Tetesi za Soka Ulaya: De Zerbi, Keane au Hoddle kuokoa jahazi la Spurs?

Chanzo cha picha, Getty Images/bbc
Tottenham Hotspur wamefanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Olympique de Marseille Roberto De Zerbi kuhusu uwezekano wa kumpa nafasi katika majira ya joto iwapo timu hiyo itasalia katika Ligi kuu (Telegraph)
Meneja na mchezaji wa zamani wa Tottenham Glenn Hoddle amesema yuko tayari kuisaidia timu hiyo kuepuka kushuka daraja iwapo kocha wa muda Igor Tudor ataondolewa baada ya kupoteza mechi zake tatu za mwanzo. (Mail)
Mchezaji mwingine wa zamani wa Tottenham Robbie Keane pia ametajwa kuwa miongoni mwa wagombea wakuu wa kumrithi Tudor iwapo klabu hiyo ya kaskazini mwa London itaamua kumtimua Tudor. (TeamTalk)
Mabingwa wa Italia Napoli wanataka kuchukua hatua haraka ili kumfunga kwa mkataba wa muda mrefu kiungo wa Scotland Scott McTominay, 29, huku kukiwa na vilabu kadhaa vya ligi kuu England vinavyomtaka. (Goal)
Mshambuliaji wa Newcastle United William Osula, 22, amesema hajui mustakabali wake utakuwa vipi, lakini kwa sasa anaweka mkazo wake katika timu hiyo ya Tyneside. Mchezaji huyo raia wa Denmark awali alihusishwa kutimikia VfB Stuttgart. (ChronicleLive)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Atlético Madrid Antoine Griezmann, 34, ameamua kutokuondoka katika klabu hiyo katikati ya msimu, licha ya klabu ya Marekani Orlando City SC kuonyesha nia ya kumsajili. (L'Equipe)
Manchester City wanatarajiwa kumpa mkataba mpya kiungo wa England Phil Foden, 25, mkataba wake wa sasa utakapomalizika mwishoni mwa msimu ujao, ingawa mazungumzo yanaweza kuwa magumu kutokana na kiwango chake kinachoyumba. (The Athletic)
Kiungo wa England Mason Mount, 27, hana mpango wa kulazimisha kuondoka Manchester United katika dirisha la usajili la majira ya joto. (Football Insider)
Manchester United wamejulishwa kuwa klabu ya Uturuki Trabzonspor haiko tayari kulipa kiasi kinachotakiwa cha pauni milioni 40 hadi 43 kwa ajili ya kumsajili kipa wa Cameroon Andre Onana, 29. (MEN)
Winga wa Brentford Kevin Schade, 24, anaendelea kuvivutia vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya huku Tottenham Hotspur, Bayern Munich na Inter Milan zikitajwa kuvutiwa na saini yake. (TeamTalk)















