Rigathi Gachagua: Kiongozi muwazi na jasiri aliyeondolewa madarakani

Rigathi Gachagua

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Basillioh Rukanga
    • Nafasi, BBC News, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua hatimaye ameondolewa madarakani baada ya seneti kupiga kura kufuatia hoja ya madai 11 dhidi yake yaliopitishwa na bunge .

Kiogozi huyo aliondolewa madarakani akiwa hospitalini baada ya kuugua muda mchache tu kabla ya kutakiwa kufika katika bunge la seneti ili kutoa ushahidi.

lakini Rigathi Gachagua ni nani haswa?

Naibu Rais wa Kenya, anayepigwa vita, Rigathi Gachagua, anajiita “msema kweli”, akijigamba kwamba amekuwa maarufu kutokana na kusema ukweli kuhusu uongozi.

Lakini anapokabiliwa na kesi ya mashtaka/shutuma, anasema shida hizi pia ni matokeo ya tabia yake ya kusema.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka wa 2017, haikujulikana kidogo kuhusu mwanaume ambaye, katika miaka mitano mifupi, angesimama na kuwa wa pili kwa kamanda wa Kenya.

Sio watu wengi nje ya eneo bunge la Gachagua katikati mwa Kenya walikuwa wamesikia kumhusu au mtindo wake wa siasa.

Gachagua aliibuka kidedea katika maandalizi ya uchaguzi wa 2022, alipopinga vikali chaguo la Rais Uhuru Kenyatta la mrithi anayempendelea.

Kenyatta alikuwa akimpigia debe Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Lakini Gachagua alishirikiana na William Ruto, aliyekuwa naibu wa Kenyatta wakati huo, ambaye alikuwa akigombea urais ambao mkuu wake hakutaka kumuachia urithi.

Katika mikutano ya kisiasa na duru za vyombo vya habari, Gachagua alimkashifu Kenyatta, mara kwa mara kwa maneno ambayo wanasiasa wengine hawakupendezwa nayo.

"Usiniue jinsi baba yako alivyomuua JM Kariuki," alisema katika mkutano wa Julai 2022, akimzungumzia mbunge aliyeuawa mwaka wa 1975 wakati wa utawala wa Jomo Kenyatta, rais wa kwanza wa taifa na baba yake Uhuru Kenyatta. .

Hadi leo, hakuna aliyepatikana na hatia ya kifo cha Kariuki.

Kabla ya kuwa naibu rais wa Kenya, polisi walivamia nyumba ya Gachagua na kumkamata kuhusiana na kesi ya ufisadi na utakatishaji fedha.

Mashtaka hayo yaliondolewa baada ya yeye na Ruto kuchukua mamlaka kufuatia uchaguzi wa 2022.

Alikuwa amemsaidia Ruto kushinda kwa kuungwa mkono katika Mlima Kenya - eneo kubwa zaidi la wapiga kura nchini. Gachagua na Kenyatta wanatoka huko. Kenyatta alikuwa amejaribu kuwakusanya wapiga kura wa Mlima Kenya ili kumuunga mkono Odinga, lakini alishindwa.

Rigathi Gachagua

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Muda mrefu kabla ya Kenyatta kuwa rais 2013, Gachagua alikuwa amefanya kazi naye kwa karibu, ikiwa ni pamoja na kama msaidizi wake wa binafsi kwa miaka mitano.

Lakini baada ya kuungana na Ruto, Gachagua alitoka kuwa “msiri” wa Kenyatta hadi mmoja wa wakosoaji wake wakali.

Hata hivyo, tangu kukosana na mkuu wake wa sasa, Gachagua ameomba msamaha kwa Kenyatta, akisema ilikuwa "upumbavu" kwake "kupigana na ndugu yangu mwenyewe".

Unyenyekevu huu ni tofauti kabisa na matamshi yake kwani mgombea mwenza wa Ruto, mchanganuzi Javas Bigamo alikuwa hata amemtaja Gachagua kama "mbwa wa kisiasa anayeogopwa ambaye Ruto alihitaji kuweza kukabiliana na Rais Kenyatta katika eneo la kati".

Gachagua alisifiwa kama mhamasishaji bora, ambaye alikuwa akiwasikiliza watu wa kawaida mashinani.

Hata hivyo pengine hakuwa mtu ambaye wengi walitarajia kuchukua wadhifa huo wa naibu, ikizingatiwa kwamba Gachagua alikuwa tu mwanasiasa kwa miaka mitano na alikuwa akipambana na wagombea wengi wenye uzoefu.

Ruto alieleza kuwa amemchagua Gachagua kwa sababu "ni mmoja wa viongozi wanaopenda watu wa kawaida".

Mtaalamu wa siasa Bobby Mkangi hapo awali aliiambia BBC kwamba uwezo wa Gachagua kujadili njia yake ya kufika kileleni "akizingatia majina mengine ambayo yanatajwa na kujulikana kitaifa" ni "kitu kikubwa".

Lakini miaka miwili tu baada ya kuingia madarakani, uwezo huo unaonekana kulegalega na kumwacha Gachagua akipambana na rais na katika nafasi ambayo wabunge wengi wanashinikiza kuondolewa kwake.

Anatuhumiwa kwa ufisadi, utakatishaji fedha, utovu wa nidhamu, ukaidi na uonevu wa maafisa wa umma.

Huku hoja hiyo ikiwasilishwa bungeni Jumanne, mbunge anayewasilisha hoja hiyo Mwengi Mutuse alisema kuwa wabunge 291 kati ya 349 walitia saini waraka huo wakishinikiza kuondolewa kwa Gachagua.

Gachagua

Chanzo cha picha, Getty Images

Gachagua amekuwa akishutumiwa kila mara kwa kuwa jeuri na mkali, ilikuwa mojawapo ya sababu ambazo baadhi ya watu walibishana dhidi ya kuchaguliwa kwake kuwa mgombea mwenza kabla ya uchaguzi wa 2022. Lakini katika miezi ya hivi karibuni, ukosoaji huu umeongezeka.

Anakanusha tathmini hii ya tabia yake, pamoja na madai kwamba anawatenganisha wanasiasa wenzake.

Anasema anachofanya ni “kusema ukweli”, jambo ambalo anasisitiza kuwa limemfanya asiwe maarufu ndani ya mirengo fulani ya kisiasa.

"Sitahatarisha kanuni zangu," alisema mwishoni mwa wiki huku wito wa kushtakiwa kwake ukifikia kikomo.

Mara nyingi Gachagua amejitambulisha kama mtoto wa wapigania uhuru wa Mau Mau, ambao walipigana na utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Alizaliwa mwaka wa 1965 na wazazi ambao amesema walikuwa wanajulikana sana kwa ushiriki wao katika kupigania uhuru. Baba yake alitengeneza na kuhudumia bunduki na mama yake alikuwa msafirishaji wa risasi na chakula cha wapiganaji hao, Gachagua alisema.

Ukoo wake umemchora kama bingwa wa watu katikati mwa Kenya, ambao wengi wao ni vizazi vya wapigania uhuru, lakini bado wanaendelea kupigania uhuru wa kiuchumi.

Kauli maarufu inayohusishwa na naibu rais ni "usiguse mlima", rejeleo la kituo chake cha usaidizi katika eneo la Mlima Kenya. Hata hivyo, pia ameshutumiwa kwa kuendeleza ukabila badala ya kuwa mtu wa kuunganisha.

Lakini Gachagua amejitetea na kusisitiza kuwa kuzungumzia eneo la kati mwa Kenya si sawa na kuhatarisha jamii nyingine.

Kabla ya kujiunga na siasa, Gachagua alikuwa na kazi kubwa.

Baada ya kumaliza chuo kikuu, alianza kufanya kazi kama msimamizi wa umma serikalini, na kama afisa wa wilaya katika maeneo tofauti nchini kote.

Wasimamizi wa wilaya wa wakati huo, wakati wa urais wa Daniel arap Moi, walijulikana kwa ustaarabu wao wa hali ya juu. Ni tuhuma ambayo amekuwa nayo, ikiwa ni pamoja na katika mazingira ya sasa.

Alifanya kazi kama msaidizi wa binafsi wa Kenyatta kati ya 2001 na 2006, wakati ambapo Kenyatta alikuwa waziri, mgombea urais na baadaye kiongozi wa upinzani.

Gachagua ni mwanasiasa tajiri, ambaye amejijengea utajiri katika biashara kwa miaka mingi. Ameoa mchungaji, Dorcas, na watoto wawili.

Mnamo 2017, aliwania kiti cha eneo bunge la Mathira, na kushinda nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na kaka yake mkubwa, Nderitu Gachagua.

Ni wakati huu ambapo tabia ya Gachagua na uwezo wake wa kisiasa ulianza kuvutia watu.

Hata hivyo matamshi yake ya hadharani, kabla na tangu alipokuwa naibu wa rais, wakati fulani yameonekana kama makosa au maoni ya moja kwa moja ya aibu.

Alisema mwaka jana kuwa serikali ilikuwa kama kampuni yenye hisa, huku wale waliopigia kura utawala wa sasa wakistahili zaidi kuteuliwa na serikali.

Seneta Danson Mungatana wiki jana alisema maneno ya Gachagua "yametenga sehemu za Wakenya, yameunda na yanaendelea kuzidisha mivutano ya kikabila".

Gachagua amejitetea mara kwa mara, lakini hivi karibuni alikiri kwamba mwishowe, huenda likawa ni jambo lile lile lililomfikisha kileleni litakalosababisha anguko lake.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdalla