Maandamano Kenya: Ukweli kuhusu farasi wa polisi walioibiwa, na habari nyingine za kupotosha

Waandamanaji

Chanzo cha picha, Getty Images

Na Peter Mwai

BBC Verify

Maandamano ya kupinga Mswada wa Kifedha wa 2024 yalipangwa na washiriki kuhamasishana kwa kiwango kikubwa kupitia mitandao ya kijami, lakini kando na taarifa za kweli kulisheheni taarifa za kupotosha ambazo zilienea sana.

Moja ya mifano ambayo wengi hawakuweza kubaini ilikuwa ya kupotosha ilikuwa ni madai kwamba mwandamanaji mmoja alikuwa amefanikiwa kutoroka na farasi wa polisi.

Ukweli kuhusu farasi wa polisi

Mkondo wa pili wa maandamano Alhamisi wiki iliyopita, polisi wa kukabiliana na ghasia walijitokeza barabarani wakisaidiana na kikosi cha polisi wanaotumia farasi.

.

Chanzo cha picha, Social Media

xx

Chanzo cha picha, Social Media

Baada ya muda, taarifa zilianza kuenea kwamba mmoja wa farasi hao alikuwa ameibiwa na mmoja wa waandamanaji kijana na kwamba polisi walikuwa wamemsihi kijana huyo kuwarejeshea farasi wao.

Video zilizowaonyesha vijana wawili wakiwa na farasi wawili waliofanana na wale waliokuwa wakitumika na polisi wakipita mbio barabarani, na hata kupitia nje ya kituo cha polisi zilisambaa sana.

Baadaye taarifa zikaashiria ni kana kwamba farasi walioibiwa walikuwa wawili, kutokana na hali kwamba polisi walioonekana kwenye video walikuwa wawili.

Siku iliyofuata, baadhi ya watu mtandaoni walifanyia utani wakisema walikuwa hawafahamu farasi wanafaa kupewa nini kama kiamsha kinywa.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna farasi wa polisi aliyekuwa ameibiwa.

Video zilizokuwa zikisambaa zilikuwa zimepakiwa kwenye mtandao wa TikTok zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Vijana hao wawili wamekuwa na farasi hao kwa muda, na kwenye akaunti hiyo ya TikTok wanaonekana na farasi hao katika maeneo mengi zaidi katika video zilizochapishwa kabla ya siku hiyo ya maandamano.

Soma pia:

Video ya tamasha nchini Ghana

Baada ya maandamano ya Jumanne wiki hii, wakati watu wakirejea makwao jioni, milio mikali ya risasi ilisikika katika mtaa wa Githurai, kaskazini magharibi mwa jiji la Nairobi.

tt

Chanzo cha picha, Social Media

Mtaa huo unapatikana takriban kilomita 15 kutoka katikati mwa jiji na wengi wanaofanya kazi jijini huishi humo.

Taarifa zilienea kwamba watu wengi walikuwa wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na vikosi vya usalama, na kukawa na video iliyosambaa sana mtandaoni ikidaiwa kuonyesha matukio katika mtaa huo.

Ilikuwa ni video ya kundi kubwa la watu wenye mienge waliokuwa wakipita barabarani, na baadhi ya watu walidai ni mienge iliyowashwa na wakazi kwa heshima ya watu waliouawa mtaani humo.

Lakini BBC iliwahi kuiangazia video hiyo [link https://www.bbc.com/pidgin/articles/cv2eyvpp3vgo ], na kubaini kwamba ilikuwa imetoka Ghana takriban miaka miwili iliyopita.

Na hii haikuwa mara ya kwanza kwa video hiyo kusambazwa kwa njia ya kupotosha.

Polisi hawakuidhinisha maandamano

Wakati mmoja, kulikuwepo na taarifa iliyodaiwa kuandikwa na Inspekta Mkuu wa Polisi akikubalia maandamano kufanyika na kueleza masharti ya kufuatwa.

Lakini taarifa hiyo ilikuwa si ya kweli na baadaye polisi waliikanusha.

Video ya ukatili ya polisi ni ya zamani

Kumekuwepo na video iliyokuwa ikisambaa ikiwaonyesha maafisa wa usalama wakimpiga vikali kijana mmoja.

.

Chanzo cha picha, Social Media

Ilidaiwa kuwa tukio la sasa hivi wakati wa maandamano.

Lakini baada ya kuchunguza, tumebaini kwamba video hiyo imekuwepo kwa muda mtandaoni. Tulipata chapisho la video hiyo la mwaka 2022, ingawa bado hatujafanikiwa kubaini hasa video hiyo ilichukuliwa wapi.

Picha ya mwandamanaji kutoka Ufaransa

Kulikuwepo na video na picha za kutoka nje ya nchi ambazo zilitumiwa kuonyesha ustadi wa waandamanaji, mfano hii ya mwanandamanaji aliyeonekana akitumia raketi ya tenisi kunasa na kurusha tena mabomu ya kutoa machozi.

Picha hii ilipigwa mwaka 2016 nchini Ufaransa wakati wa maandamano ya kupinga mageuzi ya leba nchini humo.

tt

Chanzo cha picha, Social Media

Na kumekuwa na video pia ya mwanamanaji akirejeshea polisi bomu la kutoa machozi kwa kutumia shuti kama la kandanda.

.

Chanzo cha picha, Social Media

Video hiyo imekuwa mtandaoni tangu 2020.