Afcon: Morocco itakuwa mwenyeji 2025 na Kenya-Uganda-Tanzania 2027

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Shirikisho la Soka barani Afrika Jumatano lilizipa Kenya, Uganda na Tanzania haki ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika 2027.

Rais wa CAF Patrice Motsepe alitangaza Zabuni ya Pamoja ya Afrika Mashariki kama mshindi wa haki za kuandaa bonanza la kwanza la kandanda la Afrika baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF mjini Cairo, Misri.

"Mustakabali wa soka wa Afrika haujawahi kuwa angavu zaidi…katika siku za usoni taifa la Afrika litashinda Kombe la Dunia," Motsepe alisema.

Mataifa ya Afrika Mashariki yalizishinda Misri, Senegal, Botswana na Algeria - ambao walijiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho siku mbili kabla ya kutangazwa rasmi - kwa haki za kuandaa.

Katika jitihada hizo, Kenya inasemekana kuwa mbele ya uboreshaji wa Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Moi, Kasarani, na Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, huku Uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret, zaidi ya kilomita 300 kutoka mji mkuu, ikiwa ni chaguo la tatu.

Uganda inasemekana kutumia Uwanja wa Namboole .Haijulikani ni chaguo gani la pili na la tatu lilitolewa, au ni vifaa gani vya mafunzo vimeahidiwa.

TH

Chanzo cha picha, AFCON

Kama ilivyotarajiwa na wengi, toleo la 2025 litafanyika Morocco. Itakuwa mara ya pili kwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuandaa michuano hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 1988. Washindani wengine wa 2025 (Algeria, Zambia na zabuni ya pamoja ya Benin/Nigeria) wote walikubali kujiondoa jambo ambalo liliiacha Morocco kama nchi ya pekee. Itaipa Morocco nafasi kubwa ya kuleta Kombe la Dunia barani Afrika mnamo 2030 kama sehemu ya ombi lao la pamoja.

Hatua ya kuzipa Kenya ,Uganda na Tanzaniafursa hiyo inaipa Afrika Mashariki nafasi ya kwanza tangu 1976 kuandaa mechi hizo wakati Ethiopia ilipokuwa mwenyeji .

Toleo lijalo, Afcon 2023, itafanyika nchini Ivory Coast, na litaanza Januari 13, 2024.

Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa ulioidhinishwa na CAF tayari umetajwa kama utakaotumiwa nchini Tanzania. Chamazi Complex - makao ya Azam FC, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na baadhi ya viwanja vya Dodoma, Arusha na Zanzibar ni baadhi ya sehemu ambazo Tanzania italenga kuviboresha ili kukidhi viwango vya Caf.

Kenya ilishinda maombi ya kuandaa makala ya Afcon 1996 pamoja na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika 2018, lakini katika hafla zote mbili ilipokonywa haki kwa sababu viwanja kadhaa havikuwa tayari.