Wakenya wanaovuma kwa michango yao katika maandamano ya Gen-Z

Chanzo cha picha, Faith Odhiambo(@FaithOdhiambo8)/X
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili News
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Maandamano ya hivi karibuni nchini Kenya ambayo yamekuwa yakifanywa na vijana yanayofahamika kama maandamano ya Gen-Z na yaliwashangaza sio Wakenya tu bali Afrika na ulimwengu mzima, hususan ni namna ambavyo yalivyokuwa yakipangwa na kuitikiwa kwa wingi na vijana.
Maandamano hayo yalikuwa tofauti na maandamano mengine yaliyofanyika awali ambapo viongozi na waandalizi wake hujulikana, na mara nyingi yamekuwa yakifanyika kwa misingi ya kisiasa na kikabila.
Kulingana na waandamanaji wa Gen-Z, hawana uongozi, kabila wala mrengo wa kisiasa.
Hata hivyo katika maandamano haya kumekuwa na nyuso au watu ambao wameonekana kuwa mstari wa mbele kwa kutoa mchango wa aina mbali mbali katika kuyafanikisha .
Hii ni kutokana na ushawishi wao au ufuasi walionao miongoni mwa vijana na hasa katika mitandao ya kijamii au kwa ajili ya hatua na kauli zao zilizonaswa katika vyombo vya habari .
Baadhi yao ni waandaaji wa maudhui ya mtandaoni huku wengine wakiwa ni wanaharakati wa haki za binadamu na kiraia. Hawa ni baadhi yao na namna walivyochangia katika kufanikisha maandamano hayo ya Kenya ambayo sasa yametulia .
Kasmuel McOure

Chanzo cha picha, Kasmuel McOure/@_KasKazini
Kijana huyu huvalia suti za mvuto na mwenye haiba ya juu. Hii ndio picha unayoiona unapomtazama Kasmuel McOure. Akiwa mwanaharakati na mshawishi wa mitandao ya kijamii Mcoure hakujulikana sana kwa wengi hapo awali, lakini umaarufu wake umechipuka kufuatia maandamano ya hivi karibuni dhidi ya Muswada wa Fedha 2024 nchini Kenya yaliyobadilika na kuwa maandamano dhidi ya serikali ya Kenya na Rais Ruto .
Alijitokeza sio tu kwa suti zake nadhifu, lakini pia kwa hotuba zake kali zilizokuwa za mvuto wa waandamanaji wa Gen-Z zilizoshirikishwa mara nyingi kwenye mitandao ya kijamii kama Isntagram, X na Tiktok. Anatambulika kuwa mwanamuziki anayepiga aina mbalimbali za ala za muziki .

Chanzo cha picha, Kasmuel McOure/@_KasKazini
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamemfananisha kijana huyu mwenye umri wa miaka 33 na mpigania uhuru wa Kenya Tom Mboya, na mpigania haki za raiaWeusi wa Marekani Martin Luther King.
Licha ya Jumbe zake za mtandao wa X (zamani Twitter) na picha zake kutoka kwa maandamano haraka zilisambaa, ushiriki wake sugu wa maandamano ya hivi karibuni nchini Kenya umeimarisha hadhi yake kama mwanaharakati mashuhuri.
Licha ya kukabiliwa na hali ngumu, ikiwamo kutekwa nyara kwa muda mfupi ambako baadhi wanadai kuliandaliwa, Kasmuel aliendelea kutoa maoni yake na kuwatia moyo vijana wengine kuupinga muswada na kuipinga serikali ya Rais William Ruto kwa ujumla
Kulingana naye kuvaa kwake suti hata wakati wa maandamano kunatokana na kwamba katika maisha yake ya utotoni hakuwa na mavazi mazuri aliyoyatamani, suti ikiwa mojawapo. ''Ninavaa suti kila siku, nikiitoa ni wakati naingia kitandandani'' , alisema katika mahojiano kwenye mtandao wa kijamii.
Faith Odhiambo

Chanzo cha picha, Faith Odhiambo
Faith Odhiambo ambaye ni Makamu rais wa Chama cha wanasheria nchini Kenya (LSK) amekuwa kipenzi cha umma baada ya kuwa mstari wa mbele kuwatetea waandamanaji waliokuwa wakikamatwa na polisi .
Mwanasheria huyu mwenye umri wa miaka 38, amesifiwa na kupata umaarufu sana kwa kufanya kazi usiku na mchana kutetea haki na usalama wa waandamanaji na kutaka wale waliokamatwa na kutekwa nyara waachiliwe huru mara moja.
Wakati wa maandamano ,Faith na LSK walijipata na majukumu makubwa ya kuhitajika katika sehemu mbali mbali za nchi ili kuwasaidia watu waliokuwa wamekamatwa au kuchukuliwa kwa njia zisizofaa na polisi .

Chanzo cha picha, Faith Odhiambo/X
Amekuwa akionekana kwenye televisheni na mitandao ya kijamii akilaani mauaji ya waandamanaji, kushiriki binafsi katika kuwatafuta, kushinikiza kuwaachilia na kuwawakilisha waliofikishwa kortini .
Alitumia mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na ule wa X, kuuhamasisha umma kuripoti matukio ya ghasia au kukamatwa kiholela wakati wa maandamano.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Bi Faith ambaye awali alikuwa Katibu ya Bodi ya Shirikisho la wanasheria wanawake pia ni mhadhiri wa sheria katika Chuo kikuu cha Nairobi na ameshikilia nyadhifa mbalimbali za kisheria nchini Kenya.
Mike Muchiri

Chanzo cha picha, Mike Muchiri/Facebook
Akiwa amejilimbikizia Tuzo mbalimbali kama vile tuzo ya Mshawishi bora 2024 (Best Influencer 2022, Tuzo ya DMA Awards, Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 27 aliyeshinda tuzo ya kuwa na ushawishi mkubwa mtandaoni mwaka wa 2019/20, Varsity Awards, GOLD winner, Kuza Awards 2023-Muchiri alikuwa na maarufu hata kabla ya maandamano.
Hivyo basi ilikuwa rahisi kwake kuwahamasisha vijana hususan wa kizazi cha Gen -Z kuukataa Muswada wa Fedha 2024 uliokuwa wakati huo ukisubiriwa kupitishwa na hatimaye kupitishwa na bunge.
Mike Muchiri atakumbukwa kwa kuwa mtu wa kwanza kutafsiri Muswada wa Fedha 2024, kwa lugha yake mama Gikuyu, kwa lengo la kuwafahamisha watu wasioelewa kiswahili au kiingereza kilichokuwemo ndani ya muswada huo.

Chanzo cha picha, muchiri.mike/ Instagram
‘’Nilitafsiri Muswada wa Fedha 2024 katika lugha ya Kikikuyu halafu nikatafuta watu wengine wa kutafsiri kwa lugha nyingine za kiasili ili watu mashinani waelewe yaliyokuwemo ndani ya muswada’’, Muchiri aliiambia runinga moja nchini Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Mike alituma jumbe zake kuwafahamisha wananchi kwamba Muswada wa Fedha 2024 umetafsiriwa kwa lugha za kiasili.
‘’Tumevuka mipaka ya kikabila na kutafsiri muswada wa fedha katika lugha zetu mbalimbali, kuthibitisha nguvu yetu katika umoja. Kwa pamoja, tunasimamia Kenya iliyo bora’’
Mike Muchiri, alikuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha 2024 akifanikiwa zaidi kutokana na kazi anayoifanya-ubunifu wa maudhui ya kidigitali hususan kwenye mitandao ya kijamii.
Eric Omondi

Chanzo cha picha, Erick Omondi
Akiwa msanii maarufu wa vichekesho Afrika Mashariki, na mwanaharakati, Eric Omondi si mgeni katika harakati za kutafuta haki za kiraia nchini Kenya. Kabla ya maandamano ya hivi punde, alishiriki katika maandamano mbali mbali yakiwemo maandamano ya kupinga ufisadi, na kulalamikia kuongezeka kwa kiwango cha mfumuko wa bei za bidhaa .
Bw Omondi mwenye umri wa miaka 41, ameonekana katika maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen-Z nchini Kenya kupinga utendaji kazi wa rais William Ruto na kumtaka aondoke madarakani.

Chanzo cha picha, Erick Ombondi/X
Kulingana na Omondi amekamatwa na polisi ‘’mara 13’’, tangu alipoanza kudai haki za kiraia hususan kudai kupunguzwa idadi ya magavana wa kaunti, wabunge na kuwajibisha maafisa wa serikali ‘’wanaopora mali ya umma’’.
Katika maandamano ya hivi karibuni ya vijana wa Gen- Z Omondi alionekana akiandamana na baadaye kukabiliwa na polisi wa kupambana na ghasia mbele ya bunge siku chache kabla ya waandamanaji kuvamia bunge hilo.
Amekuwa akitumia umaarifu wake kuwahamasisha Wakenya kuukataa Mswada wa Fedha wa mwaka 2024 kupitia kampeni mbali mbali za mtandaoni ikiwa ni pamoja na #RutoMustGo
Wanjiru Wanjira

Chanzo cha picha, Wanjira Wanjiru/ X
Akitumia kauli kali na za moja kwa moja Wanjira Wanjiru amekuwa akionekana kwenye vituo mbali mbali vya habari akitoa tuhuma dhidi ya viongozi wa taifa la Kenya akiwemo Rais William Ruto, Bunge, Serikali na kuwalaumu maafisa wa usalama aliowashutumu kuwapiga na kuwauwa waandamanaji .
Wanjiru Wanjira ni mwanaharakati wa kike wa haki za kiraia . Umaarufu wake pia umeongezeka zaidi katika kipindi cha maandamano ya hivi karibuni ya vijana nchini Kenya.

Chanzo cha picha, Wanjira Wanjiru/ Instagram
Mwanadada huyu mwenye umri wa miaka 28, muasisi mwenza wa Kituo cha Haki za kijamii cha kitongoji cha Mathare (Mathare Social Justice Centre), amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha watu kupinga ufisadi na ukiukaji wa haki za kijamii unaodaiwa kutekelezwa na viongozi wakuu wa Kenya.
Kampeni yake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari iliyogubikwa na kauli kali dhidi ya Rais Ruto na serikali yake imekuwa wazi katika kipindi hiki cha maandamano ya Gen – Z.
Boniface Mwangi

Chanzo cha picha, Boniface Mwangi
Boniface Mwangi ni mwanaharakati, mwanasiasa na mpigapicha na ni mmoja wa Wakenya wenye sauti na ujasiri nchini Kenya.
Bw Mwangi si mgeni katika harakati za maandamano ya kudai utekelezwaji wa katiba na haki za binadamu.
Umaarufu wake ulichipuka kwa kasi kwa mara ya kwanza alipofichua picha za nadra alizozipiga katika matukio ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya. Alipoandaa maonyesho ya picha hizo katikati mwa jiji la Nairobi zilizoibua hisia miongoni mwa Wakenya wengi na jamii ya kimataifa, kuhusu mauji hayo.
Katika kipindi cha maandamano ambayo sasa yamefifia Mwangi alikuwa mstari wa mbele katika kuandaa kampeni za maandamano kwenye mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Instagram na kuhamasisha waandamanaji vijana kushiriki maandamano ya kudai haki za kiraia kufuatia kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa Kenya 2024 na baadaye kudai Rais Ruto andoke madarakani.
Amekuwa akionekana kusambaza jumbe za maandamano chini ya kampeni mbali mbali za mtandaoni kama vile #RejectFinanceBill2024, #RutoMustGo,", #Occupy Parliament, #TotalShutdown na #OccupyState House, #ZakayoStopKillingUS na nyinginezo.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Mwangi anafahamika kwa kushiriki katika misururu mingi ya maandamano nchini Kenya, yakiwemo maandamano dhidi ya mfumuko wa bei za bidhaa na kupinga ufisadi. Alikuwa mstari wa mbele katika kuandaa maandamano mbali mbali ikiwa ni pamoja na maandamano dhidi ya bunge ambapo waandamanaji walipeleka damu ya nguruwe mbele ya bunge kuonyesha hasira zao dhidi ya kile walichokiita ulafi wa wabunge mwaka 2017.
''Tumemwaga damu ya nguruwe ili kuonyesha kuwa wabunge ni walafi kama nguruwe," alisema Boniface Mwangi, mwandalizi wa maandamano ya "Occupy Parliament". Mwanaharakati huyo wa Kenya alikamatwa wakati wa maandamano hayo
Harakati zake za kudai haki za kiraia zimekuwa mara nyingi zikisababisha kukamatwa kwake mara kwa mara.
Hussein Khalid

Chanzo cha picha, Haki Afrika
Hussein Khalid, ni mwanaharakati wa haki za binadamu, mwanasheria na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya HAKI Afrika.
Kuanzia kuandamana , kutembelea majeruhi na familia zao hadi kuhudhuria mazishi, na kudai haki kwa waathiriwa - Khalid ameonekana kuwa pamoja na vijana wa Kenya kwenye harakati zao kikamilifu.

Chanzo cha picha, Hussein Khalid/ X
Aidha ameonekana mara kwa mara katika harakati za kutoa hamasa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii akiwataka kushiriki maandamano ya kuupinga Mswada wa Fedha 2024, yaliyopanuka zaidi na kuwa na madai mbali mbali ikiwa ni pamoja na kumtaka Rais William Ruto aondoke madarakani.
Ushawishi wake katika maandamano haya kwa kiasi kikubwa umeonekana kuwa mkubwa kutokana na uzoefu wake katika utetezi wa haki za kiraia na kibinadamu.
Shadrack Kiprono (Al maarufu Shad Khalif)

Chanzo cha picha, Shadrack Kiprono (shad_khalif)
Kiprono ni mwanaharakati wa haki za kiraia ambaye pia alijitokeza wakati wa maandamano ya Gen -Z kupingwa Mswada wa Fedha 2024, ambao ungeongeza ushuru kwa bidhaa za kimsingi.
Harakati zake za kuhamasisha maandamano zilijikita kwenye mitandao ya Instagram na X.
Alionekana pia kwenye vyombo vya habari akielezea msimamo wake mkali wa kumkata Ruto na utawala wake wote, jambo ambalo lilipelekea kukamatwa kwake, tukio lililorekodiwa na video ya CCTV.
Katika kanda hiyo ya video, mwanaharakati huyo ambaye alionekana akitembea ndani ya jumba la maduka katika eneo la South B mjini Nairobi aliandamwa na kundi la watu ambao walimkamata kwa lazima .

Chanzo cha picha, Shadrack Kiprono (shad_khalif)
Shadrack alikuwa ameonekana katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini humo kabla ya maandamano ambapo alisisitiza msimamo wake kuhusu Mswada wa Fedha wa kuwahimiza waandamanaji kuchukua hatua mitaani.
Tukio la kukamatwa kwake kiliibua hasira miongoni mwa waandamanaji, lakini baadaye aliachiliwa huru.
Imehaririwa na Yusuf Jumah












