Maelfu ya waandamanaji wasisitiza kuondolewa kwa Muswada wa fedha wa 2024 jijini Nairobi
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili

Chanzo cha picha, Reuters/Monica Mwangi
Makabiliano makali yamezuka katikati ya mji wa Nairobi na viungani mwake baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji wanaopinga muswada wa fedha wa 2024 na kuwatawanya.
Umati wa waandamanaji uliokuwa umebeba mabango na kuimba nyimbo za kuikashifu serikali ulianza kukusanyika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Nairobi kuanzia saa moja alfajiri.
Waandamanaji hao wanaoshirikisha vijana wa Gen Z na ambao wamejihami kwa maji na simu za rununu kuelezea msimamo wao dhidi ya muswada huo waliandamana wakati ambapo bunge likijadili marekebisho ya muswada huo wa fedha.
Bungeni

Chanzo cha picha, Reuters
Wabunge wa upinzani ambao awali walikuwa wamewasilisha mapendekezo ya kurekebisha muswada huo, walifutilia mbali marekebisho hayo na kutaka muswada huo kukataliwa wote kwa jumla.
Muswada huo ulipita awamu ya pili wiki iliyopita baada ya wabunge 204 kuunga mkono huku 115 wakiupinga.
Baada ya hapo muswada huo utasogea awamu ya tatu ambapo Bunge litaupigia kura ukiwa na marekebisho mapya.
Maandamano hayo yalijiri huku shughuli za biashara katikati ya mji huo zikisitishwa kufuatia kufungwa kwa idadi kubwa ya maduka na shughuli zengine.
Siku ya Jumatatu, serikali ilionya Wakenya wanaopanga kuandamana Jumanne dhidi ya aina yoyote ya ghasia na uharibifu wa mali.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki, mbali na kukiri kwamba kila Mkenya ana haki ya kuandamana au kulaani, alisisitiza kwamba waandamanaji hawapaswi kukiuka haki na uhuru wa wengine.
Barabara zafungwa Nairobi

Chanzo cha picha, BBC/Gladys Kigo
Maafisa wa usalama jijini Nairobi nchini Kenya, mapema leo walifunga barabara kadhaa muhimu zinazoelekea kwenye majengo ya Bunge kabla ya maandamano makubwa ya kupinga mswada wa fedha.
Barabara za Parliament Road na City Hall Way, miongoni mwa zingine, zimefungwa kwa magari na watembea kwa miguu huku hatua za usalama zikiimarishwa.
Magari ya polisi ya kuzima ghasia na malori yamewekwa katika barabara hizo kama vizuizi katika njia kuu zinazoelekea bungeni.
Maandamano hayo, yaliyoandaliwa na mashirika mbalimbali ya kiraia yamevutia uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana kote nchini.

Pingamizi dhidi ya Muswada wa fedha wa 2024

Chanzo cha picha, Getty Images
Waandalizi wa maandamano hayo, vijana ambao wanafahamika kama Gen Z wanatoa wito kwa zaidi ya watu milioni moja kujitokeza na kushiriki.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Kenya Reject-Finance Bill 2024," yamekuwa yakishika kasi na kuvutia maelfu ya watu mitaani kuonyesha upinzani wao.
Waandamanaji wanahoji kuwa mpango wa kukusanya kodi zinazopendekezwa katika muswada huo zitazidisha hali ngumu ya kiuchumi kwa Wakenya wa kawaida.
Tayari Shule kote nchini zimeagizwa kufungwa mapema kwa mapumziko ya katikati ya muhula ili kuwaepusha wanafunzi kutokana na matokeo ya vurugu.
Imeandaliwa na Seif Abdalla












