Kumekuwa na vita vingapi baina ya Israel na Lebanon? Na ni kwanini vilitokea?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel nchini Lebanon mwaka 2006: Wanajeshi wa Israel walitekeleza uvamizi wao wa tano mkubwa nchini Lebanon tangu mwaka 1978.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Israel imeanza uvamizi wa ardhini nchini Lebanon, baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya mabomu dhidi ya jirani yake na kulenga operesheni dhidi ya kundi la wanamgambo la Hezbollah.

Hii si mara ya kwanza kwa mashambulizi kama hayo kufanyika na mapigano yaliyopita yamekuwa na matokeo mchanganyiko.

Je, wakati huu unaweza kuwa tofauti na uvamizi wa awali?

1978: Uvamizi wa kwanza

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakati wa uvamizi wa 1978 kusini mwa Lebanon, unaojulikana kama "Operesheni Litani."

Lebanon imekuwa kituo kikuu cha wakimbizi wa Kipalestina baada ya kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948. Miongoni mwa wakimbizi hao ni wanamgambo wa Kipalestina, kama vile PLO.

Wanamgambo hao waliishambulia Israel kutoka Lebanon, na kuiingiza nchi hiyo katika mgogoro.

Israel iliivamia Lebanon kwa mara ya kwanza mwaka 1978 kujibu shambulio la kundi la kijeshi la Palestina Liberation Organization (PLO), ambalo lilikamata basi baada ya kufika ufukweni. Katika ghasia zilizofuatia, raia 38 wa Israel waliuawa katika kile kinachojulikana kama mauaji ya barabara ya pwani.

Vikosi vya Israel viliingia kusini mwa Lebanon na kuondoka miezi miwili baadaye. Walianzisha eneo la amani katika nchi yao jirani, ambapo walibaki askari wapatao 2000.

Uvamizi huu wa kwanza ulisababisha vifo vya wapiganaji 2,000 na raia upande wa Lebanon. Kwa upande wa Israel, wanajeshi 18 waliuawa.

1982: Uvamizi mkubwa zaidi

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakati wa uvamizi wa 1978 kusini mwa Lebanon, unaojulikana kama "Operesheni Litani."

Operesheni muhimu zaidi ya Israel nchini Lebanon ilifanyika mwaka 1982, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon.

Maelfu ya wanajeshi wa Israel, wakiongozwa na mamia ya vifaru na magari ya kivita, walivuka mpaka, hasa kuifurusha PLO, ambayo ilikuwa imeendelea kuishambulia Israel kutoka Lebanon.

Lengo la Israel lilikuwa kulenga maeneo ya PLO ili kuwazuia kushambulia Israeli.

Vikosi vya Israel vilipenya katika maeneo mbalimbali na kufanikiwa kufika viungani mwa mji mkuu Beirut, ndani ya wiki moja.

Wakati wa mashambulizi hayo, wanajeshi wa Israel walihusika na mauaji ya wakimbizi wa Kipalestina.

Waisraeli walijiondoa miezi mitatu baadaye, na kuunda eneo la amani (lisilo na mapigano) ndani ya Lebanon.

Kwa upande wa Lebanon, hadi watu 20,000 waliuawa, wengi wao wakiwa raia. Kwa upande wa Israel, wanajeshi 654 waliuawa.

1996: Adui mpya na uvamizi mpya

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maelfu ya raia wa Lebanon wamekwama katika mapigano kati ya Hezbollah na Israel, kama watu hawa katika mji wa Tebnin nchini Lebanon mwezi Aprili 1996.

Uvamizi wa Israel wa mwaka 1982 ulifanikiwa kuisambaratisha PLO, ambayo ilikuwa imehamisha makao yake makuu kutoka Lebanon hadi Tunisia. Lakini baada ya hapo, kundi la kijeshi la Hezbollah liliundwa, ambalo pia linaichukulia Israel kama adui yake na linataka kulishambulia.

Mwezi Aprili 1996, vikosi vya Israel viliingilia kati kwa mara ya kwanza dhidi ya Hezbollah, kujibu mashambulizi ya roketi ya kundi hilo. Uvamizi huo ulikuwa mdogo katika operesheni ambayo ilidumu kwa zaidi ya wiki mbili.

Kwa mara nyingine tena, raia waliteseka: wapiganaji kumi na watatu wa Hezbollah na hadi raia 250 waliuawa upande wa Lebanon. Israel haikupata hasara yoyote.

Israel na Hezbollah zimeendelea kutofautiana, huku mashambulizi kadhaa ya roketi yakifanywa na wanamgambo wa Kiislamu na mashambulizi ya mabomu yaliyotekelezwa na jeshi la anga la Israel.

2006: Siku 34 za vita

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Israel aliyejeruhiwa akikimbilia katika mpaka wa Israel baada ya uvamizi wa kusini mwa Lebanon, Julai 24, 2006.

Baada ya hapo ilikuwa Julai 2006. Mbali na kulipua miji ya Israel katika mpaka huo, wapiganaji wa Hezbollah walivuka mpaka na kuyashambulia magari mawili ya kijeshi na kuwaua wanajeshi wanane na kuwateka nyara wengine wawili.

Israel ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya anga na mashambulizi ya makombora dhidi ya maeneo yote ya Lebanon, vizuizi vya makombora ya angani na majini, na uvamizi wa ardhini kusini mwa Lebanon.

Vita hivyo vilidumu kwa siku 34 na kumalizika kwa usitishaji mapigano.

Watu 1,191 waliuawa nchini Lebanon, wengi wao wakiwa ni raia. Kwa upande wa Israel, wanajeshi 121 na raia 44 waliuawa.

Wataalamu wa kijeshi wanasema nini?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel waliuzingira mji mkuu wa Lebanon, Beirut mwaka 1982.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanajeshi wa Israel waliuzingira mji mkuu wa Lebanon, Beirut mwaka 1982.

Hatua ya Israel dhidi ya Hezbollah imebadilisha uwiano kati ya nchi hizo mbili kwa sasa, kwa mujibu wa mhariri wa BBC wa kimataifa Jeremy Bowen: "... Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Israel imeliangamiza kundi la Hezbollah, na kuharibu nusu ya silaha zake, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na Israel na kuivamia Lebanon.

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Israel Yoav Stern ameiambia BBC kuwa anaamini mkakati sawa na ule wa mwaka 2006, ambao ulikuwa wa uvamizi mdogo, utafanyika tena wakati huu - kinyume na ule wa mwaka 1982.

"Huu utakuwa ni uvamizi wa polepole, makini na wenye mahesabu, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa miji ya kusini mwa Lebanon moja baada ya mwingine, badala ya kuanzisha uvamizi wa haraka na wa kina," Stern alisema.

Anaongeza kuwa Hezbollah imekuwa katika miji ya kusini mwa Lebanon kwa muda mrefu, na hivyo inazuia Israeli kuikalia miji hii na kuiacha haraka.

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Timu za utafutaji na uokoaji zikijaribu kuwatafuta wale waliouawa katika shambulizi la anga la Israel katika kambi ya Wapalestina ya Ain Al Hilweh huko Sidon, Lebanon, Oktoba 1, siku ambayo Israel ilitangaza kuwa vikosi vyake vimeanza kuingia Lebanon.

Hata hivyo, kuna tofauti kati ya hali ya Lebanon na kampeni ya Israel huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, na jeshi la Israeli linaweza kusambaratisha upinzani wa Hamas.

Hali nchini Lebanon inaweza kuwa ngumu zaidi, licha ya mashambulizi ya mafanikio dhidi ya miundombinu na uongozi wa Hezbollah.

"Hezbollah sio Hamas: imeharibiwa, lakini bado ina silaha na imeweka kimkakati," anasema Profesa Amin Saikal, mtaalamu wa Mashariki ya Kati katika chuo kikuu cha taifa cha Australia.

"Kundi hilo litakuwa na uwezo wa kupambana na upinzani usio na mwisho kwa uvamizi wa Israeli. Hii inaweza kuwa na gharama kubwa ya kibinadamu na vifaa kwa taifa la Kiyahudi," anaelezea.

Jeremy Bowen anasema Israel bado haijafikia moja ya malengo yake makuu katika kampeni ya Gaza.

"Hezbollah ina, kwa akaunti zote, mitandao mikubwa ya mahandaki na mitambo kusini mwa Lebanon. Moja ya malengo yao ya kijeshi wakati walipoingia Gaza ilikuwa ni kuvunja mtandao wa mahandaki wa Hamas, na karibu mwaka mmoja baadaye bado hawajafanikiwa."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla