Naibu wa rais nchini Kenya Rigathi Gachagua kujitetea bungeni leo

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rigathi Gachagua
    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Naibu wa rais nchini Kenya Rigathi Gachagua amesema kwamba atawasili bungeni hii leo ili kujitetea.

Naibu huyo ambaye anakabiliwa na hoja ya kumuondoa madarakani amesema kuwa atawasili mbele ya bunge pamoja na kundi lake la mawakili mwendo wa saa kumi na moja jioni ili kujitetea.

Akizungumza na waandishi habari nyumbani kwake huko Karen Jijini Nairobi, Kiongozi huyo amesema kwamba kabla ya yeye kuwasilisha hoja yake ya kujitetea atahitaji bunge kusikiliza maoni ya Wakenya waliomchagua.

Kiongozi huyo alisema anatumai wabunge watamruhusu kujibu tuhuma zote bila kuingiliwa.

Gachagua, amesema aliita kikao hicho na waandishi wa habari kutoa utetezi wake kwa Wakenya waliomchagua kabla ya kuwasili mbele ya wawakilishi hao.

"Nafikiri ni haki wakati wabunge wataamua kwamba wanataka kumwondoa Naibu Rais afisini, watu waliomchagua Rigathi Gachagua kuwa Naibu Rais wasikie upande wake," akasema.

Hoja ya kumuondoa madarakani iliwasilishwa Septemba 26 na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Mbunge huyo alitaja sababu 11 ambazo anataka Gachagua aondolewe afisini, ikiwa ni pamoja na kujilimbikizia mali ya hadi Sh5.2 bilioni katika muda wa miaka miwili pekee, kumhujumu Rais na kukuza ukabila.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Aidha amepuuzilia mbali mchakato wa kusikilizwa kwa maoni ya Wakenya kuhusu kuondolewa kwake madarakani akisema kwamba mpango wote huo ulishindwa kuafikia malengo yake.

“Majibu ya Naibu Rais hayakuwapo ili kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi,” Gachagua alisema na kuongeza kuwa mchakato huo ulifanywa katika njia ambayo Wakenya wengi hawakuweza kufahamu.

Akiangazia baadhi ya mashtaka yaliowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mutuse Mwengi ambapo ni pamoja na masuala ya Ufisadi, kiongozi huyo amesema kwamba baadhi ya mali anazomiliki ni urathi kutoka kwa ndugu yake mkubwa aliyefariki.

Gachagua anasema kuwa sehemu kubwa ya utajiri wake wa Sh5.2 bilioni ni sehemu ya mali ya ndugu yake marehemu Nderitu Gachagua.

'Heshimuni mtu aliyekufa', Gachagua alimwambia mbunge aliyewasilisha hoja ya kutaka aondoke madarakani bungeni.

Kiongozi huyo anasema kwamba Nderitu aliwakabidhi yeye pamoja na wakili mkuu Njoroge Regeru, na Mwai Mathenge mali yake ya kidunia ambayo ilikuwa igawanywe kwa familia yake.

“Katika wasia wake, marehemu kaka yangu alitoa mali na pesa taslimu. Miongoni mwao ni Hoteli ya Olive Garden, Vipingo Beach Resort, Queens Gate Apartment, na Langata Highrise Flats,” Gachagua alisema. "Mutuse anadai nilipata mali hizi baada ya kuwa naibu wa rais 2022, licha ya ukweli kwamba kaka yangu alikufa 2017."

Gachagua amekanusha madai hayo yote na kuyataja kuwa ni uwindaji unaochochewa kisiasa.

"Huo ni mpango wa kuniondoa ofisini kwa sababu ya mazingatio mengine na hauna uhusiano wowote na ukiukaji wa katiba, utovu wa nidhamu uliokithiri [au] kufanya uhalifu wa kimataifa au wa kitaifa," alisema.

Kulingana na Gachagua, kushtakiwa kwake siku ya Jumanne kutakuwa kitendo cha aibu zaidi katika historia ya bunge, kwani wabunge watajaribu kumuondoa kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia kwa msingi wa uzushi.

Alisema kumuomba msamaha rais hapo jana hakumaanishi kwamba anakubali makosa hayo.

Amewaapuzilia mbali wale waliodhani kwamba anaitisha mkutano na wanahabiri ili kujiuzulu '' mimi ni mtu niliyechaguliwa na watu milioni 7.2 , siwezi hata mara moja kujiuzulu, nitapigana hadi mwisho'', alisema bwana Rigathi.

Tofauti kati ya rais Ruto na Gachagua zimeongezeka katika siku za hivi karibuni. Gachagua anasema ametengwa na amekanusha shutuma za washirika wa Ruto kwamba alihusika na maandamano ya kupinga serikali mapema mwaka huu.

Rais Ruto alimchagua Gachagua kama naibu wake katika uchaguzi wa 2022 ambapo walimshinda aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga katika uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkali.

Lakini ni kesi gani haswa inayomuandama naibu huyo wa rais bungeni?

Kulingana na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mutuse Mwengi, anakabiliwa na tuhuma kumi.

Gachagua analaumiwa kwa kukinzana na sera za serikali na kukosa kutekeleza majukumu yake kama Naibu Rais, hivyo basi kukiuka kanuni ya uwajibikaji wa pamoja wa Baraza la Mawaziri.

Hoja hiyo ya Mutuse Mwengi pia inadai kuwa Gachagua aliingilia shughuli za ugatuzi wa kaunti, kuhujumu ugatuzi na kutishia idara ya mahakama, hatua inayokiuka kanuni ya uhuru wa idara ya mahakama.

Vilevile hoja hiyo inataja utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, kutomtii Rais, kuwaonea maafisa wa umma, na kushawishi vitendo vya rushwa.

Mbunge huyo wa Kibwezi Magharibi anasema kwamba bwana Gachagua alishindwa kuheshimu na kutetea Katiba, huku matamshi yake ya uchochezi yakidaiwa kukiuka Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa kwa kuendeleza chuki za kikabila.

Aidha Gachagua anadaiwa alijihusisha na ufisadi, ufujaji wa pesa na matumizi mabaya ya ofisi, kukiuka sheria za kupambana na ufisadi , kutoa taarifa za uongo na uovu na kukiuka kanuni za adhabu na sheria ya uongozi na uadilifu.

Kwa kura hiyo kupita , itahitaji thuluthi mbili za wabunge ambao wanashirikisha wabunge wa chama cha Raila Odinga cha ODM ambaye hivi karibuni ameonekana akishirikiana na Rais Ruto.