'Tutapigana' - Ten Hag bado hajakata tamaa, lakini je, kocha huyo wa Man United anakaribia kupoteza kazi yake?

Chanzo cha picha, Getty Images
Zilipotimia dakika 90 uwanjani Estadio do Dragao, Erik ten Hag alionekana kukaribia mwisho wake.
Timu yake ya Manchester United ilikuwa imepoteza uongozi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Porto na ilikuwa ikielekea kupoteza.
Kichapo ambacho huenda hakikuthibitisha mwisho wa muda wa Ten Hag ndani ya Old Trafford lakini bila shaka kingemwacha akitetemeka, zaidi ya hapo awali.
Lakini kabla hali hiyo kutimia, Harry Maguire aliruka kwa kichwa na kusawazisha na kupunguza shinikizo kwa meneja wake.
"Tutafika tunakoelekea," Ten Hag aliiambia TNT Sports. "Usituhukumu kwa wakati huu, tuhukumu mwishoni mwa msimu.
"Tupo kwenye mchakato, tutaboresha. Tumekuwa na misimu miwili ambayo tumefika fainali, tutaendelea na kupambana."
Huku United kwa sasa ikiwa katika nafasi ya 13 kwenye jedwali la ligi ya Premier , na uvumi kufuatia kichapo cha 3-0 nyumbani kwa Tottenham kwamba Ten Hag alikuwa na mechi mbili kuokoa kibarua chake, uamuzi wa Mholanzi huyo kufungasha virago huenda ukafika mapema zaidi ikiwa hakutakuwa na maboresho makubwa.
"Unaweza kuona uhusiano kati ya wafanyikazi na timu," Ten Hag aliongeza.
"Wachezaji wapo pamoja, wana ari kubwa na wanataka kuafikia malengo yao, tuna mawazo mazuri lakini katika sehemu za ulinzi lazima tuongeze nguvu.
"Tulicheza mechi kadhaa bila kufungwa ikimaanisha tunaweza kuimarisha safu ya ulinzi, kwa hivyo lazima turudi kwenye tabia hiyo."
Je, hali ni mbaya kiasi gani? Takwimu zinasema nini kuhusu ukufunzi wa Ten Hag?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya Ten Hag kuendelea kujiamini yeye na timu yake, takwimu zinaonyesha kwamba ukosoaji kutoka nje huenda upo sahihi.
Tangu Mholanzi huyo ajiunge na klabu hiyo mwaka wa 2022, hakuna klabu yoyote ya Ligi Kuu iliyofungwa mabao matatu au zaidi katika mechi mara nyingi zaidi katika michuano yote kuliko mabao 24 ya United.
Zaidi ya hayo, katika mechi 62 walizocheza tangu kuanza kwa msimu uliopita, United wamefungwa mara 31 – ikiwa ni zaidi ya timu yoyote ya sasa ya Ligi Kuu.
Wamecheza mechi nne bila kufungwa kufikia sasa msimu huu lakini kwa timu yenye matamanio ya kuwania mataji makuu nyumbani na Ulaya, kuruhusu kufungwa mabao mawili au zaidi katika kila mechi ni jambo lisilopendeza.
Ina maana kwamba licha ya kufanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi nne zilizopita za ugenini za Ulaya, United wamepoteza mechi mbili na hawajashinda hata moja.
Sare ya huko Porto pia ilikuwa mfano mwingine wa tabia isiyohitajika ambayo wameanzisha: ya kutupa uongozi.
The Red Devils sasa wamecheza mechi tano bila ushindi katika mashindano ya Uropa licha ya kuongoza kwa angalau mabao mawili kati ya matatu kati ya hayo.
United sasa wamecheza mechi tano bila ushindi katika mashindano ya bara Ulaya , licha ya kuongoza kwa magoli mawili katika mechi tatu.
Kwa kuwa tayari wamekabiliwa na maswali juu ya uwezo wao wa kufunga mabao msimu huu, kwa kweli haiashirii vyema kwamba wanaweza kuruhusu mabao kama haya - na hata wanapojiweka mbele, wanawaruhusu wapinzani wao kukomboa.
Ten Hag yupo ukingoni
Hata baada ya kuepuka kushindwa nchini Ureno, Ten Hag bado anatazamwa na jicho la karibu kabla ya mechi ya Jumapili ya ligi dhidi ya Aston Villa.
Alisalia katika klabu hiyo msimu huu, baada ya timu yake kumaliza katika nafasi ya nane na kushinda Kombe la FA.
Ingawa matokeo mabaya ya msimu huu yameshuhudia shinikizo kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 kuongezeka tena, Mark Ogden, mwandishi mkuu wa ESPN, hatarajii kwamba Ten Hag atatimuliwa hata iwapo United itapoteza katika uwanja wa Villa Park.
"Nitashangaa ikiwa atapoteza kazi yake," aliambia BBC Radio 5 Live. "Kwa msingi kwamba hakuna pesa.
"Manchester United wanatumai ataboresha mambo. Ni wazi anapitia shinikizo kubwa’’
Lakini ni muda gani atasalia ikiwa matokeo hayataboreka pia ni suala jingine.
"Tabia ya wachezaji ni kama wamehudhuria somo la hisabati na mwalimu ambaye hawapendi na wote wanatoka wakiwa wamechanganyikiwa," Ogden aliongeza.
"Kwa kweli hakuna aina yoyote ya uchangamfu kutoka kwa Erik ten Hag hadi kwa wachezaji. Ten Hag hana haiba ya kusimamia klabu kubwa."
Ili kushinda timu ya Villa iliyochochewa na ushindi maarufu dhidi ya Bayern Munich, Ten Hag atalazimika kutafuta njia ya kuwatia moyo wachezaji wake la sivyo atashindwa kwa mara ya nne katika mechi saba za ligi ya premia .
"Erik ni mstahimilivu, ameonyesha hivyo lakini Villa Park itakuwa ngumu sana," kiungo wa zamani wa Manchester United Owen Hargreaves aliambia TNT Sports.
"Ni mtihani mkubwa na anahitaji kutafuta njia ya kurejea katika ushindi.
"Kabla ya mechi, tunaangazia kwamba wana matatizo ya ufungaji. Leo walikuwa na matatizo ya ulinzi. Wakati mwingine inaonekana kama wanapata suluhu na baadaye kitu na kitu kingine kinafanyika.
"Kuna matatizo mengi, yeye [Erik ten Hag] amekuwepo kwa muda mrefu. Kutakuwa na maswali mengi."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah












