Kesi ya Diddy inaanza lini? Na unayofaa kujua kuhusu matatizo yake ya kisheria
Emma Vardy
Ndani ya mahakama

Chanzo cha picha, Getty Images
Nadine Yousif
BBC News
Sean 'Diddy' Combs, mmoja wa wasanii wa rapa na nguli wa muziki waliofanikiwa zaidi nchini Marekani, hivi karibuni atafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya utumwa wa ngono na ulaghai.
Katika kikao kilichohudhuriwa na Bw Combs siku ya Alhamisi, jaji aliamua kesi yake itaanza Mei 5 mwaka ujao.
Bw Combs, akiwa amevalia sare ya gereza , aliketi kando ya mawakili wake huku hakimu akijadili kuweka zuio dhidi ya mawakili au waendesha mashtaka kujadili kesi hiyo hadharani au na vyombo vya habari.
Familia ya Bw Combs iliketi kwenye viti ndani ya chumba cha mahakama. Rapa huyo alisema kimya kimya kwa ishara "I love you"(Nawapenda) kwa kundi hilo lililojumuisha binti zake watatu, wanawe wa kiume watatu na mama yake. Pia mara kwa mara aliweka mkono wake moyoni mwake na kufanya ishara ya maombi.
Mbali na kesi hiyo ya jinai, Bw Combs anashtakiwa na makumi ya watu ambao wamemshtaki kwa unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji na unyanyasaji wa kingono.
Bwana Combs amekana hatia katika kesi ya jinai na mawakili wa rapa huyo mara kwa mara wameshikilia kwamba hana hatia, wakiziita tuhuma dhidi yake "za uwongo na kashfa".
Hapa kuna mchanganuo wa matatizo ya kisheria dhidi ya Combs.
Kesi ya Diddy itafanyika lini?
Siku ya Alhamisi, Jaji wa mahakma ya Wilaya ya Marekani Arun Subramanian alipanga kesi hiyo hadi Mei ijayo, na itafanyika Manhattan.
Alhamisi ilikuwa mara ya tatu kwa rapa huyo kufika mahakamani tangu kukamatwa kwake.
Mwendesha mashtaka Emily Johnson alimweleza hakimu kwamba serikali itahitaji wiki tatu kuwasilisha kesi yake.
Wakili wa utetezi Marc Agnifilo alisema timu ya rapa huyo itahitaji wiki kwa ajili ya kesi hiyo.
Kesi hiyo ilipokwisha, baadhi ya wafuasi wa Mr Combs walikawia mlangoni, huku wakiwa na nia ya kumtazama na wakitarajia kumwona rapa huyo alipokuwa akisindikizwa.
Je, Diddy ametuhumiwa kwa nini?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Rapa huyo anakabiliwa na mashtaka ya jinai katika mahakama ya shirikisho. Pia anakabiliwa na kesi nyingi kutoka kwa watu ambao wamemshtaki kwa kuwadhuru na kuwatumia vibaya kujifaidisha.
Katika kesi ya jinai ya shirikisho, Bw Combs ameshtakiwa kwa utekaji nyara, dawa za kulevya na kulazimisha wanawake katika shughuli za ngono, wakati mwingine kwa kutumia bunduki au kuwatishia kwa vurugu.
Katika uvamizi katika jumba lake la kifahari la Los Angeles, polisi walipata vifaa ambavyo wanasema vilikusudiwa kutumiwa katika karamu zinazojulikana kama "freak offs", pamoja na dawa za kulevya na zaidi ya chupa 1,000 za mafuta ya watoto.
Kando, Bw Combs anakabiliwa na msururu wa kesi zinazomtuhumu kwa ubakaji na shambulio.
Tony Buzbee, wakili wa Texas anayeshughulikia baadhi ya kesi hizi, amesema kuwa zaidi ya wanawake na wanaume 100 kutoka kote Marekani wamefungua kesi dhidi ya msanii huyo wa rap.
Baadhi wamedai kuwa mashambulizi hayo yalitokea wakiwa watoto wadogo, wakiwemo wenye umri wa miaka tisa, Bw Buzbee amesema.
Matatizo ya sasa ya Bw Combs yalianza aliposhtakiwa na mpenzi wake wa zamani Cassandra Ventura, ambaye pia anajulikana kama Cassie, mwishoni mwa 2023. Alimshutumu kwa kumdhulumu na kumbaka.
Kesi hiyo ilitatuliwa kwa kiasi kisichojulikana cha fedha siku moja baada ya kuwasilishwa, na Bw Combs akishikilia kutokuwa na hatia.
Wiki zilizofuata, wanawake wengi waliwasilisha kesi mahakamani wakimtuhumu Bw Combs kwa unyanyasaji wa kijinsia, na shutuma zilizoanzia 1991. Mmoja wao alidai kwamba "alifanyiwa utumwa wa ngono" na "kubakwa na kundi" na rapa huyo na wengine wawili alipokuwa na umri wa miaka 17.
Bwana Combs alijibu msururu wa kesi katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram mnamo Desemba, akiandika: "INATOSHA."
“Sikufanya mambo yoyote ya kutisha yanayodaiwa. Nitapigania jina langu, familia yangu na ukweli,” alisema.
Miezi tisa baadaye, alikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Diddy yuko wapi sasa?
Bwana Combs amekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Gereza la Metropolitan huko Brooklyn, New York tangu kukamatwa kwake Septemba 16.
Mawakili wake wamedai kuachiliwa kwake akisubiri kusikilizwa kwa kesi, wakitoa mfano wa hali "mbaya" ya jela hiyo.
Jaji wa shirikisho la New York alikataa ombi lao la dhamana, akisema kuwa Bw Combs alikuwa na "hatari kubwa ya kukimbia".
Nini kinafuata katika kesi ya jinai ya Diddy?
Mawakili wake Jumatano waliiomba mahakama kutupilia mbali video ya mwaka wa 2016, inayoonyesha Bw Combs akimpiga teke mpenzi wake wa zamani Cassie Ventura alipokuwa amelala katika ukumbi wa hoteli.
Walisema kuwa serikali iliwajibika kwa kuvujisha video hiyo kwa CNN, na kwamba "imesababisha uharibifu, utangazaji wa upendeleo mkubwa ambao unaweza tu kuchafua nia ya jopo la majaji na kumnyima Bw Combs haki yake .
Mawakili wa serikali wanakanusha kuvujisha video hiyo kwa vyombo vya habari, wakisema kuwa serikali haikuwa nayo kabla ya kutangazwa mwezi Mei.
Wakati video hiyo ilipoibuka, Bw Combs alituma msamaha, akisema: "Nilichukizwa nilipokifanya kitendo hicho."
Mawakili wake bado wanapigania kumtoa rapa huyo kwa dhamana. Siku ya Jumanne, waliwasilisha rufaa wakisema kwamba Bw Combs alikuwa amekubali "masharti ya kizuizi" juu ya kuachiliwa kwake kutoka jela ambayo ingemzuia kutoroka.
"Bw Combs anachukuliwa kuwa hana hatia. Alisafiri hadi New York kujisalimisha kwa sababu alijua kwamba angefunguliwa mashtaka,” mawakili wake walisema kwenye jalada la mahakama.
"Alichukua hatua za ajabu kuonyesha kwamba alikusudia kukabiliana na kupinga mashtaka, sio kukimbia."
Wanasheria hao pia wamedai kuwa kila mtu aliyehusika katika kile kinachojulikana kama "freak offs" alikuwa mtu mzima aliyekubali'
Ikiwa ana hatia, Diddy atakabiliwa na kifungo cha jela?
Ndiyo.
Bw Combs anakabiliwa na kifungo cha maisha jela ikiwa atapatikana na hatia kwa kosa la ulaghai. Anakabiliwa na shtaka jingine la kisheria la miaka 15 kwa utumwa wa ngono.
Je, kesi ya Diddy itakuwa hadharani?
Kesi zote za shirikisho nchini Marekani ziko wazi kwa umma, isipokuwa katika hali nadra kesi zinapojumuisha taarifa nyeti zinazohusu usalama wa taifa.
Kufikia sasa, kesi zote za korti za Bw Combs zimekuwa wazi kwa vyombo vya habari na umma.
Hakuna vikao vya keshi hiyo hata hivyo, ambavyo vimepeperushwa moja kwa moja. Mahakama nyingi za shirikisho haziruhusu kamera au vifaa vya elektroniki kwenye chumba cha mahakama.
Wasanii wa michoro kwa kawaida huhudhuria vikao hivi ili kuchora taswira na matukio kutoka mahakamani kwa vyombo vya habari na umma.
Je, Diddy anaweza kukabiliwa na mashtaka zaidi?
Haijabainika iwapo Bw Combs atakabiliwa na mashtaka zaidi ya jinai.
Waendesha mashtaka, hata hivyo, wamesema kwamba uchunguzi "unaendelea" na wamewahimiza waathiriwa zaidi wenye malalamishi kufikia mamlaka.
Mwandishi wa BBC Emma Vardy alichangia kuripoti taarifa hii.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












