Makali ya shoka la gharama ya maisha yanavyoziponda nchi za Afrika Mashariki

wateja

Chanzo cha picha, AFP

Na Peter Mwangangi

BBC Swahili, Nairobi

Raia wa mataifa tofauti ya Afrika Mashariki wamekuwa wakishuhudia ongezeko la gharama ya maisha baada ya bei za huduma na bidhaa kadhaa kupanda.

Baadhi ya bidhaa ambazo zimeathirika ni chakula, mafuta ya dizeli na petroli, unga, nauli, miongoni mwa nyingine.

Bei za mafuta

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Kati ya Oktoba mwaka wa 2022 na Oktoba mwaka 2023, bei ya lita moja ya petroli nchini Kenya iliongezeka kwa asilimia 21.7% huku dizeli ikipanda kwa asilimia 25.8% kwa lita, kwa mujibu wa shirika la takwimu nchini humo KNBS.

Nchini Tanzania katika kipindi sawa na hicho, bei ya lita moja ya petroli iliongezeka kwa asilimia 13.4% kutoka Tsh 2,886 hadi Tsh 3,274 mjini Dar Es Salaam, kwa mujibu wa Mamlaka ya kawi na maji EWURA.

Hali kadhalika bei ya lita moja ya dizeli mjini Dar Es Salaam iliongezeka kwa asilimia 11.8% kutoka Tsh 3,083 hadi Tsh 3,448.

Nchini Uganda, bei za mafuta zimesalia kuwa juu. Mnamo Novemba mwaka wa 2023, lita moja ya petrol iliuzwa kwa jumla ya UGX 5,660, na dizeli kuuzwa kwa UGX 5,270 kwa lita.

Athari ya kodi

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Grace Mulinge, Mtaalamu wa kodi kutoka shirika la ukaguzi wa mahesabu la Ernst & Young (EY) anasema mabadiliko katika utozaji wa ushuru yamekuwa na athari kwa gharama ya maisha, akitoa mfano wa taifa la Kenya ambalo limeshuhudia mabadiliko makubwa katika suala hili mwaka 2023.

“Kulikuwa na ruzuku kwenye mafuta lakini ikaondolewa na rais William Ruto. Kabla ya kuondolewa kwa ruzuku hiyo, bei za mafuta zilikuwa chini lakini sasa zimeongezeka. Pia kuna kodi ambazo zimeongezewa kama vile kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 8% hadi 16%, na kodi kwa wanaopata mishahara. Hii imesababisha fedha zinazobakia kwa wafanyakazi kuwa kidogo na hivyo kupunguza uwezo wao wa kununua bidhaa,”anasema Grace.

Mtaalamu wa uchumi Ken Gichinga anasema hali ya sasa pia imechangiwa na sababu zingine za ndani na nje katika miaka ya nyuma, kuanzia janga la Covid-19 mwaka 2020, uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2022, vita vya Urusi na Ukraine, na pia vita vya Israel na Hamas katika ukanda wa Gaza.

Makadirio ya ukuaji wa uchumi 2024

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Benki ya Dunia inakadiria kwamba ukuaji wa uchumi wa mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika utashuka kutoka asilimia 3.6% mwaka wa 2022 hadi kufikia asilimia 2.5% mwaka 2023. Hata hivyo inasema huenda hali ikaimarika kidogo katika mwaka wa 2024.

Benki ya maendeleo ya Afrika AfDB pia ina mtazamo wa matumaini kwamba hali itaimarika. Katika ripoti yake ya hivi karibuni, benki hiyo inasema kuwa uchumi wa mataifa ya Afrika Mashariki utashuhudia ukuaji wa jumla ya asilimia 5.8% katika mwaka 2024.

“Kwa kiasi kikubwa, mapato ya nchi za Tanzania, Uganda, Kenya hutokana na serikali kutumia pesa kwa miradi ya miundombinu kama vile barabara, madaraja, lakini mapato yanayotokana na sekta ya kibinafsi sio kubwa licha ya kuwa watu wengi wako katika sekta hiyo. Serikali hizi zinahitaji kuwekeza katika mikakati ya kuimarisha sekta ya kibinafsi ili kuongeza nafasi za ajira na mapato ya wananchi,”anasema Ken.

Wakati bei za bidhaa zinaongezeka lakini kipato kiko pale pale, mtu binafsi anaweza kufanya nini ili kumudu hali?

Haya ni mambo matatu ambayo wataalamu wanasema unafaa kuzingatia:

  • Punguza matumizi yasiyokuwa ya lazima: Tumia fedha ulizo nazo katika kukidhi mahitaji muhimu kama chakula, makazi na kadhalika.
  • Pia punguza matumizi katika mambo yasiyokuwa muhimu sana kamavile burudani, pombe na sigara. Unaweza pia kutumia teknolojia kwa manufaa yako. Kwa mfano, badala ya kutumia nauli kwenda mjini kukutana na mtu ambapo pia utagharamikia chakula, mnaweza kuzungumza kwa njia ya mtandao ukiwa nyumbani.
  • Nunua bidhaa kwa jumla: Badala ya kununua bidhaa katika maduka ya reja reja, unaweza kununua kwa wingi katika maduka ya jumla kwa bei nafuu. Katika hali hii pia utaweza kutumia bidhaa hizo kwa muda mrefu.

  • Kwa wafanyabiashara wanaotaka kujiendeleza, zingatia mikopo mbadala isiyokuwa na riba kubwa. Unaweza kuzungumza na familia au marafiki, ambao masharti yao yatakuwa na afueni kidogo kuliko yale ya taasisi za kifedha.

Imehaririwa na Yusuf Jumah