ya kuonyesha na kuonekana na wametengwa kabisa. Kiuhalisia, sasa tuna watawala na watawaliwa tu," anasema.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Reza Pahlavi ana umri wa miaka 65 na ameishi zaidi ya maisha yake uhamishoni nchini Marekani

Lakini jina ambalo watu wengi wanalizungumzia katika mitaa ya miji na miji ya Iran ni la mtoto wa Shah wa zamani wa Iran, Mwanamfalme Reza Pahlavi, ambaye ana umri wa miaka 65 na ametumia muda mwingi wa maisha yake uhamishoni mjini Washington.

Katika miaka ya hivi karibuni, umaarufu wa Reza Pahlavi umeongezeka ndani ya Iran, ambapo wengi hutazama nyuma kwa furaha enzi za Shah, hasa miaka ya 1970, wakati Wairani walikuwa miongoni mwa mataifa yaliyostawi zaidi kutokana na mapato makubwa ya mauzo ya mafuta, mradi wangeweka siasa zao wenyewe.

Lakini Reza Pahlavi ameshindwa kuwaunganisha Wairani kwa njia yoyote ile. Kwa hakika, wengi wanaamini kwamba amekuwa mgawanyiko, na kushindwa kuunganisha upinzani wa Iran nje ya nchi chini ya bendera moja, na ameamua kwenda peke yake, akidai kuwa taifa liko nyuma yake.

Na hata kama angekuwa kiongozi pekee, Wairani wanatamani ndani ya nchi, ni ngumu kumfikiria katika nafasi ya kuchukua madaraka. Hana msingi wa shirika nchini Iran ambao unaweza kumsaidia kupata madaraka.

Wengi wanahoji kwamba umaarufu wake usiotarajiwa ndani ya Iran wakati wa maandamano ya hivi majuzi unatokana na ukweli kwamba waandamanaji wengi walimwona kama mdai tu wa mamlaka akisimama dhidi ya serikali inayochukiwa.

Wengi wa waandamanaji hao wanapendelea mtu ambaye hana historia ya ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu na anataka uhusiano bora na nchi za Magharibi.

"Kwa sasa, mabadiliko madogo hayana uwezekano wa kukidhi matakwa ya waandamanaji, kwa sababu maandamano haya yanahusu suala kubwa zaidi," anasema Sanam Vakil, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika jumba la wasomi la Chatham House huko London.

Bi Vakil anaongeza: "Maandamano haya yanahusu kubadilisha kabisa jinsi Iran inavyotawaliwa, mbali na watu binafsi na mfumo ambao umekuwa madarakani kwa takriban miongo mitano."

Lakini Ayatollah Khamenei, ambaye anaweza kuwa na muda wa kutosha kwenye chumba hicho cha kulala, anaweza kuwa anakagua akilini mwake kile kilichotokea katika wiki tatu zilizopita na jinsi alivyofikia hatua hii.

Anaweza kujisikia kuridhika na ukweli kwamba utawala umebaki mwaminifu kwake hadi sasa. Hakuna dalili ya IRGC kutokuwa mwaminifu kwake. IRGC ni taasisi ambayo iliundwa kimsingi kulinda serikali.

Matamshi ya kutawanyika ya Bw.Trump yamejenga hisia kwamba uwezekano wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya IRGC na vikosi vingine vya usalama vinaweza kudhoofisha na kusambaratisha, na hivyo kufungua njia kwa idadi kubwa ya waandamanaji kuupindua utawala huo.

Amewahimiza waandamanaji kuendelea kuandamana na kukalia majengo ya serikali. "Msaada upo njiani," alisema.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Waandamanaji, ambao kwa kiasi kikubwa wamejiondoa barabarani huku vikosi vya usalama vikiwa tayari kufyatua risasi na kuua, huenda wakatiwa moyo tena na kurejea barabarani kutokana na chokochoko za Bw. Trump

Wengi wao sasa wanaamini kwamba wanahitaji uingiliaji kati wa kigeni ikiwa wanataka kumaliza mfumo huu.

Lakini hata kama hakuna msaada wowote njiani, Wairani wanajua kwamba hivi karibuni au baadaye watarejea mitaani, wakiwa wamejifunza somo kutokana na wimbi la maandamano ya hivi majuzi.

Kutumia nguvu

Katika kipindi cha miaka 16 iliyopita, Wairani wameingia mitaani mara kadhaa kumpinga Ayatollah Khamenei.

Duru ya mwisho ilikuwa mwaka 2022, kufuatia kifo cha Mahsa Amini chini ya ulinzi wa polisi kwa "hijabu isiyofaa."

Wimbi la maandamano lilizuka nchini kote chini ya kauli mbiu ya "Wanawake, Maisha, Uhuru," ambayo iliendelea kwa wiki kadhaa na hatimaye kukandamizwa kwa nguvu na vurugu kali na vikosi vya usalama.

Wakati huo, shinikizo dhidi ya wanawake kutoka kwa watu wenye msimamo mkali wa Kiislamu ndilo lililowaleta watu mitaani. Wengi walidhani inatosha.

.

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano wakati huu yalikuwa yanahusu riziki

Wakati huu maandamano yalikuwa juu ya mkate na uchumi. Kutokana na kushuka kwa thamani ya rial, wachuuzi sokoni hawakuweza tena kuendelea na kazi yao, na wengi hawakuwa na uwezo wa kujikimu.

Umaskini unaenea kwa kasi chini ya shinikizo la vikwazo vya kimataifa na, pengine muhimu zaidi, usimamizi mbovu.

Wakati huo huo, Iran inakabiliwa na uhaba wa maji, umeme, na hasa gesi. Hii ni pamoja na kwamba Iran ina hifadhi ya pili kwa ukubwa wa gesi asilia duniani. Pia, uzembe wa mamlaka umesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unaweza kubaki milele.

Kiongozi mkuu wa Iran amekiri kuwa wafanyabiashara wa sokoni na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiandamana tangu mwishoni mwa mwezi uliopita walikuwa na matakwa ya kweli. Walisema kuendelea kuporomoka kwa sarafu hiyo kumewafanya washindwe kufanya biashara.

Kiongozi huyo wa Iran amesema kuwa mamlaka za nchi hiyo zinajaribu kutatua tatizo hilo, lakini pia amesema tatizo hilo lilitokana na maadui.

Kulingana na Ali Ansari, ukosefu wa uwekezaji katika miundombinu umekuwa mbaya kwa nchi. "Matatizo yanayokabili mfumo huo ni ya kimuundo na yanarudi nyuma miaka mingi," anasema.

Bw. Ansari anaongeza: "Kwa maelezo haya, hata wachumi wa utawala wenyewe wanasema kwamba ikiwa tungetatua matatizo yetu ya sasa, kwa mfano, kushindwa kutoa huduma za msingi kwa wananchi, itakuwa ni kwa sababu hatujawekeza katika miundombinu miaka 20 iliyopita.

Ayatullah Khamenei anajua kwamba hana suluhu kwa mengi ya masuala hayo, hususan uchumi; ni mgogoro ambao unaweza tu kuwa mbaya zaidi.

Lakini licha ya umwagaji damu wa wiki za hivi karibuni, anaweza kujiwazia kuwa sasa si wakati wa kupoteza ujasiri na kwamba lazima asonge mbele kwa mkono wa chuma.

Hata hivyo, anaweza kujiwazia kuwa amepewa utume wa kuitawala nchi ili kueneza Uislamu safi na kwa radhi za Mwenyezi Mungu.