Maandamano Kenya: Jinsi bunge lilivyotenda kinyume na matarajio ya Wakenya

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Bunge la Kenya
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Uvamizi wa bunge la Kenya Jumanne tarehe 25 mwezi wa Juni uliotekelezwa na vijana wa Gen Z waliokuwa wakipinga mswada wa fedha wa 2024 ulionesha hasira walionayo Wakenya dhidi ya viongozi wao.

Zaidi ya waandamanji 50 waliuawa wakati wa maandamano hayo kulingana na tume ya kitaifa ya haki za binadamu na mamia wengine wakijeruhiwa na kukamatwa huku idadi isiojulikana wakitekwa nyara na vitengo vya usalama vya serikali.

Haya yanajiri huku wabunge wakirejelea vikao vyao leo Jumanne, tarehe 23 Julai, baada ya mapumziko mafupi.

Hatahivyo wanafungua vikao hivyo katika siku, ambayo waandamanaji wameapa kuendeleza maandamano dhidi ya serikali,baada ya kuhamakishwa na hatua ya rais William Ruto kuwarejesha tena katika baraza la mawaziri ,viongozi sita waliokuwa katika baraza ambalo alilivunja wiki moja iliyopita . Rais Ruto mwishoni mwa wiki aliapa 'kukabiliana vikal' na watakaorejea barabarani akiwataja kuwa 'waporaji' na 'wanaovuruga amani ya nchi'

Maandamano hayo yalianza Nairobi lakini sasa yameenea katika maeneo mengine ya Kenya, ikiwa ni pamoja na Mombasa na hata Eldoret, mji wa eneo la Bonde la Ufa ambayo ni ngome ya kisiasa ya rais William Ruto .

Bunge ambalo limejionesha kama eneo ambalo limekuwa likiwapigania Wakenya na kulinda maslahi yao, sasa limekuwa likikosolewa kwa kupuuza maslahi ya Wakenya.

Taasisi hiyo ya kutunga sheria imeshutumiwa kwa ufisadi kuhusiana na jukumu lake la kuangalia jinsi serikali inavyotekeleza majukumu yake huku baadhi ya wanaharakati wa haki za kibinadamu wakidai kwamba limekuwa likitumiwa na rais kupitisha chochote anachotaka.

Unaweza pia kusoma

Lakini haya yote yalianza wapi?

Bunge la Kenya lina jumla ya viti 349: Kati ya hao kuna wabunge 290 waliochaguliwa moja kwa moja kutoka maeneo bunge huku wanawake 47 wakichaguliwa kutoka kwa kaunti wanazotoka mbali na wawakilishi 12 waliopendekezwa pia wakiteuliwa bila ya kupigiwa kura moja kwa moja.

Muda tu baada ya rais William Ruto kutawazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliopita, alianzisha kampeni za mapema za kujaribu kuwavutia baadhi ya wabunge wa upinzani kujiunga na serikali yake, hali iliodhoofisha upinzani kwa kiwango kikubwa.

Licha ya lalama za kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwamba Kiongozi huyo alikuwa anaenda kinyume na demokrasia ya taifa hili, rais Ruto hakusita kwani aliendelea na mpango wake wa kuwarushia ndoano wabunge wa upinzani.

Na hilo lilipofaulu miswada yote ya serikali imekuwa ikipita bungeni licha ya pingamizi ya hapa na pale ya upinzani uliodhoofika.

Muswada wa fedha 2024

Muswada wa hivi karibuni kupitishwa ulikuwa ule wa fedha wa 2024 licha ya pingamizi kutoka kila upande.

Hatua hiyo ilichukua shinikizo za vijana wa Gen Z ambao waliandamana na hadi kuingia bungeni kumzuia rais kuudhinisha na kuwa sheria.

Muswada huo ulipitishwa na wabunge 195 wanaounga mkono serikali dhidi ya wabunge 106 kutoka kwa upinzani.

Kupuuzwa kwa maoni ya vikao vya umma

Aliyekuwa wakati mmoja Spika wa bunge Kenneth Marende aliambia Nation.Africa kwamba umme umekasirishwa na viongopzi hao kwasababu hawasikizi maoni yao.

Watu wanahisi kwamba bunge limefeli, wanahisi kwamba utendakazi wao upo chini sana ya matarajio yao. Wakati bunge linapofeli katika jukumu lake la kuunda sheria , uwakilishi na kuiangalia serikali , uwezo huo hurudi kwa wananchi waliolipatia, alisema Marende.

Tumeona umma ukijitokeza na kusema kwamba hawana haj ana muswada Fulani, lakini bunge limeshindwa kusikiliza maoni hayo ya waajiri wao na ndiposa hasira ya hivi karibuni, alinukuliwa na Nation.Africa akiongezea.

Athari za ushuru unaopendekezwa

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya Kisiasa Joseph Kioko Wabunge waliwafeli Wakenya baada ya kushindwa kuelezea athari za kupitisha muswada wa fedha wa 2024.

‘Ilimchukua Mbunge Gathoni Wa Wamuchomba kutoka katika chama tawala kuwasihi wabunge wenzake kutopotisha muswada huo kwani ungekuwa na athari mbaya kwa Wakenya, kilio ambacho kiliambulia patupu’, alisema kioko.

Vilevile Bwana Kioko amewashtumu wabunge wa upinzani pia kwa kushindwa kutoa hamasa ya kutosha kuhusu miswada ya kodi kwa Wakenya.

Anasema badala yao viongozi hao wameamua kulalamika kwamba walikuwa na idadi ndogo kuweza kuzuia miswada hiyo kupitishwa bungeni.

Teuzi za kikabila serikalini

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bunge la Kenya

Kuhusu uteuzi wa baadhi ya maafisa serikalini, mchambuzi huyo anasema kwamba bunge lilizembea katika kuhakikisha kuwa kuna uwakilishi kote maeneo yote nchini.

Anasema baadhi ya viongozi walioteuliwa na serikali na kupitishwa na bunge kuhudumu serikali wamekuwa kutoka makabila mawili licha ya kuwa kuna zaidi ya makabila 45 nchini.

‘Watu wanahisi kwamba Wabunge hawawawakilishi ipasavyo na kwamba wamekuwa vipaza sauti wa rais.

Tunoana kwamba hii leo kabla ya muswada kupitishwa bungeni wanaitwa Ikulu ya rais na kuambiwa la kufanya. Hii ina maana kwamba viongozi hawa hawawakilishi watu waliowachagua bali matumbo yao’, alisema bwana Kioko.

Sheria ya nyumba za bei nafuu

Kupitishwa kwa sheria ya Nyumba za bei nafuu , ni suala jingine ambalo Wakenya waliiomba serikali kutolazimisha Wakenya wafanyakazi wasiohitaji nyumba hizo kulipa ushuru wa ujenzi wake.

Ushuru huo unalenga kufadhili ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini, ingawa utekelezaji wake ulizua shutuma nyingi.

Sauti za upinzani na sehemu kubwa ya umma walielezea kusikitishwa na ushuru huo, wakiiona kama mzigo wa ziada licha ya hali ngumu ya maisha wanayopitia.

Vikwazo vya kisheria hapo awali vilichelewesha kupitishwa kwa mswada huo, huku jaji akisimamisha makato kutokana na kukosekana kwa mfumo mwafaka wa kisheria.

Licha ya pingamizi kutoka kwa wabunge wa upinzani, muswada huo ulifanyiwa marekebisho na kuridhiwa na Wabunge.