Sababu za kutaka kumuondoa madarakani naibu rais wa Kenya

Chanzo cha picha, X/Rigathi Gachagua
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wandani wa Rais wa Kenya William Ruto waliwasilisha hoja bungeni siku ya Jumanne ya kumshtaki Naibu Rais Rigathi Gachagua wakimtuhumu kwa kuchochea chuki za kikabila na kuidhoofisha serikali.
Tofauti kati ya rais Ruto na Gachagua zimeongezeka katika siku za hivi karibuni. Gachagua anasema ametengwa na amekanusha shutuma za washirika wa Ruto kwamba alihusika na maandamano ya kupinga serikali mapema mwaka huu.
Pia wanadai kwamba Gachagua amejihusisha na masuala ya ufisadi , kuihujumu serikali na kukuza siasa za kikabila.
Rais Ruto alimchagua Gachagua kama naibu wake katika uchaguzi wa 2022 ambapo walimshinda aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga katika uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkali.
Gachagua anatoka katika eneo la Mlima Kenya ambapo Rais Ruto alijipatia wingi wa kura ili kuibuka mshindi.
Tayari washirika wa kiongozi huyo wamefanya majaribio kadhaa ya kuzuia kura hiyo ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Wabunge wanaomuunga mkono rais Ruto wamesema kwamba wana zaidi ya idadi inayohitajika ya kumuondoa kiongozi huyo serikalini.
Zaidi ya wabunge 250 wanadaiwa kuunga mkono hoja hiyo ya kumtimua naibu huyo wa rais madarakani.
Lakini ni kesi gani haswa inayomuandama naibu huyo wa rais bungeni?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mutuse Mwengi, anakabiliwa na tuhuma kumi.
Gachagua analaumiwa kwa kukinzana na sera za serikali na kukosa kutekeleza majukumu yake kama Naibu Rais, hivyo basi kukiuka kanuni ya uwajibikaji wa pamoja wa Baraza la Mawaziri.
Hoja hiyo ya Mutuse Mwengi pia inadai kuwa Gachagua aliingilia shughuli za ugatuzi wa kaunti, kuhujumu ugatuzi na kutishia idara ya mahakama, hatua inayokiuka kanuni ya uhuru wa idara ya mahakama.
Vilevile hoja hiyo inataja utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, kutomtii Rais, kuwaonea maafisa wa umma, na kushawishi vitendo vya rushwa.
Mbunge huyo wa Kibwezi Magharibi anasema kwamba bwana Gachagua alishindwa kuheshimu na kutetea Katiba, huku matamshi yake ya uchochezi yakidaiwa kukiuka Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa kwa kuendeleza chuki za kikabila.
Aidha Gachagua anadaiwa alijihusisha na ufisadi, ufujaji wa pesa na matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka sheria za kupambana na ufisadi , kutoa taarifa za uongo na uovu na kukiuka kanuni za adhabu na sheria ya uongozi na uadilifu.
Kwa kura hiyo kupita , itahitaji thuluthi mbili za wabunge ambao wanashirikisha wabunge wa chama cha Raila Odinga cha ODM ambaye hivi karibuni ameonekana akishirikiana na Rais Ruto.

Chanzo cha picha, Ruto Campaign
Je, mchakato wa kumuondoa naibu wa rais unasemaje?
Mbunge, akiungwa mkono na angalau theluthi moja ya wajumbe wote, anaweza kutoa hoja ya kushtakiwa kwa naibu rais kwa msingi wa ukiukwaji mkubwa wa kifungu cha Katiba au sheria nyingine yoyote:
Pale ambapo kuna sababu kubwa za kuamini kwamba kiongozi huyo ametenda uhalifu chini ya sheria ya kitaifa au kimataifa; au kwa utovu wa nidhamu uliokithiri.
Iwapo angalau theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge wataunga mkono hoja hiyo
Spika wa Bunge atamjulisha Spika wa Seneti kuhusu azimio hilo ndani ya siku mbili:
Naibu Rais ataendelea kutekeleza majukumu ya afisi ya Naibu Rais akisubiri matokeo ya kesi ya mashtaka.
Ndani ya siku saba baada ya kupokea taarifa ya azimio kutoka kwa Spika wa Bunge-
Spika wa Seneti ataitisha mkutano wa Seneti ndani ya siku saba ili kusikiliza mashtaka dhidi ya Naibu Rais; na Seneti, kwa azimio, inaweza kuteua kamati maalum inayojumuisha wanachama kumi na moja kuchunguza suala hilo.
Kamati iliyoteuliwa kuchunguza suala hilo itaripoti kwa Seneti katika muda wa siku kumi iwapo itapata maelezo ya madai dhidi ya Naibu Rais kuwa yamethibitishwa.
Wanachama wa Kamati Maalum watakula Kiapo au Uthibitisho, kama Spika wa Seneti atakavyoagiza, wakiwasilisha kwamba watatekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa bidii.
Je, naibu rais atapewa fursa ya kujitetea?
Naibu Rais atakuwa na haki ya kufika na kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi wake.
Kamati Maalum inaweza kusikiliza uwakilishi wa mjumbe aliyetoa hoja katika Bunge na wajumbe wengine wa Bunge.
Ikiwa kamati maalum itaripoti kwamba maelezo ya tuhuma yoyote dhidi ya Naibu Rais hayajathibitishwa, mashauri mengine hayatachukuliwa chini ya Ibara ya 145 ya Katiba kuhusiana na madai hayo.
Iwapo imethibitishwa, bunge la Seneti, baada ya Naibu Rais kupata nafasi ya kusikilizwa, itapiga kura kuhusu mashtaka ya kumshtaki.
Seneti itapiga kura ya 'ndiyo' au 'la' kuhusu kila shtaka la kumshtaki).
Iwapo angalau thuluthi mbili ya wanachama wote wa Seneti watapiga kura kuunga mkono shtaka lolote la kumshtaki, Naibu Rais atakoma kushikilia wadhifa huo.
Ikiwa hayajathibitishwa, Naibu Rais ataendelea kushikilia wadhifa huo.














