Hakuna kisingizio cha ghasia za kikoloni nchini Kenya, Mfalme asema

Chanzo cha picha, EPA
Mfalme Charles amekiri "vitendo vya kuchukiza na visivyofaa vya unyanyasaji vilivyofanywa dhidi ya Wakenya" wakati wa harakati zao za kupigania uhuru.
Katika ziara yake ya kitaifa nchini Kenya, Mfalme alizungumzia "makosa" ya enzi ya ukoloni wa Uingereza.
Katika hotuba yake kwenye dhifa ya jioni iliyoandaliwa na serikali jijini Nairobi alielezea kuhusu "masikitiko na majuto yake makubwa" akisema "hakuna kisingizio".
Lakini Mfalme hakutoa msamaha rasmi - ambao ungepaswa kuamuliwa na mawaziri wa serikali.
Kujibu, Rais wa Kenya William Ruto alisifu ujasiri wa Mfalme kwa kuangazia "suala hilo licha ya ugumu wake''.
Rais wa Kenya alimwambia Mfalme kwamba utawala wa kikoloni ulikuwa wa "kikatili kwa watu wa Afrika" na kwamba "mengi bado yanafaa kufanywa ili kupata fidia kamili".
Kabla ya ziara ya kitaifa ya Mfalme nchini Kenya, ya kwanza katika nchi ya Jumuiya ya Madola tangu kuanza kwa utawala wake, kumekuwa na uvumi kwamba Ufalme utaomba msamaha.
Ingawa Mfalme hakuomba msamaha, hotuba yake katika Ikulu ya Kenya ilikuwa ni utambuzi muhimu na wenye maneno makali dhidi ya makosa yaliyofanywa wakati wa ukoloni.
Wakati Kenya inaadhimisha miaka 60 ya uhuru, Mfalme aliwaambia wasikilizaji wake: "Ni muhimu sana kwangu kwamba ninafaa kuongeza uelewa wangu wa makosa haya, na kwamba nikutane na baadhi ya wale ambao maisha na jamii zao ziliathiriwa pakubwa."

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchini Kenya kuna kumbukumbu za kukandamizwa kwa uasi wa Mau Mau, ambapo maelfu waliuawa na kuteswa miaka ya 1950 kabla ya uhuru.
Muongo mmoja uliopita serikali ya Uingereza ilielezea "majuto yake kwamba ukiukwaji huu ulifanyika" na kutangaza malipo ya karibu pauni milioni 20 kwa zaidi ya watu 5,000, katika kile ilichokiita "mchakato wa upatanisho".
Wafalme wanapaswa kuzungumza juu ya ushauri wa mawaziri na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak tayari amekataa wito wa kuomba msamaha kuhusu suala tofauti la utumwa.
Hatua ya kukosa kuomba msamaha katika safari hii huenda imewakatisha tamaa baadhi ya Wakenya kama David Ngasura wa ukoo wa Talai wa Kenya.
Ameandika barua kwa Familia ya Kifalme kuomba msamaha na fidia - na kwa kujibu Kasri la Buckingham ilielekeza ombi lake kwa Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo.
Iwapo kuna wasiwasi kuomba msamaha itafasiriwa kama kukubali dhima na kusababisha madai ya kisheria, Wakenya walionusurika na unyanyasaji wa utawala ya kikoloni wanahoji kuwa ingesaidia kuleta uponyaji na kufungwa.
Mfalme Charles, ambaye alikariri kuwa "nyakati zenye uchungu zaidi za uhusiano wetu mrefu na mgumu", aliambia wasikilizaji wake kwamba urafiki kati ya Uingereza na Kenya unaweza kuimarishwa kwa "kushughulikia historia yetu kwa uaminifu na uwazi".

Chanzo cha picha, Getty Images
Kauli yake yalikwenda mbali zaidi kuliko hotuba ya Rwanda mwaka jana ambapo alizungumzia "kwa undani huzuni yake binafsi" kutokana na mateso yanayosababishwa na biashara ya utumwa.
Sehemu ya hotuba ya Mfalme nchini Kenya ilitolewa kwa lugha ya Kiswahili, alipokuwa akionyesha uhusiano kati ya nchi hizo na kukumbuka mapenzi aliyokuwa nayo marehemu mama yake kwa watu wa Kenya.
Katika siku hiyo ya ziara ya kiserikali, Mfalme Charles alifanya mkutano na Rais Ruto, alitembelea shamba la mjini na kukutana na wajasiriamali vijana wa teknolojia wa Kenya.
Mfalme pia alitembelea jumba la makumbusho linalohusu historia ya Kenya na vita vyake vya uhuru.
Familia ya kifalme, haswa katika ziara za nchi za Jumuiya ya Madola, imezidi kukabiliwa na maswali juu ya urithi wa ukoloni na utumwa, na wito wa kuomba msamaha na fidia.

Chanzo cha picha, Reuters

Chanzo cha picha, PA Media

Chanzo cha picha, Reuters
Mapema mwaka huu, Buckingham Palace ilisema utafiti ulifanywa kuchunguza uhusiano wa Ufalme na biashara ya watumwa.
Lakini utafiti uliochapishwa hivi karibuni umefichua taswira tata katika mitazamo ya kifalme kuelekea utumwa, huku familia ya kifalme ya miaka ya 1800 ikigawanyika juu ya kukomesha utumwa.
Baadaye William IV alikuwa mtetezi wa utumwa, wakati binamu yake Mtawala wa Gloucester alikuwa kiongozi mkuu wa kampeni ya kukomesha utumwa.
Katika siku chache zijazo, ziara ya kitaifa nchini Kenya itazingatia njia ambazo Uingereza na Kenya zinafanya kazi pamoja katika nyanja mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na fursa za ajira kwa vijana.
Pia kutakuwa na mkutano na viongozi wa kidini ambao watazungumzia kuhusu uhusiano kati ya jumuiya.












