Maandamano Kenya: Tunachofahamu kufikia sasa

Na Abdalla Seif Dzungu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polisi wakikabbiliana na waandamanaji Kenya

Katika siku ya pili ya maandamano yaliotishwa na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini Kenya licha ya hali ya kawaida ya biashara kuathirika siku ya kwanza ya maandamano .

Kulingana na uchunguzi wetu, maeneo ambayo utulivu umeanza kurejea hatahivyo yameandikisha idadi kubwa ya maafisa wa polisi huku biashara nyingi zikiendelea kufungwa kwa siku ya pili mfululizo.

Maandamanbo hayo yameitishwa na upinzani kupinga gharama ya juu ya Maisha na muswada wa fedha wa 2023 uliozuiwa na mahakama baada ya bunge kuunga mkono. Lakini ni nini haswa kinachoendelea kote nchini?

Tunachokifahamu kufikia sasa

Tukianzia katika kaunti ya Kisumu ni kwamba baada ya hali mbaya ya mshikemshike kati ya waandamanaji na polisi hapo jana , hii leo hali imekuwa tulivu ijapokuwa biashara zimefungwa na hakuna kinachoendelea kwasababu mji umesalia kuwa mahame ijapokuwa idadi ya maafisa wa polisi imeongezeka katika mji huo .

Vilevile katika mkoa wa kati kulikuwa na hali tete katika kituo cha polisi cha Wanguru huko Mwea baada ya jamaa na familia ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kufika katika kituo hicho wakitaka kiongozi huyo aliyekamatwa hapo jana kuachiliwa la sivyo awasilishwe mahakamani.`Hatahivyo mbunge huyo alidaiwa kuondolewa katika kituo hicho na duru zimearifu kwamba amehamishwa katika kituo kimoja cha polisi mjini Nairobi.

Katika eneo la Saboti kituo cha biashara cha Matisi , mtu mmoja amedaiwa kudungwa kisu hadi kufa alipokuwa akijaribu kuzima moto uliokuwa umewashwa na waandamanaji.

Mashirika ya haki za kibinadamu yaonya dhidi ya utumizi wa nguvu kupitia kiasi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji Kenya

Wakati huohuo mashirika mawili tofauti ya haki za binadamu yametaja idadi ya waliofariki katika maandamano nchini Kenya kufikia watu 30 tangu maandamano ya kuipinga serikali yaanze wiki mbili zilizopita.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shirika la Amnesty International kupitia Mkurungenzi wake Mkuu Irungu Houghton wakati huohuo limeshtumu utumiaji wa nguvu kupitia kiasi unaotekelezwa na maafisa wa polisi dhidi ya waandamanaji.

Vilevile shirika la haki zi kibinadamu la Haki Afrika limewataka maafisa wa polisi kutotumia kile walichokitaja kuwa nguvu kupitia kiasi dhidi ya waandamanaji wanaopigania haki yao.

Kiongozi wa shirika hilo Hussein Khalid amesema kwamba takriban watu 27 wameripotiwa kufariki tangu maandamano hayo ya kuipinga serikali yalipoaza wiki mbili zilizoisha kutokana na nguvu za kupitia kiasi zinazotumiwa na maafisa wa polisi.

Hivyobasi Shirika hilo limetoa wito kwa vinara wawili Rais William Ruto na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kulegeza misimamo yao na kuendelea na majadiliano ili kutafuta suluhu ya mambo yanayowakumba Wakenya kwa sasa.

Wamesema kwamba asilimia kubwa ya wanaoathirika ni Watoto na wanawake huku wakitaka hali hiyo itatuliwe kwa haraka.

Polisi wakabiliana na waandamanaji Kibra

Vilevile katika eneo la Kibra ambalo lipo jijini Nairobi,

Ghasia zinaendelea kuripotiwa huku polisi wakikabliana na baadhi ya waandamanaji katika mtaa wa `Woodely.

Tukisalia jijini Nairobi katika eneo la Mathare: Maafisa wa usalama wanazidi kuwazuia waandamanaji hususan katika eneo la number 10. Moshi mweusi umetanda katika eneo hilo kutokana na vitoa machozi. `Polisi wanaendelea kuwazuia waandamanaji na kuwarudisha hadi katika makazi yao.

Katika eneo la Kangemi lililoshuhudia hali mbaya ya maandamano siku ya Jumatano utulivu mdogo umerejea ijapokuwa kuna idadi kubwa ya polisi. Matairi yaliokuwa yamewashwa moto hapo jana yamekuwa yakiendelea kuondolewa katika baadhi ya barabara. Baadhi ya raia wamefungua biashara zao huku usafiri ukiendelea kama kawaida.

Rais Ruto awapongeza polisi kwa kukandamiza Maandamno

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais William Ruto

Naye akizungumzia kuhusu maandamano hayo Rais William Ruto ambaye yuko eneo la Isio , amesema kwamba serikali yake itaendelea kulinda usalama na demokrasi ya taifa la kenya kwa hali na mali.

Akizungumza baada ya kufungua barabara katika eneo hilo, Rais Ruto amesema kwamba serikali yake haiwezi kukubbali mtu mmoja kukandamiza uchumi wa taifa kupitia maandamano.

Alisema lazima tulinde amani yetu huku akiwaambia wale wanofanya maandamano kwamba hali iliopo kwasasa haiwezi kuimarika kupitia maandamano na badala yake akawataka kuunga mkono serikali katika sera zake za kilimo na muswada wa nyumba ili kubuni ajira kwa vijana .

Ruto vilevile aliwapongeza maafisa wake wa polisi kwa kusimama imara na kuzima maandamano.

Katika eneo la Nakuru: Hali ni tofauti, shughuli katika eneo la shabab – zimerejea kama kawaida huku wafanyabiashara wakirudi kazini. Maafisa wa usalama wameimarisha doria ili kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha. Watu 37 wamedaiwa kukamatwa katika siku ya kwanza ya maandamano.

Shule kufunguliwa leo

Mjini Nairobi licha ya serikali kutangaza kuwa masomo yataendelea shuleni siku ya Alhamisi baada ya shule kufungwa hapo jana, ni shule chache zilizofuata agizo hilo na kufungua taasisi hizo.

Miongoni mwa shule zilizofunguliwa, ni walimu tu waliojitokeza kwa wingi huku wanafunzi wachache wakionekana.

Katika kaunti ya Kisumu shule nyingi zimeendelea kufungwa licha ya agizo la serikali kuzitaka zifunguliwe hii leo.

Viongozi wa dini wawataka Raila na Ruto kujadiliana

Na kule mjini Mombasa takriban Viongozi 200 wa dini waliokuwa wakikongamana wamewataka Vinara wawili waje pamoja na kuzungumza. ‘’Hakuna haja ya kujipiga kifua. Vita sio suluhu pande zote mbili ni vizuri kuketi chini ili kuongea .

Na kisiwani Lamu viongozi wa dini vilevile wamewataka viongozi wawili Raila Odinga na William Ruto kufanya majadiliano.

‘’Ni jambo linalokhera kuona watu wakipoteza mali na Maisha yao. Tunaomba Ruto na upinzani kukaa na kufanya majadiliano. Mataifa ya nje wanaopoona maandamano inaathiri utalii na biashara katika kisiwa cha Lamu’’, walihitimisha.