Rigathi Gachagua: Bunge la Seneti Kenya sasa kuamua hatma ya naibu wa rais

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wabunge nchini Kenya wamepitisha hoja ya kumuondoa madarakani naibu wa rais Rigathi Gachagua. Wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo, ilhali 44 waliipinga na kufikia thuluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa afisini
Hoja itapelekwa kwa Seneti, ambayo itafanya kazi kama mahakama ya kesi na itatoa uamuzi wa mwisho ndani ya siku kumi.
Theluthi mbili ya wingi inahitajika ili kupita.
Hapo awali, naibu rais alifika mbele ya bunge na kuwasilisha ushahidi wa kutosha ili kukabiliana na mashtaka 11 ya kumuondoa madarakani.
Anakabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo ufisadi, kumhujuu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila
Bw Rigathi Gachagua alishikilia kwamba hana hatia akidai kuwa amekuwa akitetea maslahi ya Wakenya.
Siku moja kabla ya kufika bungeni Gachagua alisema; ''Sina nia ya kujiuzulu kutoka wadhifa wangu na nitapambana hadi mwisho.''
Gachagua alifika bungeni kujitetea dhidi ya mashtaka 11 na kumekuwa na tofauti kubwa kati yake na rais William Ruto.
Tofauti kati ya Gachagua na rais William Ruto zimeonekana kuzidi na kufika hatua hii ambapo hoja hiyo inajadiliwa bungeni.
Gachagua awali alikuwa amesema hoja kama hiyo haiwezi kufikishwa bungeni kwa mjadala bila idhini ya rais William Ruto na alithibitisha hilo jana .
Licha ya kumuomba msamaha rais Ruto,naibu wa rais alisema hatua hiyo ya Jumapili haimaanishi kwamba ana makosa au hatia hasa kuhusiana na sababu zilizotolewa za kutaka aondolewe afisini.
Nini kilifanyika bungeni Jumanne?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bunge la Kitaifa limejadili hoja hiyo jana (Jumanne) na Gachagua akapewa fursa ya kujitetea. Baadaye wabunge walipiga kura na kuamua kumuondoa afisini .
Gachagua siku ya Jumatatu (07/09/2024) alisema madai dhidi yake hayana msingi wala ushahidi na alisisitiza msimamo huo alipofika bungeni dhidi ya kila sababu iliyotolewa dhidi yake
Gachagua alipuuza sababu zote ambazo zilitajwa katika hoja ya mbunge huyo kuanzia ile ya umiliki wa kiasi kikubwa cha mali ambayo alidai ilikuwa ni mali ya marehemu kaka yake ,gavana wa zamani wa Nyeri Nderitu Gachagua.
Alidai kuwa hatua ya kutaka kumuondoa afisini ni njama ya kisiasa inayoendeshwa na watu 'wenye hila , wasioogopa kuanzisha vita na wafu ili kujikita uongozini'.
Katika kilichoonekana kama ishara ya mgawanyiko zaidi kati yake na Rais William Ruto, Gachagua alidai kuwa hawezi kuidhinisha maamuzi ya serikali yanayoonekana kukiuka matakwa ya katiba kama vile utekaji nyara, mauaji ya kiholela na kuhamishwa kwa watu kutoka makazi yao kwa njia ya kikatili.
Alisema kama Mkenya yeyote ana haki ya kukosa Mkurugenzi mkuu wa shirika la kitaifa la ujasusi kwa utepetevu uliosababisha maandamano ya vijana miezi ya Juni na Julai mwaka huu na hilo halifai pia kutumiwa kama sababu ya kumtaka kuondolewa madarakani.
Hatua gani itakayofuata?

Chanzo cha picha, Getty Images
Spika wa Bunge Moses Wetangula ana siku mbili za kumpa taarifa Spika wa Seneti kuhusu matokeo ya mchakato wa leo. Kisha, Spika wa Seneti Amason Kingi ana siku saba kuwafahamisha maseneta.
Baada ya hapo, Seneti ina siku kumi za kuwasilisha kesi dhidi ya Gachagua, ambayo huenda itaanza Jumanne Oktoba 22. (Kwa sasa, Seneti pia inashughulikia hoja ya kumjondoa madarakani gavana wa Kaunti ya Kericho.)
Kesi ya Gachagua inaweza kutekelezwa katika kikao cha pamoja(cha seneti nzima) au kikao cha kamati, lakini kutokana na uzito wake, huenda kikawa kikao cha seneti nzima .Spika wa Seneti ataongoza kesi hiyo, maseneta watapata nafasi ya kumhoji Gachagua huku mawakili wake wakitarajiwa kuwahoji mashahidi waliowasilishwa na bunge.
Mmoja wa mashahidi hao ni Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.
Baada ya kesi ya mashtaka katika Seneti, kura ya thuluthi mbili itatosha kumtimua naibu rais kutoka afisi yake, kulingana na utaratibu wa kumuondoa madarakani ulioainishwa chini ya Kifungu cha 150 cha katiba.
Lakini naibu wa rais atasalia madarakani iwapo hoja hiyo itakataliwa na theluthi moja ya maseneta au iwapo Seneti itaunda kamati ambayo itapata sababu za kushtakiwa kukosa ithibati au msingi.
Naibu Rais pia atakuwa na haki ya kufika au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi dhidi yake.
Kamati Maalum inaweza kusikiliza hoja za mwakilishi au mbunge aliyewasilisha hoja hiyo katika Bunge na wajumbe wengine.
Ikiwa kamati maalum itaripoti kwamba maelezo ya tuhuma yoyote dhidi ya Naibu Rais hayajathibitishwa, mashauri mengine hayatachukuliwa chini ya Ibara ya 145 ya Katiba kuhusiana na madai hayo.
Iwapo yatathibitishwa, bunge la Seneti, baada ya Naibu Rais kupata nafasi ya kusikilizwa, litapiga kura kuhusu mashtaka dhidi yake.
Seneti itapiga kura ya 'ndiyo' au 'la' kuhusu kila shtaka dhidi yake.
Iwapo angalau thuluthi mbili ya wanachama wote wa Seneti watapiga kura kuunga mkono shtaka lolote la kumshtaki, atalazimika kuchia nafasi yake
Ikiwa hayatathibitishwa, naibu wa rais ataendelea kushikilia wadhifa huo.
Imehaririwa na Ambia Hirsi












