Kwanini rais wa Kenya anataka wananchi wampende mtoza ushuru

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Basillioh Rukanga
- Nafasi, BBC News, Nairobi
Wakenya wanaendelea kuelewa ukweli na maana ya msemo wa zamani kwamba kodi, pamoja na kifo, ndio vitu viwili pekee vyenye uhakika katika maisha.
Hii ni kwa sababu Rais William Ruto anajaribu kuwashawishi kwamba wanapaswa kutoa pesa nyingi zaidi walizotafuta kwa jasho lao kama ushuru, akisema kwamba, kodi wanayotozwa ni kidogo sana.
Hivi karibuni alihoji kwamba Wakenya "wamefanywa kuamini kuwa wanalipa ushuru wa juu zaidi" wakati ukweli ni kwamba, alisema, mzigo wao wa ushuru ulikuwa chini ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine barani Afrika na kwingineko.
"Lazima tuongeze ushuru wetu," alisema, lakini akakiri kwamba hatua ya kutekeleza hilo "itakuwa ngumu".
Tangu achaguliwe kuwa rais mnamo Agosti 2022, serikali ya Bw Ruto imeongeza ushuru uliokuwepo kwa kiasi kikubwa huku pia ikianzisha kodi mpya.
Ushuru unaotozwa kwa mishahara umepanda, ushuru wa mafuta umeongezeka maradufu na watu pia wanalipa ushuru mpya wa ujenzi wa nyumba nafuu na wanatakiwa kulipa zaidi kwa ajili ya bima ya afya.
Bw Ruto anahoji kwamba ikiwa watu wanataka huduma bora za umma na kupunguzwa kwa mzigo wa deni wa nchi, basi wanapaswa kulipa zaidi.
Lakini wengi wameghadhabishwa.
Kutozwa kwa baadhi ya kodi mpya, huku gharama ya maisha ikiwa imepanda, kulisababisha maandamano makubwa mwaka 2023.
Leo hii, mazungumzo ya kawaida baina ya raia mara nyingi hutawaliwa na uchungu wa kutozwa ushuru, na maoni ya rais yamewakasirisha Wakenya ambao tayari wanahisi kulemewa na mzigo wa gharama ya maisha.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bw Ruto alisema kwamba mwaka uliopita, ushuru uliokusanywa na serikali ulifikia asilimia 14% ya thamani ya uchumi kwa ujumla, takwimu ambayo inajulikana kama uwiano wa ushuru ukilinganisha na Pato la Taifa (tax-to-GDP ratio), ilhali kiwango cha “mataifa mengine yenye vigezo sawa na Kenya katika bara la Afrika ni cha kati ya 22% na 25% kwa jumla”.
Hii "inamaanisha kuwa kodi zetu ziko chini sana ukilinganisha na zile za wenzetu", rais alisisitiza.
Hata hivyo, haikuwa bayana alikuwa akimaanisha nchi zipi aliposema "wenzetu". Ingawa ni kweli kwamba Afrika Kusini, Morocco, Mauritius na Namibia zote zina uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa ambao uko karibu au zaidi ya 20%, zingine nyingi, ikiwa ni pamoja na Nigeria, Ghana, Uganda, Tanzania na Zambia, hazina.
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Afrika (AU), wastani wa uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa katika bara zima mwaka 2021 ulikuwa 15.6% - idadi ambayo haiko juu sana kuliko ya Kenya.
Wakili na kiongozi mmoja katika upinzani Miguna Miguna alitoa muhtasari wa hisia ambazo wengi wanahisi.
"Wakenya wanatozwa ushuru kupita kiasi, wanakandamizwa, wanatumiwa vibaya na kunyanyaswa," alichapisha kwenye mtandao wa X, ambao zamani ulifahamika kama Twitter, akiongeza kwamba watu "hawapati thamani ya hata 1% kutoka kwa ushuru wetu!"
Licha ya ghadhabu hizo, kodi zaidi ziko njiani - rais ameeleza umuhimu wa kuongeza ushuru katika miaka michache ijayo hadi angalau 20% ya Pato la Taifa kufikia mwisho wa muhula wake mnamo 2027.
Ametetea hatua ya kupandishwa kwa kodi zaidi ili kuongeza mapato ya serikali na kupunguza ukopaji. Kenya ina deni la kitaifa la karibu $80bn (£62bn), na sehemu kubwa ya deni hilo lilirithiwa kutoka kwa tawala zilizopita.
"Utawala uliopita ulikuwa na mtindo wa kukopa kupita kiasi. Utawala wetu unasawazisha, na kulipa madeni pamoja na kuimarisha tena uchumi," msemaji wa serikali Isaac Mwaura aliiambia BBC.
Tayari, pendekezo la bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa kifedha linajumuisha kodi mpya ambazo zinaonekana kutopendwa, ikiwa ni pamoja na ushuru wa lazima kwa wamiliki wa magari na ushuru wa mauzo ya mkate pamoja na miamala ya kifedha.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini mwanauchumi Odhiambo Ramogi anahoji kuwa kuangalia suala hili kwa mtazamo wa uwiano wa ushuru kwa Pato la Taifa haifai na sio suluhu inayohitajika.
Anasema kuwa tatizo sio suala la kodi kuwa chini sana, na kwamba tatizo ni kuwa hakuna ufanisi katika ukusanyaji wa kodi, na kwamba utawala mbovu unamaanisha kuwa kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha katika matumizi mengi ya serikali.
Mwanauchumi huyo anadokeza kuwa licha ya hatua za sasa, badala yake uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa umeshuka, hali inayoonyesha kuwa watu wengi zaidi wanazuilia pesa zao.
Anahusisha hili na jambo linalofahamika kama athari ya "Laffer Curve" - nadharia ambayo inajaribu kuelezea uhusiano kati ya kodi na mapato. Inapendekeza kwamba wakati kodi zinapovuka kiwango fulani, zinapunguza motisha ya watu kufanya kazi na kulipa ushuru.
"Viwango vya juu vya ushuru kwa kawaida husababisha ukusanyaji mdogo wa ushuru," anasema.
Bw Ramogi anasema kuwa nchi za Magharibi zilizo na viwango vya juu vya ushuru kwa ujumla huwa zina huduma nzuri za umma.
Kinyume chake, anahoji, licha ya kuwa na kodi nyingi zinazowakabili Wakenya, watu bado wanapaswa "kulipia karo za shule, bili za hospitali, lazima ulipie huduma zote za umma, ni ushuru mara mbili kila mahali".
Anasema ili kukua, Kenya inapaswa kwanza kuhakikisha ushuru unakusanywa na kutumiwa kwa njia ipasavyo, na pia kukomesha ufisadi - tatizo ambalo msemaji wa serikali anasema Rais Ruto tayari "ameeleza wazi" kuhusu kulishughulikia.
Ken Gichinga, mkuu wa kampuni ya uchanganuzi ya Mentoria Economics, anaongeza kuwa ushuru wa juu unaweza kusababisha athari zaidi kwasababu huongeza gharama ya kufanya biashara, ambayo husababisha kufungwa kwa biashara hizo, watu kupoteza ajira na hatimaye kupunguza kiwango cha ushuru unaokusanywa.
Pia kuna baadhi ya wanaopinga mtazamo wa rais kwamba kuongeza kodi ili kuwiana na baadhi ya nchi nyingine za Kiafrika kutaleta matokeo bora ya kiuchumi.
Mwanauchumi na mbunge wa zamani Billow Kerrow anataja mataifa mawili makubwa kiuchumi barani Afrika: Nigeria, ambayo mwaka 2021 ilikuwa na uwiano wa chini wa kodi kwa Pato la Taifa, na Afrika Kusini, ambayo ilikuwa mojawapo ya nchi zilizo na uwiano wa juu zaidi barani. Kwa kifupi, kiwango cha kodi sio ishara ya nguvu au ukubwa wa uchumi.
"Mtazamo wa kushangaza wa serikali kuhusu ushuru unapotosha kabisa," Bw Kerrow aliambia runinga ya KTN.
Lakini rais anaonekana kutotikisika katika uamuzi wake.
"Nina kazi kubwa ya kufanya ili kueleza watu wanielewe," alisema.
"Watu watalalamika lakini najua hatimaye watashukuru... Inabidi tuanze kuishi kulingana na uwezo wetu."
End of Unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Peter Mwangangi












