Je mawaziri 11 walioteuliwa na Rais Ruto ni akina nani?

.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais

Maelezo ya picha, Rais William Ruto
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais William Ruto ametangaza mawaziri kumi na moja kati ya 22 katika baraza lake la mawaziri.

Katika hotuba yake kwa taifa , rais Ruto amesema kwamba idadi ya mawaziri waliosalia itatangazwa wiki ijayo baada ya mashauriano.

Haya yanajiri baada ya shinikizo kuongezeka kwa Rais kuchagua watu wenye uwezo ambao watamsaidia kutekeleza ajenda yake.

Rais amesema kwamba uteuzi huo ambao ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali - unafuatia mashauriano katika sekta ya kisiasa katika jaribio la kurudisha amani na utulivu nchini.

Orodha hiyo pia ilikuwa na Mawaziri sita waliofukuzwa kazi, ambao sasa wanarejea katika wizara tofauti, huku Prof. Kithure Kindiki, Alice Wahome na Adan Duale wakiendelea kushikilia nafasi zao za zamani.

Mawaziri walioteuliwa ni:

  • Kithure Kindiki - Waziri wa masuala ya Ndani
  • Dkt. Debra Mulongo Barasa - Waziri wa Afya
  • Alice Wahome - Waziri wa Ardhi
  • Aden Duale - Waziri wa Ulinzi
  • Davis Chirchir - Waziri wa Uchukuzi
  • Rebecca Miano - Mwanasheria Mkuu
  • Soipan Tuya - Waziri wa Mazingira
  • Julius Migosi - Waziri wa Elimu
  • Eric Muriithi - Waziri wa Maji
  • Dr Margaret Ndungu- Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia
  • Andrew Karanja - Waziri wa Kilimo

Wateule wapya watalazimika kuchunguzwa kabla ya kuzingatiwa ili kuidhinishwa na bunge kama Mawaziri.

"Ninaendelea kufanya mashauriano katika sekta mbalimbali kuhusu usawa wa Baraza la Mawaziri ambalo nitaliteua hivi karibuni. Mashauriano yapo katika hatua ya juu na michakato ya ndani katika sekta mbalimbali inaendelea ili kuwezesha uteuzi wangu wa uwiano wa Baraza hili la Mawaziri,” alisema Rais.

.
Maelezo ya picha, Waziri wa Ulinzi Aden Duale ni miongoni mwalioteuliwa kwa mara ya pili katika wizara zao

Uteuzi huo unajiri huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa katika Muungano wa upinzani nchini Azimio ambapo baadhi ya viongozi wamepinga kuhusu kufanyika kwa mazngumzo yoyote yatakayopelekea baadhi ya viongozi wao kuorodheshwa katika baraza hilo.

.
Maelezo ya picha, Alice Wahome ameridishwa katika wizara yake ya Ardhi

Vyama tanzu vya Muungano wa Azimio vyatofautiana

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Huku Chama cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kikionekana kuunga mkono mazungumzo ya kuunda serikali ya Umoja nchini, Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na wenzake wa vyama vya Narc Kenya, Dap Kenya na Jubilee wamejitenga na mpango huo.

Awali muda mchache kabla ya hotuba hiyo ya Rais, Kinara wa chama cha Wiper katika Muungano wa Azimio Kalonzo Musyoka alipinga mpango wowote wa kuwajumuisha viongozi wa upinzani katika serikali hiyo ya Muungano.

Alidai kuwa ushiriki wowote ni sawa na usaliti kwa vijana wa Kenya ambao wameendelea kutoa maoni yao dhidi ya mazungumzo wiki chache zilizopita kupitia maandamano dhidi ya serikali.

"Hatutashiriki au kuunga mkono mapendekezo ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Kenya Kwanza. Huu ni usaliti dhidi ya Wakenya, hasa kwa Gen Z na milenia, ambao wamelipa gharama ili kuondoa nchi hii kutoka kwa utawala mbaya wa Kenya Kwanza, ushuru wa juu, ufisadi, ukabila, ukosefu wa ajira, na gharama ya juu ya maisha,” alisema.

“Iwapo mwanachama wetu yeyote atachagua kujiunga na serikali inayopendekezwa na Kenya Kwanza ya umoja wa kitaifa, hatutakuwa sehemu ya uamuzi huo; watakuwa wanajiunga kwa nafasi zao binafsi, si kwa niaba ya Azimio,” alihitimisha

Wiki moja iliopita rais Ruto alishinikizwa kuvunja baraza lake la mawaziri na waandamanaji wa Gen Z waliodai kwamba , baadhi ya mawaziri hao walikuwa wakikabiliwa na kesi za mauaji, ufisadi huku wengine wakidaiwa kukosa hata vibali vya kuongoza wizara walizopewa.