Kitumbua cha Ruto na Gachagua kinavyoingia mchanga na kuzua joto la kisiasa Kenya

th

Chanzo cha picha, RUTO CAMPAIGN

    • Author, Yusuf Jumah
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Miaka miwili tu baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya uliowaingiza madarakani Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua, yaonekana kipindi cha fungate kimefika tamati.

Wiki za hivi karibuni katika siasa za Kenya zimeshuhudia kile kinachoweza kuitwa 'sarakasi' za siasa za Kenya ila inakuwa wazi kwamba kila mambo yanavyobadilika, ndivyo yanavyosalia yalivyokuwa -na hasa katika siasa za taifa hilo la Afrika mashariki.

Naibu wa rais Gachagua sasa anakabiliwa na tishio la kutimuliwa mamlakani kupitia hoja itakayowasilishwa bungeni na washirika wa Rais William Ruto. Katika upande mmoja wa malumbano hayo ni rais na viongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) wanaoumuunga mkono na katika upande wa pili ni naibu wake na viongozi ambao wamesimama naye.

Hatua ya hivi punde inayoashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya wawili hao ni ile ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kutangaza kwamba serikali itawafungulia mashtaka viongozi kadhaa wanaodaiwa kupanga na kufadhili maandamano ya vijana yaliyotikisa serikali miezi ya Juni na Julai. Wanaohusishwa na njama hizo ni washirika wa Naibu wa Rais.

Ufichuzi huo unajiri wiki moja tu baada ya Gachagua kufichua 'mateso' aliyosema ameyapitia katika muda wa mwaka mmoja uliopita alipohojiwa katika kituo cha runinga na Citizen.

Katika mahojiano hayo Gachagua alitoa kauli ambazo zimewaghadhabisha sana washirika wa rais Ruto na kuwafanya kujizidisha harakati zao za kutaka kumuondoa mamlakani. Je, ngoma hii itaishia wapi?

Unaweza Pia Kusoma

Kiini cha malumbano ni nini?

Gachagua na Ruto

Chanzo cha picha, Getty Images

Mvutano kati ya rais wa Kenya na naibu wake sio jambo geni katika siasa za taifa hilo la Afrika Mashariki.

Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta alifungua ukurasa wa malumbano na makamu wa rais wa kwanza wa nchi hiyo Jaramogi Oginga.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hilo limekuwa suala ambalo limejirudia katika tawala zilizofuata na hadi wakati rais wa sasa William Ruto naye alipotofautiana kisiasa na rais wa nne wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kinachomkabili Rigathi Gachagua ni zimwi ambalo lilimuandamana William Ruto katika muhula wa pili alipokuwa naibu wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Gachagua hata hivyo anadai kwamba anachokipitia ni 'kibaya' zaidi hata kuliko masaibu ya Ruto chini ya Uhuru Kenyatta. Amewashtumu washirika na wasaidizi wa rais Ruto kwa kuwa na hila dhidi yake kwa sababu yeye ni ''Msema Kweli''.

Amesema msimamo wake wa kuwaambia Wakenya ukweli ndio unaomfanywa kupigwa vita na watu katika kambi ya rais Ruto. Katika mahojiano yake ya runinga Gachagua alisema kwamba hakuna hoja ya kumuondoa mamlakani inayoweza kuwasilishwa bungeni bila idhini ya rais Ruto na hilo linangojewa kwa hamu ili kuthibitishwa na wengi kwamba kweli rais Ruto amekubali naibu wake kutimuliwa endapo wabunge wataiwasilisha hoja kama hiyo bungeni na kuijadili.

Naibu wa rais amelalamikia visa vya kudharauliwa, kutukanwa na kufichwa kuhusu mipango ya serikali na hata kuzuiwa kumfikia rais. Kupitia mahojiano ya runinga Gachagua alimrai rais Ruto kumruhusu ''afanye kazi kwa miaka mitatu iliyosalia bila kumhangaisha''.

Kauli hiyo yake ilitoa taswira ya kudorora kabisa kwa uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili ambao waliungana kugombea uongozi na kumshinda Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022.

Kambi ya rais Ruto nayo inadai kwamba Gachagua amekuwa akimhujumu rais Ruto na serikali yake. Viongozi wanaomuunga mkono rais sasa wanamhusisha naibu wa rais na maandamano ya vijana wa Gen Z wakisema lilikuwa jaribio la ''mapinduzi''.

Gachagua pia anashtumiwa kwa kuwa ''mkabila''. Wakosoaji wake wanadai kama naibu wa rais hajaichukulia ofisi yake kama ya kitaifa ili kuwaunganisha Wakenya bali kama ''gawio'' na watu wa Mlima Kenya(Kumaanisha jamii ya Kikuyu) anayotoka Gachagua .

Mchambuzi wa masuala ya kisaisa Calvin Muga hata hivyo anasema tofauti kati ya wawili hao ni zaidi ya wanayosema hadharani.

Anasema rais na washirika wake hawajafurahia ujumbe wa kila mara wa Gachagua kwamba ni eneo la Mlima Kenya ndilo lililompigia kura rais Ruto kwa wingi na kumpa ushindi.

Hiyo ni kauli ambayo Gachagua ameikariri kila anapopata fursa na huenda haijawapendeza viongozi wanaomuunga mkono rais Ruto.

Kuingizwa kwa washirika wa Raila Odinga serikalini pia kumetafsiriwa kama hatua nyingine ya kupambana na nguvu ya Gachagua. Uwepo wa viongozi wa upinzani serikali umechangia pia kuzidisha malumbano ya kisiasa yanayoshuhudiwa sasa kati ya Ruto na Gachagua .

Gachagua ameonekana pia kuchukua misimamo ambayo imeonekana kumuacha rais Ruto katika hali ambayo haijawapendeza washirika wake. Alisema wazi kwamba serikali na viongozi wangewasikiliza kwa makini wananchi kuhusu mswada wa fedha wa mwaka wa 2024 uliokataliwa naumma. Mswada huo ulichangia hamaki za raia na kuishia kufutwa na rais Ruto baadaye licha ya kuidhinishwa na Bunge.

Pia Gachagua amelaumiwa na washirika wa rais Kwa kuhutubia taifa kupitia runinga akishtumu Mkuu wa Idara ya Ujasusi Noordin Hajji kwa 'kutomlinda' rais kabla ya maandamano ya vijana kwa kukosa kuipa serikali habari za kuelezea uhalisia wa manung'uniko ya wananchi kuhusu mapendekezo ya kuwakata ushuru yaliyokuwa katika mswada huo .

'Akiba ya maneno'

th

Chanzo cha picha, Reuters

Iwapo kuna kizuri ambacho huibuka katika mabaya yote ya siasa ni mafunzo ambayo walio makini wanaweza kuyapata.

Inakuwa dhahiri kwamba katika kila hali,kwa raha au taabu-ni vyema kujifunza 'kuweka akiba ya maneno'.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amejionea mwenyewe udhaifu wa binadamu kutoweza kutabiri yajayo. Baada ya kumkabili kimabavu rais wa zamani Uhuru Kenyatta wakati akimtetea William Ruto katika kampeni za uchaguzi wa 2022-Gachagua sasa amesema anajutia sana aliyosema na kumfanyia rafiki huyo wake wa zamani.

Gachagua katika mahojiano ya runinga hivi maajuzi, amekiri kwamba Uhuru Kenyatta ndiye kigogo na 'mfalme' wa siasa za eneo la Mlima Kenya (Jamii ya Kikuyu).

Ni abautani nzito sana kwa kiongozi ambaye hakusita kuieleza duniani nzima siku ya kwanza akiingia madarakani akila kiapo kwamba Kenya sasa ilikuwa nchi ''huru'' baada ya yeye na William Ruto kushinda uchaguzi.

Uhuru Kenyatta alikuwa akimuunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga. Miaka miwili baadaye - Odinga sasa ni mshirika wa Ruto na Gachagua amelazimika kupiga breki. Rais Ruto anaongoza kampeni ya kuhakikisha Odinga anachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kinaya kinachomkodolea macho Gachagua ni ahadi yake na Ruto kwamba vyombo vya usalama havitawahi kutumiwa kupambana na wapinzani wa kisiasa. Miaka miwili baadaye washirika wake wanakabiliwa na tishio la kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ambayo sasa Gachagua anadai ni 'ya kisiasa' na ni mbinu ya serikali kutumia idara za usalama kuwakandamiza wapinzani wa kisiasa.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa X ujumbe

'Maigizo' ya kuwafumba macho Wakenya?

TH

Chanzo cha picha, EPA

Wafuatiliaji wa masuala ya Kenya hata hivyo watashangaa kuhusu kipindi hiki cha uhasama kati ya rais Ruto na naibu wake. Ahadi nyingi walizotoa wawili hao wakati wa kampeni huenda zisiwape wengi matumaini kwamba watazitekeleza iwapo hawaaminiani kuzitimiza ahadi za kibinafsi walizotoleana.

Wakati makabiliano hayo ya kisiasa yakiendelea, kuna mapambano ya wananchi, wafanyakazi,wafanyabiashara waajiri na wamiliki wa viwanda ambao wanalalamikia hali ngumu ya kiuchumi.

Usiri mkubwa unaoghubika mipango ya kukodisha uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kwa kampuni ya Adani kutoka India, malalamishi kuibuliwa kwamba kampuni ya Apeiro Ltd, inayomiliki hisa nyingi zaidi katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ilishinda zabuni ya kuweka mfumo wa kiteknolojia wa kufanikisha mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ambayo ni kampuni iliyo uhusiano wa kibiashara na kampuni ya Adani Group ni mambo yanayozua hofu ya kuwepo njama za kupora fedha za umma.

Ufichuzi kwamba mabilioni ya fedha za umma zinaporwa kufadhili siasa za uchaguzi ujao na serikali kuendelea kunyemelea mishahara ya wafanyakazi kupitia makato kama tozo ya nyumba na mradi wa Bima ya Afya SHIF, ni mzozo unaoendelea kutokota'

Lalama za wazazi na wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusu mapungufu katika mfumo mpya wa kufadhili elimu ya juu ni baadhi ya masuala yanayohitaji kuingiliwa kati.

Kuvurugika kwa mazingira bora ya kufanyia biashara na kudorora kwa mapato ya wamiliki wa viwanda, gharama ya juu ya bidhaa za kimsingi,ukosefu wa fedha za kufadhili shughuli za serikali za kaunti na huduma mbovu katika hospitali za umma ni masuala yanayoibuliwa kila uchao.

Migomo ya kila mara ya watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta mbalimbali kuhusu ahadi za nyongeza ya mishahara na mazingira mbaya ya kufanyia kazi ni baadhi ya changamoto ambazo zinahitaji kushughulikiwa na hivyo basi habari za mpasuko katika muungano tawala wa Kenya Kwanza huenda zisiwape Wakenya wengi afueni ya kuwepo muda au raslimaliza za kushughulikia kero hizo.

Ni kipi kitafuata?

TH

Chanzo cha picha, EPA

Kwa sasa mengi kuhusu kitakachotokea ni utabiri tu unaoweza kukisiwa.

Kilicho wazi hata hivyo ni hamu ya wengi kuona jinsi mirengo ya kisiasa itakayoibuka na mkondo wa siasa za Kenya miaka mitatu kabla ya uchaguzi mwingine.

Taifa hilo bado halijaunda tume mpya ya uchaguzi na tayari mengi yanafanyika kwa kasi. Siku zijazo katika bunge la Kenya zimebeba mengi ambayo yatatoa taswira ya mwelekeo na fikra za wahusika wakuu katika toleo hili jipya la vigogo wa kisiasa kutofautiana baada ya kufika mawindoni.

Iwapo jamii zao zitajipata mnadani au kutumika kama chambo kwa awamu nyingine ya uvuvi au kama kinga dhidi ya makali na joto la kisiasa, itakuwa ni muendelezo wa 'sarakasi' za siasa za Kenya.

Iwapo hatua ya rais Ruto kuingia katika ushirikiano wa kisiasa na Raila Odinga ilikuwa karata yake ya 2027- basi mazito yapo njiani kwa sababu matokeo yake huenda yakawaunganisha washirika wake wa zamani na wapinzani wake wa tangu jadi.

Katika siasa hakuna maadui au marafiki wa kudumu lakini kwa mwananchi wa kawaida, huenda cha kudumu kikawa matumaini ''hewa'' yaliyojazwa ahadi tamu za wanasiasa ambazo husahaulika pindi kiapo cha kutwaa usukani kinapotamkwa.

Unaweza Pia Kusoma

Imehaririwa na Ambia Hirsi