Mambo 5 unayofaa kujua kuhusu mpango wa Kenya kukodisha uwanja wa JKIA kwa kampuni ya Adani Group

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mamia ya abiria walikwama kwa muda mrefu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi, mojawapo ya vitovu vya usafiri vilivyo na shughuli nyingi zaidi barani Afrika siku ya Jumatano.
Wafanyakazi waligoma kutokana na mipango ya serikali ya kukodisha uwanja huo kwa kundi la Adani la India. Lakini kwa nini wana hasira sana kuhusu dili la uwanja wa ndege?
Haya hapa mambo matano muhimu unayohitaji kujua.
1. Adani Group ni akina nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Adani Group ni mojawapo ya kampuni kubwa zaidi ya India, inayoongozwa na bilionea Gautam Adani-mtu wa pili kwa utajiri India.
Kampuni hiyo inafanya kazi katika sekta nyingi za nishati, miundombinu na usafiri, wakiwa na uwekezaji mkubwa duniani kote, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, bandari na mitambo ya kuzalisha umeme.
Kampuni hiyo imeongeza uwekezaji wake Afrika na tayari ina mkataba wa uendeshaji wa bandari nchini Tanzania .Imesema lengo lake kuwekeza katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya ni kuboresha uwanja huo na kuzidisha ushindani wake katika kanda ya Afrika Mashariki .
2.Kwa nini mpango huu umezua utata?

Mwaka jana, mtandao wa kimataifa wa waandishi wa habari wa uchunguzi ulishutumu Adani Group kwa kununua hisa zake kupitia makampuni ya nje ya nchi ili kuongeza bei ya hisa zake.
Kundi hilo lilikana madai hayo. Mikataba ya Adani ya ng'ambo mara nyingi imekuwa ikikosolewa.
Wanaharakati nchini Bangladesh wanasema nishati inayotolewa na Adani kupitia mkataba mkuu wa umeme ni ghali sana, ikiiacha Bangladesh na pengo la $500m katika ulipaji wa deni lake
Makunzi ya upinzani na wanaharakati wanaoipinga kampuni hiyo wamedai kwamba Adani Group imekuwa ikitumia ushirikiano wake wa karibu na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kupata kandarasi kubwa nchini humo .
3. Tunajua nini kuhusu mpango huo?

Chanzo cha picha, State House Kenya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Serikali ya Kenya imependekeza kukodisha uwanja mkuu wa ndege wa Nairobi kwa Adani Group kwa miaka 30 ili kubadilishana na uwekezaji wa $ 1.85 bilioni. Hii itatumika kujenga njia ya pili ya ndege mpya, kati ya mambo mengine.
Serikali inasema uwanja wa ndege unafanya kazi zaidi ya uwezo na unahitaji uwekezaji wa kibinafsi ili kuuboresha.
Rais William Ruto amewahi kuzungumzia umuhimu wa kuboresha uwanja huo akisema;
'Uwanja wa ndege tulionao Nairobi umetengenezwa kwa matandarua. Huu ni muundo wa muda ambao tuliuweka, sijui, karibu miaka saba iliyopita. Na ndio sababu tunahitaji kufanya kazi na wawekezaji kutupatia uwanja mpya wa ndege jijini Nairobi'
Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura Jumatano alitoa taarifa kujaribu kuweka wazi mpango huo akisisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba mpango mzima huo wa kukodisha uwanja wa JKIA ulilenga kuboresha uwanja wa ndege na kuunda nafasi za ajira kwa Wakenya .Katika taarifa yake aliweka muhtasari wa manufaa wanayofaa kutarajia Wakenya katika mpango huo ,huku akibainisha kwamba hakuna makubaliano yaliyotiwa saini

Chanzo cha picha, Ofisi ya Msemaji wa Serikali Kenya
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Lakini Muungano wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga nchini Kenya umesema mpango huo utasababisha Wakenya kupoteza kazi huku Adani akileta wafanyakazi wasio Wakenya.
4. Kwanini mpango huo sio wa kawaida?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni kawaida kwa viwanja vya ndege duniani kote kusimamiwa na makampuni ya kigeni. Kwa mfano, Uwanja wa Ndege wa Heathrow wa London unamilikiwa na kundi la wawekezaji wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na wawekezaji kutoka Uhispania na Qatar.
Lakini suala kuu hapa ni masharti ya makubaliano, na kama maslahi ya Wakenya yatalindwa.
Loyford Nkonge Mwekahazina wa muungano wa wafanyakazi wa usafiri wa angani , anasema;
'Sababu ya kwanini wafanyikazi wameamua kugoma ni kwa sababu Kuna uwezekano kwamba watapoteza kazi zao, au ikiwa hawatapoteza kazi zao, kuna uwezekano kwamba watajadili upya masharti ya utendakazi ambayo yatakuwa ya kuwandamiza'
5. Je, mpango huo utaidhinishwa?
Mkataba uliopendekezwa ulisitishwa kwa muda na Mahakama ya Kuu siku ya Jumanne, baada ya Chama cha Wanasheria nchini Kenya na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya kudai kuwa haukuwa wa lazima na utaleta thamani duni kwa walipa kodi.
Sasa wana kibali cha kuomba mapitio ya kisheria ya mipango hiyo. Serikali imesema iwapo utaidhinishwa, kutakuwa na ulinzi au kinga zitakazowekwa ili kulinda maslahi ya nchi.
Imehaririwa na Seif Abdalla












