'Hali ni mbaya' Kaskazini mwa Gaza,UN yasema huku ikitoa msaada kwa mara ya kwanza katika wiki mbili

Takriban Wapalestina 400,000 wamesalia kaskazini mwa Gaza, kulingana na Umoja wa Mataifa, na katika siku za hivi karibuni, imeshutumu "idadi kubwa ya majeruhi ambao ni raia".

Muhtasari

  • Ukraine yakanusha kusambaza ndege zisizo na rubani kwa waasi wa Mali
  • Israel itajibu Iran kwa kuzingatia maslahi ya taifa - Waziri Mkuu
  • Emir wa Qatar aishutumu Israel kwa kuzidisha 'uchokozi'
  • Libya yaikosoa Nigeria kwa kususia mechi ya kufuzu Afcon
  • Seneti kuendelea na hoja ya kumuondoa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua - Mahakama
  • Nilikuwa na mipango ya kuwawekea vikwazo mawaziri wa Israel - Cameron
  • UN yasema haitawaondoa walinda amani kutoka Lebanon
  • Mahakama kuamua leo iwapo Seneti itaendelea na hoja ya kumuondoa mamlakani Naibu Rais Kenya
  • Bei ya mafuta ya Petroli yashuka Kenya
  • Katibu Mkuu wa NATO: 'Muungano utafanya kila kitu kumzuia Putin kufikia malengo yake nchini Ukraine'
  • Vita nchini Ukraine: Zelensky aliahidi kuwasilisha "mpango wake wa ushindi" wiki hii
  • Mendy asema alikopeshwa pesa na wachezaji wenzake wa zamani wa Manchester City
  • Sean 'Diddy' Combs atuhumiwa kumnyanyasa kingono mvulana katika kesi mpya
  • Lebanon yasema watu 21 wameuawa katika shambulio la anga kaskazini mwa nchi hiyo

Moja kwa moja

Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Ukraine yakanusha kusambaza ndege zisizo na rubani kwa waasi wa Mali

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Ukraine imekanusha madai kwamba ilitoa ndege zisizo na rubani kwa waasi wanaopigana dhidi ya jeshi la Mali na mamluki wanaoungwa mkono na Urusi.

    Madai hayo yanatokea baada ya gazeti la Le Monde lenye makao yake mjini Paris kuripoti kwamba ndege zisizo na rubani za Ukraine zilikuwa zikitoa msaada kwa waasi wa Tuareg "ambao wananufaika na uungwaji mkono kutoka Kyiv".

    Serikali ya Mali inayoongozwa na jeshi ilihitimisha muungano wa muda mrefu na mkoloni wa zamani Ufaransa mwaka 2022 kwa ajili ya Urusi katika jitihada za kukabiliana na uasi uliodumu kwa miaka mingi kaskazini mwa nchi hiyo.

    Lakini imeshindwa kuzima machafuko na hivi karibuni ilipata hasara kubwa, pamoja na washirika wake wa Urusi.

    Soma zaidi:

  3. Israel itajibu Iran kwa kuzingatia maslahi ya taifa - Waziri Mkuu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Israel ataisikiliza Marekani lakini atafanya maamuzi ya mwisho kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa, ofisi ya waziri mkuu wa Israel ilisema, huku uvumi kuhusu jibu lake kwa shambulio kubwa la kombora la Iran ukiendelea.

    Taarifa hiyo fupi ilitolewa kujibu taarifa ya Washington Post ambayo ilisema Benjamin Netanyahu aliiambia Marekani kuwa yuko tayari kulenga maeneo ya kijeshi nchini Iran - badala ya vituo vya nyuklia au mafuta.

    Likiwanukuu maofisa wawili, gazeti la Post lilisema Netanyahu alitoa maoni hayo wakati wa mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden Jumatano iliyopita, walipojadili kuhusu kulipiza kisasi kwa Israel.

    Iran ilirusha takriban makombora 200 ya balistiki kuelekea Israel tarehe 1 Oktoba. Mengi ya makombora hayo yalinaswa, jeshi la Israel lilisema.

    Soma zaidi:

  4. Emir wa Qatar aishutumu Israel kwa kuzidisha 'uchokozi'

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, ameishutumu Israel kwa kuchagua kuongeza kile anachoeleza kuwa "uchokozi" kwa "kutekeleza mipango iliyotayarishwa" katika Ukingo wa Magharibi na Lebanon.

    Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la Shura, chombo kinachotunga sheria nchini humo, Al Thani amesema sababu ya Israel kufanya hivyo ni "kuona kwamba uwezo wa mzozo kuongezeka upo".

    Anasema "njia rahisi na salama zaidi" ya kukomesha mzozo unaoongezeka kwenye mpaka wa Lebanon ingekuwa "kusitisha vita vya maangamizi huko Gaza".

    Qatar, pamoja na Misri na Marekani, imekuwa mpatanishi mkuu katika majaribio ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kutekwa nyara na Hamas na Israel huko Gaza.

  5. Libya yaikosoa Nigeria kwa kususia mechi ya kufuzu Afcon

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirikisho la Soka la Libya (LFF) limelikosoa lile laNigeria baada ya timu yake ya taifa kurejea Afrika Magharibi kabla ya mechi yao ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 mjini Benghazi.

    Kikosi cha Super Eagles kiliamua kususia mechi hiyo, iliyoratibiwa kuchezwa saa 19:00 GMT Jumanne, baada ya kukwama katika uwanja wa ndege wa Al Abraq wakati ndege yao ilipoelekezwa huko Jumapili.

    Baada ya kuhifadhiwa kwenye jengo la kituo, katika eneo la takriban kilomita 230 (maili 143) kutoka walikokusudia, wajumbe wa Nigeria walirudi nyumbani na kuwasili Kano Jumatatu alasiri.

    Hata hivyo, Libya walifanya mazoezi kabla ya mchezo huo na wanaonekana kujiandaa kujitokeza kwenye Uwanja wa Martyrs mjini Benina kutimiza kibarua hicho licha ya wapinzani wao kugomea mchujo huo.

    Taarifa kutoka kwa LFF ilisema "inalaani" hatua zilizochukuliwa na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) katika kukataa kucheza mchezo huo, na kusema itachukua "hatua zote muhimu za kisheria" kuhifadhi maslahi timu ya Knights ya Mediterranean.

    Nahodha wa Super Eagles William Troost-Ekong alitetea uamuzi wa kikosi hicho kususia mechi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

    "Kandanda ni juu ya heshima, na hiyo huanza kwa kujiheshimu," alisema kwenye chapisho kwenye X.

    "Lengo letu la kufanya vyema zaidi kwa soka la Nigeria halitabadilika kamwe. Natarajia kuendelea na safari yetu ya Afcon 2025 mwezi ujao kwa njia ifaayo."

    Bodi ya nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) inachunguza mazingira baada ya Nigeria "kukwama katika mazingira ya kutatanisha".

    Kuna uwezekano wa matokeo kadhaa, huku uwezekano wa Libya kupewa ushindi wa mabao 3-0 au Caf kuamuru mechi hiyo ichezwe baadaye.

    Rufaa kwa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo pia inawezekana, na Nigeria inatazamiwa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Caf.

    Awali LFF ililalamikia jinsi wachezaji na maafisa wao walivyotendewa walipowasili Nigeria kwa ajili ya mechi ya kufuzu mjini Uyo wiki iliyopita, ambayo ilishuhudia ndege yao ikitua kwa saa nyingi mbali na uwanja wa mechi na wachezaji kuchelewa kusafiri kwa muda mrefu.

    Soma zaidi:

  6. Habari za hivi punde, Seneti kuendelea na hoja ya kumuondoa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua - Mahakama

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama imetoa uamuzi wake na kuruhusu Bunge la Seneti nchini Kenya kuendelea na hoja ya kumuondoa madarakani Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua.

    Jaji Chacha Mwita wa Mahakama ya Juu ndiye aliyetoa uamuzi huo.

    Gachagua aliwasilisha hoja 26 mahakamani kuhusu kuendelea kwa kikao cha Seneti kinachotarajiwa kukaa Jumatano kujadili kuondolewa kwake madarakani lakini sasa kesi hiyo iliyowasilishwa na Bunge la Kitaifa itaendelea kusikilizwa.

    Naibu Rais anatazamiwa kujitetea mbele ya Seneti siku ya Jumatano na anakabiliwa na mashtaka 11 yaliyoidhinishwa na wabunge 282 katika Bunge la Kitaifa.

    Gachagua ameshikilia kuwa zoezi la kumtimua limechochewa kisiasa na kueleza kuwa na imani kwamba mahakama itatoa uamuzi wa haki.

    Mawakili wa Gachagua, Wakili Mkuu Paul Muite na wakili Tom Macharia mnamo Jumatatu walimtaka Jaji Chacha Mwita kutoa maagizo ya kukomesha mchakato wa kuondolewa madarakani kwa Gachagua.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Nilikuwa na mipango ya kuwawekea vikwazo mawaziri wa Israel - Cameron

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    David Cameron ameitaka Uingereza kuzingatia kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Israel kama njia ya "kuweka shinikizo" kwa nchi hiyo kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

    Akiongea na kipindi cha BBC cha Today programme, Cameron ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kutoka chama cha Conservative alisema kabla ya uchaguzi alikuwa "akifanyia kazi" mipango ya kuwawekea vikwazo Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir.

    Aliwataja wawili hao kuwa ni watu wenye msimamo mkali na kusema kwa kutumia vikwazo kungetuma ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba "hii sio vizuri na inabidi ikome".

    BBC imewasiliana na Smotrich na Ben-Gvir kwa majibu.

    Duru zinasema kuwa uamuzi wa Cameron ulisitishwa kwa hofu ya kuzusha mivutano ya kisiasa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

    Kulikuwa na wasiwasi kuhusu kuzusha ghasia katika maeneo bunge ambapo maoni kuhusu Mashariki ya Kati yaligawanyika.

    Pia ninaelewa kuwa Marekani ilipinga kuwawekea vikwazo Smotrich na Ben-Gvir wakati huo, na Uingereza ilionekana kutaka kuweka vikwazo pamoja na washirika wake Marekani na Ulaya ili kuongeza athari zao.

    Cameron leo alitoa wito kwa serikali mpya ya chama cha Labour kufuatilia vikwazo dhidi ya wawili hao, akiashiria matamshi waliyotoa ya kuwahimiza watu kusimamisha misafara ya misaada inayoingia Gaza na kuhimiza vurugu zinazofanywa na walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

    Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy, mrithi wa Cameron, alisema katika mkutano wa chama chake mwezi uliopita kwamba alibaini kuwa lugha inayotumiwa na wawili hao "haikubaliki kabisa".

    Na wakati akiwa upinzani, Lammy alikuwa akikosoa mara kwa mara mawaziri wote wawili.

    Ofisi ya Mambo ya Nje haijatoa maoni yoyote juu ya maamuzi ya baadaye ya vikwazo.

    Lakini baadhi ya vyanzo vinasema uamuzi wowote wa kuwawekea vikwazo mawaziri hao wawili wa Israel unaweza kucheleweshwa hadi baada ya uchaguzi wa Marekani.

  8. UN yasema haitawaondoa walinda amani kutoka Lebanon

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Umoja wa Mataifa unasema walinda amani wake kusini mwa Lebanon watasalia kwenye nyadhifa zao, licha ya matakwa ya mara kwa mara ya Israel kwamba wanapaswa kuondoka na kuachia vikosi vyake vilivyoko huko.

    Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amewaambia waandishi wa habari mjini New York kwamba uamuzi wa kuacha kikosi vya UN viendelee kusalia katika nafasi yake umeungwa mkono kikamilifu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi wanachama zinazochangia wanajeshi katika kikosi hicho.

    Siku ya Jumapili Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alionya waziwazi akiutaka Umoja wa Mataifa kuhama kutoka kambi zake kusini mwa Lebanon, ambazo alisema zinatumika kama ngao kwa wapiganaji wa Hezbollah.

    Lakini Umoja wa Mataifa umesimama kidete.

    Mkuu wa ulinzi wa amani alisema ni muhimu kwamba vikosi vyake viendelee kusalia mahali pake, kutekeleza jukumu walilopewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusaidia raia.

    Israel inahoji kuwa Umoja wa Mataifa umeshindwa kuwazuia Hezbollah kujenga mahandaki na kuweka silaha kama maroketi na makombora karibu na mpaka, kinyume na makubaliano ambayo yalimaliza vita vya mwisho huko miaka 18 iliyopita.

    Umoja wa Mataifa unasema dhamira yake ni kusaidia pande zinazohusika katika mzozo huo, na sio kutekeleza makubaliano.

    Imeishutumu Israel kwa kulenga vituo vyake kimakusudi, huku walinda amani watano wakijeruhiwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita, tuhuma ambazo Netanyahu amekanusha.

    Soma zaidi:

  9. Mahakama kuamua leo iwapo Seneti itaendelea na hoja ya kumuondoa mamlakani Naibu Rais Kenya

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Mahakama nchini Kenya itaamua leo iwapo bunge la seneti nchini humo litaendelea na hoja ya kumuondoa mamlakani Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua au la.

    Gachagua amewasilisha hoja 26 mahakamani kuendelea kwa kikao cha seneti kinachotarajiwa kukaa Jumatano kuondolewa kwake madarakani.

    Naibu Rais anatazamiwa kujitetea mbele ya Seneti siku ya Jumatano na anakabiliwa na mashtaka 11 yaliyoidhinishwa na wabunge 282 kwa Bunge la Kitaifa.

    Huku Jaji Mkuu Martha Koome akiteua jopo la majaji watatu ili kuunganisha hoja hizo na kuamua, uamuzi mwingine muhimu zaidi utatolewa Jumanne.

    Mahakama ya Juu itaamua iwapo Seneti inaweza kuendelea na kusikiliza hoja za kumuondoa mamlakani Gachagua.

    Gachagua anasisitiza kuwa mashtaka dhidi yake yamechochewa kisiasa na alionyesha imani kuwa mahakama itatoa uamuzi wa haki.

    Mawakili wa Gachagua, walisema kuwa mchakato wa Bunge wa kumtimua haukuwa wa kikatiba kutokana na kutokuwepo kwa ushirikishwaji mzuri wa wananchi.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Uganda yatia saini mkataba wa ujenzi wa reli na kampuni ya Uturuki

    g

    Chanzo cha picha, URC

    Serikali ya Uganda na kampuni ya ujenzi ya Uturuki ya Yapi Merkezi zimetia saini kandarasi ya kujenga sehemu ya reli yenye urefu wa kilomita 272 (maili 169), katika jitihada za kukuza biashara ya kikanda, afisa wa Uganda alisema Jumatatu.

    Mratibu wa mradi huo wa Reli ya Standard Gauge nchini Uganda, Perez Wamburu, amesema kandarasi hiyo ni kuhusu sehemu ya kwanza ya njia ya reli ya umeme ya kilomita 1,700 iliyopangwa, na sehemu hiyo itagharimu euro bilioni 2.7 (dola bilioni 3).

    Ujenzi wa reli hiyo utaanza mwezi Novemba, Wamburu alisema.

    Mradi huo utaongeza biashara na kupunguza gharama za usafiri, katibu mkuu wa wizara ya kazi ya Uganda, Bageya Waiswa, alisema katika hafla ya kutia saini.

    Sehemu ya reli itaanzia mji mkuu Kampala hadi Malaba kwenye mpaka na Kenya, kuiunganisha Uganda isiyo na bandari na mtandao wa reli ya jirani yake na hadi bandari ya Bahari ya Hindi ya Mombasa.

  11. Bei ya mafuta ya Petroli yashuka Kenya

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bei kuu za petroli, dizeli na mafuta taa zilipungua kwa Ksh.8.18, Ksh.3.54 na Ksh.6.93 kwa lita mtawalia katika taarifa ya ukaguzi wa hivi punde wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) iliyotangazwa Jumatatu.

    Katika bei mpya zinazoanza kutumika Oktoba 15 hadi Novemba 14, lita moja ya petroli kubwa itagharimu Ksh.180.66 jijini Nairobi huku ile ya dizeli ikiuzwa kwa Ksh.168.06.

    Wakati huo huo mafuta ya taa yatagharimu Ksh.151.39 lita katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.

    “Wastani wa gharama ya petroli iliyoagizwa kutoka nje ya ilipungua kwa asilimia 8.59 kutoka dola za Marekani 697.62 kwa kila mita ya ujazo mwezi Agosti 2024 hadi dola za Marekani 637.70 kwa kila mita ya ujazo Septemba 2024; dizeli ilipungua kwa asilimia 5.52 kutoka dola za Kimarekani 673.36 kwa kila mita ya ujazo hadi dola 636.22 kwa kila mita ya ujazo ,” Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Bargoria amesema.

    Mafuta ya taa yamepungua kwa asilimia 6.73 kutoka Dola za Kimarekani 668.34 kwa kila mita ya ujazo hadi Dola 623.39 kwa kila mita ya ujazo.

  12. Katibu Mkuu wa NATO: 'Muungano utafanya kila kitu kumzuia Putin kufikia malengo yake nchini Ukraine'

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa zamani wa Uholanzi Mark Rutte alichukua wadhifa wa Katibu Mkuu wa NATO mnamo tarehe 1 Oktoba

    NATO haiogopi vitisho kutoka kwa Urusi na itaendelea kutoa uungaji mkono mkubwa kwa Kyiv, alisema Katibu Mkuu wa Muungano Mark Rutte wakati wa ziara yake ya kwanza kwenye kambi hiyo huko Wiesbaden, Ujerumani, ambapo kituo kikuu cha uratibu wa msaada kwa Ukraine kitakuwa.

    "Ujumbe [kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin] ni kwamba tutaendelea kufanya chochote kinachohitajika ili kuhakikisha kwamba hafikii malengo yake na Ukraine inashinda," alisema katika mahojiano na Reuters na Redio ya Hesse.

    Imepangwa kuwa eneo la Wiesbaden, ambacho ni kituo cha utawala cha jimbo la shirikisho la Hesse, linaloitwa usaidizi wa usalama wa NATO na mafunzo kwa Ukraine (NSATU), litachukua hatua kwa hatua kuhusu uratibu wa usaidizi wa kijeshi wa nchi za Magharibi kwa Kyiv.

    Hatua hiyo inaonekana na wengi kama jaribio la kulinda utaratibu wa msaada dhidi ya uwezekano wa kurudi kwa Donald Trump wa Republican katika Ikulu ya White House, Reuters inabainisha.

    Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na takriban watu 700, wakiwemo wanajeshi wa Ukraine na vitengo vilivyoko katika vituo vya NATO nchini Ubelgiji, Poland na Romania.

    Kambi ya Wiesbaden pia ina jeshi la Marekani linalohusika na makombora ya masafa marefu, ambayo Washington inapanga kuyaweka kwa muda nchini Ujerumani kuanzia 2026 ili kukabiliana na tishio la makombora ya Urusi katika eneo la Kaliningrad, shirika hilo linasema.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

  13. Vita nchini Ukraine: Zelensky aahidi kuwasilisha 'mpango wake wa ushindi' wiki hii

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky amesema atawasilisha "mpango wake wa ushindi" wiki hii. Kiongozi huyo wa Ukraine pia amezungumza kuhusu mpango wake wakati wa ziara ya Marekani na Ulaya, lakini maelezo yake bado hayajatangazwa hadharani.

    "Wiki hii tutawasilisha kwa washirika wote barani Ulaya mkakati wetu wa kulazimisha Urusi kumaliza vita hivi. Bila shaka, mpango wa ushindi utawasilishwa hadharani,” Ukrayinska Pravda anamnukuu Zelensky akisema.

    Mapema Jumatatu, mshauri mkuu katika ofisi ya Rais Zelensky, Sergei Leshchenko, alisema kuwa tarehe 16 Oktoba, Zelensky atazungumzia suala hilo.

    "Ni wazi, sasa kuna sababu moja tu ya tukio hili - ni uwasilishaji kwa umma wa mpango wa ushindi," Leshchenko alisema.

    Vyanzo vya gazeti la Ukraine la Ukrayinska Pravda vilithibitisha kwamba Zelensky anaweza kuwasilisha "mpango wa ushindi" kwa wabunge.

    Mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya wa masuala ya kigeni, Josep Borrell, pia alitangaza uwasilishaji wa Zelensky wa "mpango wake wa ushindi" katika mkutano wa Baraza la Ulaya, limeandika shirika la habari la Ukraine la Interfax .

    Mkutano wa Baraza la Ulaya katika ngazi ya wakuu wa nchi na serikali umepangwa kufanyika tarehe 17 na 18 Oktoba.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

  14. Mendy asema alikopeshwa pesa na wachezaji wenzake wa zamani wa Manchester City

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mendy alijiunga na City kutoka Monaco mwaka wa 2017

    Beki wa zamani wa Manchester City Benjamin Mendy anasema alikopeshwa pesa na wachezaji wenzake wakati huo Raheem Sterling, Bernardo Silva na Riyad Mahrez wakati klabu hiyo ilipoacha kumlipa baada ya kushtakiwa kwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono, aliiambia mahakama ya ajira.

    Beki huyo wa Ufaransa anadai mshahara wa £11.5m ambao haukulipwa tangu aliposhtakiwa Agosti 2021 na kusimamishwa bila malipo na City.

    Mendy, 30, aliondolewa mashtaka mwaka wa 2023 dhidi ya msururu wa mashtaka ya ubakaji na kujaribu kubaka.

    Klabu hiyo iliendelea kumlipa Mendy baada ya kukamatwa kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2020, lakini walidai kuwa hawakulazimika kufanya hivyo baada ya kushtakiwa kwa kuwa masharti yake ya dhamana, moja wapo yalimzuia kwenda karibu na uwanja wa klabu au uwanja wa mazoezi na shirikisho la soka lilimaanisha kuwa kwa kusimamishwa kwake asingeweza kutekeleza majukumu yake ya kimkataba.

    Nyaraka za mahakama zilisema Mendy "aliishiwa pesa haraka sana" na ilimbidi kuuza jumba lake la kifahari la Cheshire ili kulipia ada za kisheria za kesi, malipo ya matumizi na matunzo ya watoto baada ya kuzuiliwa kwa mshahara wake.

    "Raheem Sterling, Bernardo Silva na Riyad Mahrez wote walinikopesha pesa ili kunisaidia kujaribu kulipa ada yangu ya kesi na kusaidia familia yangu," Mendy alisema katika taarifa yake ya shahidi.

    Mnamo Novemba 2022, Mendy alituma ujumbe wa Whatsapp kwa Omar Berrada, ambaye alikuwa afisa mkuu wa uendeshaji wa kandanda wa City kuanzia Septemba 2020 hadi Julai 2024, kuuliza ni lini atapokea mishahara yake isiyolipwa lakini hakujibiwa.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Sean 'Diddy' Combs atuhumiwa kumnyanyasa kingono mvulana katika kesi mpya

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Sean "Diddy" Combs anakabiliwa na madai mapya ya ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia na mateso ya kingono baada ya msururu wa kesi mpya kuwasilishwa Jumatatu.

    Takriban kesi sita ziliwasilishwa katika mahakama ya shirikisho ya New York na wanawake wawili na wanaume wanne. Kesi hizo zinajumuisha madai ya kuanzia mwaka 1995 hadi 2021.

    Walalamikaji hao ambao hawakutajwa wanadai kuwa baadhi ya unyanyasaji huo ulitokea kwenye sherehe za Bw Combs, ambazo zilihudhuriwa na watu mashuhuri na wasanii wa muziki.

    Mawakili wa Bw Combs walikanusha madai hayo, wakisema katika taarifa kwa BBC kwamba "hajawahi kumnyanyasa mtu yeyote kingono - mtu mzima au mdogo, mwanamume au mwanamke".

    Mmoja wa wanaomshitaki alisema alikuwa na umri wa miaka 16 alipohudhuria moja ya karamu katika eneo la Hamptons mnamo 1998.

    Katika kesi hiyo, anaelezea kuwa alifurahi kupata mwaliko wa hafla ya Bw Combs, ambayo ilikuja kuwa hafla kuu ya kila mwaka ya watu mashuhuri.

    Alisema kuwa aliwaona watu mashuhuri na wasanii wengi wa muziki alipokuwa akitembea tembea, na akakutana na Bw Combs alipokuwa njiani kuelekea bafuni. Alisema alianza kuzungumza na Bw Combs kuhusu kuingia kwenye tasnia ya muziki ambapo walipoenda mahali pa faragha zaidi. Anadai kuwa wakati wa mazungumzo yao, Bw Combs alimuamuru ghafla avue nguo.

    Kesi hiyo inajumuisha picha ya wawili hao wakiwa pamoja kwenye karamu huku uso wa kijana huyo ukionekana kufichwa.

    Kulingana na shtaka hilo, Bw Combs alisema ni "utaratibu wa kupitia" na ni "njia ya kuwa nyota." Rapper huyo alimwambia kijana huyo kuwa anaweza kumfanya mtu yeyote kuwa nyota na akamwambia kijana ana "mwonekano" unaofaa [ kwa hilo], kesi hiyo inasema.

    Kesi nyingine iliyowasilishwa Jumatatu ni pamoja na kuhusu madai ya mwanamke ambaye anadai Bw Combs alimbaka katika chumba cha hoteli mwaka wa 2004 alipokuwa mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 19.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Lebanon yasema watu 21 wameuawa katika shambulio la anga kaskazini mwa nchi hiyo

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wakazi wanasema hakukuwa na onyo kabla ya shambulio hilo

    Takriban watu 21 wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio la nadra la anga la Israel kaskazini mwa Lebanon, wizara ya afya ya Lebanon inasema.

    Shambulizi hilo lililenga jengo la makazi katika kijiji cha Aitou, chenye wakazi wengi wa Kikristo mbali na maeneo ambayo jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi mengi dhidi ya kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Kishia la Hezbollah.

    Wakazi walisema kuwa familia iliyohamishwa hivi majuzi na vita imekuwa ikiishi huko.

    Jeshi la Israel halikutoa maoni yake mara moja kuhusu ripoti hizo. Lakini shambulizi hilo lilikuja baada ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuapa "kuendelea kuishambulia Hezbollah bila huruma kila mahali nchini Lebanon - ikiwa ni pamoja na Beirut".

    "Kila kitu kinafanyika kwa umakini na kwa muda uliopangwa.Tumethibitisha hili hivi majuzi na tutaendelea kulithibitisha katika siku zijazo pia,” aliongeza.

    Alikuwa akizungumza katika ziara yake katika kambi ya kijeshi kaskazini mwa Israel ambapo ndege isiyo na rubani iliyorushwa na kundi linaloungwa mkono na Iran iliwaua wanajeshi wanne wa Israel na kuwajeruhi makumi ya watu siku ya Jumapili usiku.

    Jeshi lilisema linachunguza jinsi ndege hiyo isiyo na rubani ilivyokwepa mifumo yake ya kisasa ya ulinzi wa anga na kupiga kituo cha mafunzo cha Golani Brigade kilichopo karibu na mji wa Binyamina.

    Unaweza pia kusoma:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Jumanne tarehe 15.10.2024