Kwanini maandamano ya Kenya yanaweza kuleta msiba Tanzania na Uganda?

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Kenya

Chanzo cha picha, GMG

Wiki ya pili sasa kumekuwa na maandamano katika miji kadhaa ya Kenya yaliyoitishwa na upinzani chini ya kinara wa ODM na mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu, Raila Odinga.

Kwa mujibu wa Upinzani maandamano hayo ni kuonyesha hisia zao kwa masuala kadhaa wanayoyadai. Moja kubwa ni kwamba uchaguzi uliopita wa Kenya ulikuwa wa udanganyifu na lingine serikali kushindwa kuwasaidia Wakenya kukabiliana na hali ya "kupanda" kwa gharama ya maisha.

Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa mpaka sasa kwa kupigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakikabiliana na maelfu ya waandamanaji katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Katika maandamano hayo kunadaiwa kufanyika kwa uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo kuvamiwa kwa mali za Bwana Odinga na shamba la familia ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta ambaye anamuunga mkono Odinga.

Kwa mujibu wa Bwana Odinga maandamano haya yaliyoanza wiki iliyopita na ambayo yatafanyika kila Jumatatu na Alhamisi kuanzia wiki hii hayatakuwa na kikomo.

Hatua hiyo inazidi kuongeza wasiwasi wa kiusalama kwa wakenya kutokana na mamlaka kuyapinga huku yakizuiwa kwa nguvu zote na jeshi la Polisi, lakini wasiwasi mkubwa unaweza kuhamia nje ya mipaka hasa nchi jirani za Tanzania na Uganda.

Kwanini Tanzania na Uganda zilie na ziwe na wasiwasi kwa maandamano ya Kenya?

TZ-KE

Chanzo cha picha, KAMPALA UNIVERSITY

Unaweza kujiuliza maandamano yafanyike Kibera au Mathare huko Nairobi lakini Dar es Salaam, Arusha, Tanga na miji mengine ya Tanzania ipatwe na msiba? au Moroto, Mbale, Jinja na Kampala huko Uganda wawe na wasiwasi wa maisha yao?

Tanzania, Kenya na Uganda ni mataifa ndugu kwa mambo mengi. Kuanzia kijamii, kiuchumi na kibiashara na hata kimazingira. Undugu huu unafanya taifa mojawapo linapopatwa na msukosuko, kwa namna moja ama nyingine msukosuko huo unaweza kuathiri shughuli na maisha ya wananchi wa taifa lingine kati ya haya.

Uganda ndiyo nchi inayoongoza Afrika kwa karibu miaka 10 iliyopita kwa kuagiza bidhaa zaidi na nyingi za Kenya, ndiye mteja namba moja Afrika kama sio duniani ukiacha mwaka jana Marekani kuongeza kwa 47% uagizaji wa bidhaa za kutoka Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa za serikali, katika nusu ya mwaka 2022 Uganda iliagiza karibu bidhaa za Sh36.2 za Kenya ikiwa ni sawa na dola karibu 27.3mil za Marekani.

Huwezi kuacha kuoanisha maandamano ya Kenya na hali ya maisha, biashara na shughuli zingine za Uganda. Maandamano yakiongezeka Kenya, Uganda itaingia msibani kama ilivyo kwa Tanzania.

Kibiashara - bidhaa na huduma

Uganda-Ke

Chanzo cha picha, Google

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Biashara na uhusiano wa kibiashara baina ya Kenya na Tanzania au Kenya na Uganda umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Haishangazi kuona mwaka jana marais wa nchi za Tanzania na Kenya, Samia Suluhu Hassan na mwenzake William Ruto kukubaliana kuzidi kuondoa vikwazo vya kibiashara ili kuongeza uhuru wa kibiashara na uhuru wa wafanyabiashara wa nchi hizi mbili.

Na nyuma kidogo maagizo ya rais aliyepita wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais Samia yalisaidia kushughulikiwa kwa vikwazo 56 vya kibiashara na kuchangia ukuaji wa biashara baina ya mataifa haya kwa asilimia 38% kufikia dola milioni 765 kwa mwaka 2021 pekee.

'Kati ya Januari na Novemba 2021, biashara baina ya nchi hizi imekuwa hadi kufikia trilioni 2.1 za Tanzania kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Kenya, hiyo inakuonyesha linalotokea Kenya leo linaweza kuiathiri moja kwa moja Tanzania kwenye eneo la biashara, upatikanaji wa huduma na bidhaa', anasema Beatrice Kimaro, mchumi toka Tanzania.

Katika kipindi hicho mauzo ya Tanzania kwenda Kenya yalikuwa makubwa zaidi kuliko Kenya karibu trilioni 1.16 ikilinganishwa na bilioni 938 kwa bidhaa na huduma za Kenya zilizouzwa Tanzania.

'Takwimu hizi zinakuonyesha namna Tanzania inavyoweza kuathirika zaidi na maandamano ya Kenya, kwa sababu shughuli za kibiashara zitakuwa zinaathiriwa na maandamano, maduka hayafunguliwi, usafiri kusimama mara kwa mara, huduma katika mamlaka muhimu za kibiashara zitakua zikiyumba, kwa hiyo biashara hazitaenda kama inavyotarajiwa', alisema Kimaro.

Tz-Ke

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa anachokisema Kimaro maana yake Tanzania haitauza inavyopaswa bidhaa zake kama vitunguu na mboga zingine za majani, unga wa ngano na sembe, mbao, tangawizi, mashudu ya pamba, vinywaji vya matunda na bidhaa zingine za viwandani kama marumaru za sakafuni na ukutani zinazohitajiwa sana Kenya.

Lakini Tanzania pia itapata msiba wa kukosa huduma na bidhaa za Kenya inazozitegemea. Kwa mujibu wa Benki kuu ya Kenya mauzo ya nje yaliongezeka hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 1.09 katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2022 kutoka dola milioni 865 katika kipindi kama hicho Mwaka 2021, kati ya mauzo hayo, dola milioni 226 yalikuwa mauzo kwenda nchini Tanzania.

Sabuni, mafuta ya kupikia, vifaa vya umeme na dawa ni baadhi ya bidhaa zinazoingizwa sana Tanzania zikitokea Kenya.

Pia maandamano yakichachamaa usafiri kama wa magari madogo na bodaboda katika maeneo haya utakuwa mtihani mkubwa. Kwakuwa yanategemeana sana. Lakini hata mabasi makubwa yanayofanya safari zao kati ya Nairobi - Dar es Salaam au Nairobi - Kampala hauwezi kuwa sawasawa. Lazima utaguswa na kuathiri watu waliokuwa wanategemea huduma hiyo.

Undugu, ujamaa na usafiri

Kenya

Eneo lingine ambalo Tanzania na Uganda zinaweza kuathirika ni hili na undugu na ujamaa wa kawaida baina ya jamii za pande hizi hasa wanaoishi mipakani.

Ukiwa kwenye mji wa mpakani mwa Uganda na Kenya wa Busia au Namanga unaounganisha Kenya na Tanzania, jamii inaishi kindugu kama jamii ya nchi moja. Asubuhi mtu anakunywa chai upande wa Kenya, baadae anakula chakula cha mchana upande wa Tanzania. Hivyo hivyo kwa Busia upande wa Kenya na Uganda.

Kuna watu wenye wachumba zao, wake na watoto upande wa pili wa nchi, kuna wanaofanya kazi upande wa pili wa nchi na kutoa huduma nyingine upande wa pili. Haya yote yanaweza kuathirika ikiwa maandamano yataongezeka na kusambaa zaidi katika maeneo mengi zaidi.

Kila mtu anakumbuka maandamano ya siku moja tu Machi mwaka 2019 katika eneo la Namanga yalivyotikisa shughuli za kijamii na hata kibiashara katika mpaka wa nchi hizo.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi maandamano hayo yalizuka kufuatia kutekwa nyara kwa mfanyabishara mmoja wa Kenya ambaye waandamanji hao wanasema alipelekwa nchini Tanzania.

'Dalili ya mvua'

Waswahili wanasema lisemwalo lipo na kama halipo laja, tayari dalili za athari ya maandamano haya zinaanza kujionyesha katika hatua za mapema. Japo si kubwa na bado takwimu hazijaeleza ukubwa wake, lakini tayari wafanyabiashara baina ya nchi hizi mbili Tanzania na Kenya na hata Uganda wameanza kuihisi.

Shirika la utangazaji la Kenya, KBC lilimnukuu kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Dokta Ekuru Aukot ambaye pia ni mwanasheria akisema "Maandamano ni kuhujumu uchumi na kutokujali. Rafiki yangu anayeendesha kampuni ya watalii amepoteza fursa ya watalii 50 kwa ajili ya kutembelea Masai Mara."

Nchini Uganda BBC imezungumza na Nabende Wamoto, anayeishi mpakani mwa Uganda na Kenya, pamoja na mambo mengine anasema wana wasiwasi wa kukosekana kwa bidhaa nchini humo huku wasiwasi mkubwa ukiwa ni biashara na huduma kuzorota.

"Hapa nilipo mjini Mbale ni barabara mpya kabisa iliyowekwa lami miaka miwili iliyopita inaungisha Uganda na Kenya kupitia mpaka mmoja unaitwa Lwakhakha. Na hapa nilikua nashuhudia magari ya mizigo 200 kwa siku lakini kwa wakati huu ni machache sana yanayotoka Uganda kuekekea Kenya', anasema Wamoto.

Lakini nini wasiwasi wa wafanyabiashara na wananchi wa Uganda? Wamoto anasema: 'Wafanyabiashara wana wasiwasi kwamba kunaweza kutokea shida kwa magari yao upande wa Kenya, wengi wanawasiwasi, wengi wanaogopa wengi hawawezi kuvuka mpaka kwenda Kenya'.

Kwa upande wa Tanzania Sospeter Shirima, mfanyabiashara wa vitunguu anasema ; ' Mimi nilikuwa niende Nairobi wiki iliyopita lakini nilihairisha kuangalia hali kwanza, inanipa hofu hasa kwa Nairobi, sijui itakuaje kama kila wiki maandamano yatakuwepo, kibiashara sio (itakuwa mbaya)'.

Mchumi Kimaro akizungumzia yanayowakuta wafanyabiashara sasa anasema bado athari za moja kwa moja hazitaonekana kwa sasa na kwa ukubwa wake ila kadri muda unavyokwenda zitaanza kujionyesha.

'Dalili ya mvua ni mawingu, kidogokidogo unaanza kuona hali hii leo, huwezi jua kwa kiwango gani watu wa nchi hizi mbili wataathirika katika siku zijazo za maandamano kama yataendelea, lazima hatua zichukuliwe kwa ukubwa kwa pande mbili za kisiasa Kenya kuzungumza, hakuna haja ya kutunishiana misuli', alisema Kimaro.

Afrika Mashariki haipaswi kukaa kimya kwa msiba wa jirani

Kenya

Chanzo cha picha, Government of Uganda

Mkuu wa tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki tayari amejitokeza na kutaka wadau kushiriki kumaliza mzozo uliokuwepo na unaoendelea Kenya. Wataalam akiwemo Kimaro wanasisitiza wanasiasa wa Kenya kukaa meza moja na kuzungumza.

Kwa vyovyote vile nchi za Afrika Mashariki hazipaswi kunyamaza kuiona Kenya ikiielekea kwenye kile kilichoikumba mwaka 2007. Zaidi ya watu 1000 walipoteza maisha katika ghasia za uchaguzi za mwaka 2007, ambapo maelfu ya watu waliandamana kupinga matokeo ya uchaguzi uliomuweka madarakani Mwai Kibaki.

Hata maandamano ya sasa pamoja na mambo mengine yanapinga masuala ya uchaguzi ya mwaka Agosti 2022 yaliyompa ushindi William Ruto na naibu wake Rigath Gachagua.

Maandamano imekuwa njia kubwa anayoitumia Raila Odinga kila mara karibu katika chaguzi zote nne kati ya tano za urais alizowahi kushiriki, na kwakuwa ni mwanasiasa mwenye nguvu na wafuasi wengi, athari za maandamano yake zinajionyesha kwa ukubwa wake kuanzia kusimamisha shughuli, biashara mpaka uchumi achilia mbali uharibifu wa mali, majeruhi na vifo vya watu.

odinga
Maelezo ya picha, Bwana Raila Odinga

Wasiwasi unatawala zaidi hasa kwa kuwa hayaonekani maandamano haya kama yatakoma. Na kwa uzoefu wa huko nyuma huenda yakawa na athari kila wakati yatakapofanyika.

Siku chache zilizopita Rais Ruto alisema: ' Inatosha sasa huwezi (Odinga) kuendelea kuihujumu nchi, sina tatizo na yeye kuitisha maandamano ila atawajibika kuhakikisha maisha ya wakenya hayaghasiwi, mali zao haziharibiwi, biashara zao haziathiriwi, wataweza kwenda kazini, endelea na maandamano yako'.

Lakini kabla alisikika akiwaambia viongozi wa dini nchini humo 'Mimi nataka niwaambie maaskofu haya mambo ya maandamano nyinyi mtaomba Mungu sisi tutapambana na hawa'.

Pamoja na kauli hizi za Ruto na zile za naibu wake Gachagua kuhusu Odinga na maandamano yake, hatujamsikia Uhuru Kenyatta akijitokeza lakini Odinga mwenyewe amesikika mara kadha akisema hatwishi na kauli zao ' hawajui pale tumetoka, hata baba yao Nyayo alikuwa hawezi kunitisha mimi'.

Uhuru Ruto

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Kenya Kenyatta (kushoto) akisalimiana na Naibu rais wa sasa wa Kenya, Gachagua. Katikati ni Rais Ruto, ilikuwa siku ya kukabidhiana madaraka.

Kauli zinazokinzana hivi za wanasiasa hawa zinaamsha ari ya upinzani zaidi kati ya wafuasi wanaomuunga mkono Raila na wale wanaoiyunga mkono serikali ya Ruto.

Pamoja na hayo hatujasikia kauli yoyote kusaidia kuweka mambo sawa Kenya kutoka nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, ambapo Uganda na Tanzania ni wanachama muhimu.

Kwa vyovyote vile si Tanzania, Uganda wala nchi zingine za Afrika Mashariki zinapaswa kunyamaza kimya. Kama jirani ndugu, zinapaswa hata kukaa sebuleni na wanasiasa wa Kenya kuweka mambo sawa.

Zisiingie kabisa chumbani, kwa kuwa huko ni masuala ya ndani ya nchi yasiyopaswa kuingiliwa, lakini ghasia na kusimamisha shughuli muhimu za biashara na uchumi zinagusa maslahi yao pia. Hii ni sawa na kuleta matanga ya msiba Tanzania na Uganda kwa msiba uliotokea Kenya.