Sudan: Pande zinazozozana zina sababu ya kuendelea kupigana

- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, Mwandishi BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Tarehe 1 Februari, ndege ya Sudan Airways yenye rangi ya njano na bluu ilitua katika uwanja wa ndege wa Khartoum. Abiria 160 waliokuwa kwenye ndege hiyo waliposhuka walishangilia, wakakumbatiana na kupiga picha
Hii ilikuwa ndege ya pili ya abiria kuwasili katika jiji hilo tangu mwaka 2023 na ilikuwa hatua muhimu kwa taifa hilo ikizingatiwa bado kuna tishio la mashambulizi ya droni katika nchi hiyo iliyogawanyika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wiki chache kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Sudan alikuwa ametangaza kwamba mwaka 2026 utakuwa "mwaka wa amani."
Kamil Idris aliyasema hayo mwezi Januari, wakati serikali inayoongozwa na jeshi ilipotangaza kuwa wizara za serikali zitarudi katika mji mkuu wa Khartoum uliokuwa umeharibiwa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mwaka mmoja uliopita mwandishi wa BBC Barbara Plet anasema "nilijionea Khartoum mwenyewe nikiendesha gari kwa uangalifu kuzunguka vilipuzi ambavyo havijalipuka vilivyokuwa kwenye barabara ya kutua ndege, na kutembelea maeneo ya mapokezi ya abiria yaliyoharibiwa katika jengo katika uwanja wa ndege, siku chache tu baada ya jeshi la Sudan kuurejesha mji huo kutoka kwa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF)."
Jiji hilo lilikuwa kitovu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwezi karibu miaka mitatu iliyopita, na kuacha jiji hilo likiwa limechomeka na kuharibiwa vibaya, huku serikali ikihamishiwa katika makao salama eneo la Port Sudan kwenye Bahari ya shamu.

Uharibifu ulikuwa wa kushangaza sana wizara za serikali, benki na majengo marefu ya ofisi yalionekana yakiwa yameungua.
Nilitembelea ikulu ya rais iliyoharibiwa vibaya, ambayo hata sasa bado imeharibiwa kiasi kwamba haiwezi kutumika, pamoja na ubalozi wa Uingereza, ambapo vioo vyake vya kuzuia risasi vilivyokuwa vimejaa alama za risasi vilishuhudia mapigano makali na vyumba vyake vikiwa vimeporwa.
Wakati huo ilionekana kama wakati mkubwa sana wa mabadiliko katika vita ambavyo vimesababisha uharibifu mkubwa, vifo, njaa na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia, na kuisukuma Sudan katika kile ambacho Umoja wa Mataifa (UN) umekiita "giza kubwa"
Katika safari nyingine baadaye, nilitembelea kambi ya wakimbizi katika eneo lililodhibitiwa na jeshi ili kuzungumza na watu waliokuwa wamefanikiwa kutoroka baada ya kuanguka kwa mji wa el-Fasher mwezi Oktoba, na nikasikia simulizi za mauaji ya halaiki na unyanyasaji wa kingono.
Kutwaliwa kwa mji huo katika eneo la Darfur Magharibi kulikuwa ushindi mkubwa kwa RSF. Hata hivyo, ushahidi wa ukatili uliofanywa na wapiganaji wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ulizua kilio cha kimataifa na kukashifiwa vikali.
Kwa muda mfupi wakati huo, pia ilionekana kana kwamba mataifa yenye nguvu duniani yangeweza hatimaye kuingilia kati ili kusitisha mateso mateso wanayoyapitia raia wa Sudan.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Licha ya lawama na maelezo ya kudhulumiwa kutoka kwa jamii ya kimataifa, hakuna kilichobadilika na mapigano yanaendelea .
Mwaka wa tatu wa vita hivi nchini Sudan unavyokaribia kutimia, safari hiyo ya ndege inaweza kuwa ilitoa mwanga mdogo wa hali ya kawaida. Lakini yale yanayochochea mapigano bado hayajatatuliwa.
Ikiwa hasira ya kimataifa haijatosha kushinda changamoto hizo, ni nini hasa kinaweza kuwalazimisha pande zote mbili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe?
Vita vya mara kwa mara
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sudan imekuwa katika vita kwa namna moja au nyingine kwa muda mrefu tangu ipate uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza mwaka 1956
Lakini migogoro ya awali ilikuwa ikipiganwa katika maeneo ya pembezoni, mbali na mji mkuu wa Khartoum. Vita hivi vya sasa vimepenya katikati ya nchi, na kusababisha idadi kubwa ya watu kuhama makazi yao, kuleta mgawanyiko , na hata kutishia kuigawanya taifa.
Vita hivyo vilianza baada ya Jeshi la Sudan na RSF kuanza kupambania madaraka.
RSF walikuwa wanamuunga mkono mtawala wa zamani wa kijeshi wa Sudan, Omar al-Bashir, ambaye aliondolewa madarakani mwaka 2019 kufuatia maandamano makubwa ya wananchi.
Omar al-Bashir alimpa mamlaka Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana sana kama Hemedti, kuendesha kikosi cha RSF kama walinzi maalum wa kumlinda dhidi ya changamoto zinazoweza kutokea ndani ya jeshi.
Baada ya kuondoka kwa Bashir madarakani, mvutano kati ya Hemedti na mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ulianza na baadaye kuwa vurugu.
Mwanzoni, "kulikuwa na makubaliano kwamba hii si vita vya Sudan bali ni vita vya mfumo wa usalama wa nchi," anasema mchambuzi wa siasa za Sudan Kholood Khair, mwanzilishi wa taasisi ya utafiti ya Confluence Advisory.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Lakini baadaye pande zote mbili zilipanua miungano yao na kuunganisha changamoto zao na malalamiko ya muda mrefu yaliyokuwepo tangu kuanzishwa kwa taifa hilo.
Malalamiko hayo yanatokana na utamaduni uliokita mizizi wa upendeleo kwa washirika tofauti na ufisadi mkubwa wakati jeshi la Sudan linadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa nchi.
Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye zamani alikuwa mfanyabiashara wa ngamia kabla ya kuwa maarufu, alipata utajiri mkubwa kupitia nafasi yake kama kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RSF.
Hata hivyo, kwa kuwa anatoka eneo la Darfur Magharibi, alijiweka kama mtetezi wa watu waliokasirishwa kwa kunyimwa maendeleo yaliyokuwa yanabakia kati mji mkuu.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mohamed Hamdan Dagalo anaelezea kuwa mgogoro huo unatokana na mifumo ya taifa hilo, akitangaza kuwa RSF inapania kuleta mapinduzi inayolenga kuvunja kile anachokiita "dola ya 1956" neno linalotumika kumaanisha mfumo wa dola unaotawaliwa na jeshi ulioundwa tangu Sudan ipate uhuru .
Kiongozi huyo alitangaza serikali yake pinzani yenye makao makuu eneo la Darfur.
Kwa upande mwingine, Jeshi la Sudan pia linafafanua vita hivi kama mapambano ya kuokoa taifa, likisema kinachoendelea ni uasi unaofanywa na "wanamgambo wa kigaidi."
"Kuna upinzani mkali ndani ya jeshi la Sudan la kutaka kuhalalisha kundi la RSF ikiwa ni pamoja na kukubali udhibiti wake wa maeneo fulani kupitia makubaliano ya kusitisha mapigano," anasema Ahmed Soliman, mtafiti mwandamizi wa Pembe ya Afrika katika taasisi ya utafiti ya Uingereza Chatham House.
Pande zote mbili pia zimetumia mgawanyiko wa kikabila uliokuwepo kwa muda mrefu kama silaha ya vita kati ya Waarabu w wa kusini na magharibi ambao ndio wafuasi wa RSF na Waarabu wa Bonde la Mto Nile kutoka mijini na mashambani, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiitawala nchi.
Historia ya vurugu za kikabila katika eneo la Darfur pia imechochewa tena, na wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa wakifanya mauaji ya halaiki dhidi ya jamii zisizo za Kiarabu, katika vitendo vya ukatili ambavyo Umoja wa Mataifa wanasema ni "dalili za mauaji ya kimbari"
Zaidi ya hayo, vita hivi vinachochewa pia na mataifa ya kigeni, ambayo yana maslahi ya moja kwa moja katika matokeo ya mgogoro huo au yanaona vita hivyo kama njia ya kupanua ushawishi wao katika eneo hilo.
Kuna ushahidi mkubwa ulioripotiwa kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unawapatia silaha wanamgambo wa RSF jambo ambalo Abu Dhabi inakanusha rasmi.
Jeshi la Sudan limekuwa likitumia droni za Kituruki na Iran, na pia limepokea ungwaji mkono wa kisiasa na misaada mingine kutoka Misri, Qatar na Saudi Arabia.
Jinsi ya kupata amani
Wengi wanamatumaini na diplomasia ya mazungumzo yanayofanywa na mataifa yanayojulikana kama Quad; Marekani, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Misri.
RSF imekubali pendekezo la Quad inayojumuisha kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya kibinadamu, lakini pande zote hazijajibu rasmi, na mapigano yamekua kwa kasi badala ya kupungua.
Burhan, mkuu wa jeshi la Sudan, anasema hawezi kukubali mpango huo uliopendekezwa wa kusitisha mapigano iwapo RSF haitasalimisha silaha zao
Zaidi ya hayo, pendekezo hilo linasema kuwa Sudan ijuimuishe uongozi wa kiislamu katika mustakabali wa Sudan.Hatua ambayo wachambuzi kama Ahmed Soliman ni ushawishi wa Abu Dhabi, kwani Marekani imeonyesha wazi upinzani wao kwa serikali itakayoendeshwa na Kiislamu mtazamo ambao wengi wa raia wa Sudan wanaopinga vita pia wanaunga mkono.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Inasemekana kwamba hiyo ndiyo moja ya sababu zinazosababisha UAE kuunga mkono RSF.
Vikosi vya wanamgambo wa Kiislamu ni sehemu muhimu ya jitihada za jeshi katika vita. Na taasisi za Kiislamu, ingawa zimedhoofika kutokana na mapinduzi ya mwaka 2019, bado zina ushawishi fulani.
Hii inafanya iwe ngumu kwa Burhan kukubali masharti haya.
Balozi wa Marekani, Massad Boulos, anasema ana mpango udhabiti na anamatumaini yakufikia makubaliano hivi karibuni juu ya kusitishwa kwa mapigano.
"Kusitisha silaha"
Lakini ili kusitishwa kwa mapigano itabidi kuambatanishwe na makubaliano kwamba washirika wa kikanda wasitishe kuwapa silaha pande zote mbili jambo ambalo haitakuwa rahisi kufanikisha.
"Kujaribu kusitisha mapigano wakati kila mtu anaendelea kusambaza silaha nchini humo hakuwezi fua dafu" anasema Alan Boswell, mchambuzi wa Pembe ya Afrika kutoka International Crisis Group.

Chanzo cha picha, Getty Images
Utata kuhusu nafasi ya Falme za Kiarabu
Ukosefu wa uwazi rasmi kuhusu nafasi ya UAE unafanya iwe sehemu ngumu ya kutatua mzozo huo na kupatikana kwa suluhu
Ripoti nyingi za uchunguzi, zimetaja data za ndege na picha za satelaiti, zinazoonyesha ndege za kiarabu zikisafirisha silaha hadi nchini Sudan kwa mamluki wa RSF, ushahidi zaidi, uliripotiwa na Umoja wa Mataifa.
Lakini Abu Dhabi inakanusha vikali kuwa wanaiunga mkono RSF kwa kuipa silaha na misaada mingine ya kivita.
Jinsi ya kupata amani
Ili kupata amani, mazungumzo lazima yashughulikie mizizi ya mgogoro huo hasa ukweli kwamba pande zote mbili zina sababu zinazowafanya wapate faida ikiwa vita vitaendelea.
Iwapo kusitishwa kwa mapigano kutaafikiwa, hata kwa muda mfupi kungeweza kutoa nafuu kidogo kwa raia wanaokumbwa na janga mbaya la kibinadamu huku watu milioni 25 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na watu milioni 12 wakikimbia makazi yao.
Hata hivyo, wengi wana hofu kwamba makubaliano ya muda hayataleta amani ya kudumu.
"Sioni kama kusitishwa kwa mapigano kwa ajili ya hali ya kibinadamu kutafanikiwa." Anasema Alan Boswell.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Na ingawa huu ni mgogoro kati ya nguvu mbili kubwa za vyombo vya usalama vya Sudan, kwa kiwango cha maeneo ya ndani unaendeshwa na makundi ya kikabila yaliyojiunga na RSF ambayo yanaona hii kama fursa ya kupata rasilimali na uwakilishi mzuri zaidi, au angalau kupata sehemu yao katika uchumi wa taifa hilo vita vikiendelea.
Pia kuna suala la uwajibikaji. Jeshi na vikosi vya wanamgambo, na washirika wao, wote wanatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, ukatili unaolenga makundi ya kikabila, na mauaji ya raia jambo linaloibua uwezekano wa kuwafungulia mashtaka viongozi wa kijeshi baada ya vita hivyo.
Mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea, yanafaa kuja na mfumo utakaowaruhusu makundi yenye silaha kubaki na baadhi ya mafanikio yao na kupunguza baadhi ya athari za kusitisha mapigano. Lakini hata hilo huenda lisitoshe.
Utawala wa kiraia ambayo ni pendekezo iliyotolewa na Quad katika makubaliano ya kuleta amani inamaanisha kupungua kwa mapato ya vikosi hivyo iwapo raia watachukua uongozi wa taifa hilo.
"Hofu kubwa"
Mnamo Septemba 2024 nilimuuliza afisa mmoja mwandamizi wa ulinzi wa Sudan alidhani vita hivyo vingedumu kwa muda gani alilinganisha mgogoro huo na vita vya miaka 20 vya Marekani dhidi ya Taliban nchini Afghanistan.
Historia inaonyesha kwamba vita vyote vya Sudan vimekuwa vya muda mrefu na kudumu hadi miaka 20.
Lakini mgogoro wa muda mrefu unaweza kuleta hatari ikiwemo uwezekano wa nchi kugawanyika au kusambaratika.
















