Rigathi Gachagua: Maseneta nchini Kenya wamuondoa ofisini Naibu Rais

Chanzo cha picha, Getty Images
Maseneta wa Kenya wamepiga kura ya kumuondoa Naibu Rais Rigathi Gachagua ofisini licha ya kushindwa kutoa ushahidi wake katika kesi ya kumuondoa madarakani baada ya wakili wake kusema kuwa amepelekwa hospitalini.
Katika moja ya siku za kushangaza katika historia ya hivi majuzi ya kisiasa nchini Kenya, Gachagua alipaswa kufika katika Seneti baada ya chakula cha mchana kujitetea, siku moja baada ya kukanusha mashtaka 11.
Hata hivyo, Gachagua, almaarufu Riggy G, hakufika na wakili wake akaomba kuahirishwa akisema mteja wake alikuwa akisumbuliwa na 'maumivu ya kifua' na alikuwa akitibiwa na madaktari katika Hospitali ya The Karen.
Hata hivyo baada ya muda wa saa mbili kutoka saa tisa mchana hadi saa kumi na moja jioni Gachagua hakuweza kufika bungeni .
Maseneta waliamua kuendelea na kesi bila yeye kuwepo, na hivyo kusababisha timu ya mawakili wake kuondoka katika chumba hicho.
Kukataa kwa maseneta kuchelewesha kesi hadi Jumamosi - kwa muda mrefu kama ingeruhusiwa kisheria - kunaonyesha jinsi walivyodhamiria kumuondoa Gachagua, miezi kadhaa baada ya kutofautiana na Rais William Ruto.
Wiki iliyopita, idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa - baraza la chini la bunge - walipiga kura ya kumshtaki, na kuweka msingi wa kesi yake ya siku mbili katika Seneti.
Gachgua, mfanyabiashara tajiri kutoka eneo la katikati mwa Kenya la Mlima Kenya lenye wingi wa kura ambaye alikuwepo katika bunge la seneti asubuhi, ameelezea kufunguliwa mashtaka hayo kama "unyanyasaji wa kisiasa".
Kura juu ya mashtaka 11 dhidi ya Gachagua
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa shtaka la kwanza la ukiukaji wa Jumla wa Vifungu 10 (2) (a), (b) na (c); 27 (4), 73 (1) (a) na (2) (b); 75 (1) (c), na 129 (2) ya Katiba na Ibara za 147 (1), kama zilivyosomwa na Ibara ya 131 (2) (c) na (d) ya Katiba, maseneta 53 walipiga kura ya NDIYO kumshtaki huku 13 wakipiga kura ya HAPANA.
Katika shtaka la pili la Ukiukaji Mkubwa wa Ibara za 147 (1) na 152 (1) za Katiba, 28 walipiga kura ya NDIYO huku 39 wakipiga kura ya HAPANA. Katika shtaka la tatu la Ukiukaji Mkubwa wa Ibara ya 6 (2), 10 (2) (a), 174, 186 (1), 189 (1) na Jedwali la Nne la Katiba, 19 walipiga kura za NDIYO na 46 walipiga kura ya HAPANA.
Katika shtaka la nne la Ukiukaji Mkubwa wa 160 (1) yaKatiba na Ibara za 147 (1), kama zilivyosomwa na Ibara ya 131 (2) (c) na (d) ya Katiba, wabunge 53 walipiga kura ya NDIYO kumshtaki huku 13 wakipiga kura ya HAPANA.
Shtaka la 5: Ukiukaji Mkubwa wa Ibara ya 3 (1) na 148 (5) (a) ya Katiba, na, katika shtaka la nne la Ukiukaji Mkuu wa 160 (1) wa Katiba, 49 walipiga kura ya NDIYO na 16 HAPANA huku 2 wakikataa kupiga kura. .
Shtaka la 6: Sababu kuu za kuamini kuwa Mheshimiwa Rigathi Gachagua ametenda uhalifu chini ya vifungu vya 13 (1) (a) na 62 vya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, na, katika shtaka la nne la Ukiukaji Mkuu wa 160 (1) Katiba, 47 walipiga kura ya NDIYO na 18 HAPANA na 1 hawakupiga kura.
Shtaka la 8: Sababu kubwa za kuamini kwamba amefanya uhalifu chini ya kifungu cha 132 cha Kanuni ya Adhabu na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uongozi na Uadilifu, 27 walipiga kura ya NDIYO na 40 HAPANA.
Shtaka la 9, Utovu mkubwa wa nidhamu ambao hauambatani na wito wa juu na hadhi ya heshima ya Ofisi ya Naibu Rais na mjumbe wa Baraza la Mawaziri na Baraza la Usalama la Kitaifa. H. E. Naibu Rais ameshambulia hadharani na kuhujumu kazi ya Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi na Maafisa wake), 46 walipiga kura ya NDIYO na 20 wamepiga kura ya HAPANA, huku 1 akikosa kupiga kura.
Shtaka la 10. Utovu mkubwa wa nidhamu (kutotii) 23 walipiga kura ya NDIYO na 44 walipiga HAPANA.
Shtaka la 11. Utovu mkubwa wa nidhamu (uonevu 17 walipiga kura ya NDIYO na 41 walipiga HAPANA huku 2 wakikosa kupiga kura.
Mnamo Alhamisi jioni, theluthi mbili ya maseneta 67 waliohitajika walipiga kura ya kumtimua madarakani kwa tuhuma zinazojumuisha ufisadi, kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuihujumu serikali.
Maseneta walipiga kura kwa wingi kumtia hatiani katika kura ya kwanza - kiasi cha kutosha kwake kuondolewa afisini.
Haya yanajiri miaka miwili tu baada ya Ruto na Gachgua kuchaguliwa kwa tiketi ya pamoja.
Kura hiyo inafikisha tamati ya mzozo wa miezi kadhaa katika ngazi ya juu ya serikali na kumpa fursa Ruto kujikita mamlakani.
Mzozo huo uliibuka mwezi Juni ambapo Gachagua, kwa kitendo kinachoonekana kumhujumu rais, alimlaumu mkuu wa shirika la ujasusi kwa kutomfahamisha Ruto na serikali ipasavyo kuhusu ukubwa wa maandamano ya kupinga nyongeza ya ushuru ambayo haikupendwa na watu wengi.
Katika pigo kubwa kwa mamlaka yake, Ruto alikuwa amelazimika kuondoa mapendekezo hayo ya ushuru. Alifuta baraza lake la mawaziri na kuleta wanachama wa upinzani kwenye serikali yake.
Ruto hajazungumzia tuhuma dhidi ya naibu wake.
Mwanzoni mwa kesi hiyo, mmoja wa mawakili wa Gachagua, Elisha Ongoya, alisema madai yote ni "ya uwongo, kejeli au aibu" .
Kabla ya kura hiyo, Gachagua alikuwa amesema angepinga uamuzi huo iwapo utapitishwa.
Daktari mmoja amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema Gachagua mwenye umri wa miaka 59 alienda hospitalini akiwa na tatizo la moyo, lakini alikuwa ametulia na anafanyiwa vipimo.
Vyombo vya habari vya Kenya tayari vimekuwa vikiripoti kuhusu uwezekano wa kubadilishwa kwake, huku watu wanne wakitajwa kama wanaowezwa kuteuliwa kuchukua wadhifa huo:
Gavana wa Kaunti ya Murang'a Irungu Kang'ata
Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki
Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Nini kitakachofuata?
Huku Seneti ikithibitisha kuondolewa kwake ofisini , vita vya Gachagua vitaelekea katika mahakama ambazo zinaweza kumrejesha madarakani - ikiwa ataweka sababu za kutosha - hadi uamuzi wa ombi hilo uamuliwe.
Gachagua ambaye amekuwa mashakani kwa muda sasa ameeleza mara kwa mara imani yake kwa idara ya Mahakama akiashiria kuwa yuko tayari kupigana hadi Mahakama ya Juu, vita vya muda mrefu vya kisheria ambavyo vinaweza hata kumalizika hadi mwisho wa kesi yake .















