Moja kwa moja, Iran yasema itajibu mapigo hadi Tel Aviv iwapo Marekani itathubutu kuishambulia

Onyo hilo limetolewa na mshauri mkuu wa kiongozi wa juu wa Iran, Ali Shamkhani, ambaye alisema kuwa shambulio lolote la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran litachukuliwa kama tangazo la vita.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. CAF yaipiga faini ya dola 200,000 Morocco kwa kutaka 'kuiba' taulo la Senegal

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeorodhesha adhabu walizotoa kwa Morocco na Senegal kufuatia vurugu iliyoshuhudiwa wakati wa fainali ya AFCON 2026.

    Mashabiki wengi wa mpira walikuwa na hamu ya kujua hatua zipi zitashukuliwa na shirikisho hilo huku kila upande ukiamini mwenzake alikosea na anafaa kupata adhabu kali zaidi.

    CAF limempiga marufuku kocha wa Senegal, Pape Thiaw, michezo mitano na kumtoza faini ya $100,000 kutokana na mwenendo usio wa kispoti baada ya kuwaambia wachezaji wake waondoke uwanjani wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa dhidi ya Morocco.

    CAF pia ililazimisha shirikisho la soka la Senegal kulipa faini ya $615,000 kutokana na mwenendo wa timu na mashabiki wake, huku wachezaji Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr wakifutwa michezo miwili ya CAF kwa mwenendo wa kutojali taratibu dhidi ya refa.

    Hata hivyo, ombi la Morocco la kubatilisha matokeo ya mechi baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani, jambo lililosababisha kucheleweshwa kwa dakika 14, lilitupiliwa mbali na Kamati ya Nidhamu ya CAF.

    Wenyeji Morocco pia walitakiwa kulipa faini jumla ya $315,000 kutokana na mwenendo wa wavulana wa mipira (ball boys) wakati wa mechi, mwenendo wa wachezaji na wafanyakazi wao katika eneo la VAR, pamoja na matumizi ya mwangaza leza na mashabiki.

    Kapteni wa Morocco, Achraf Hakimi (michezo miwili ya CAF, mojawapo ikisimamishwa kwa mwaka mmoja) na Ismael Saibari (michezo mitatu ya CAF), walifutwa kwa mwenendo usio wa kispoti baada ya kujaribu kuondoa taulo ya kipa wa Senegal, Edouard Mendy, wakati mvua inanyesha Rabat.

    Kocha wa Senegal, Thiaw, aliwaamuru wachezaji wake waondoke uwanjani mwishoni mwa mechi baada ya goli lao kubatilishwa, na dakika chache baadaye Morocco walipatiwa penati, ambayo hatimaye Brahim Diaz aliipoteza.

    G

    Chanzo cha picha, BackpagePix

    Soma Pia:

  2. Kiongozi wa waasi wa Congo asema mkataba wa madini muhimu na Marekani ni batili kisheria

    Nangaa akiwa katika mkutano wa waandishi wa habari wa M23 mjini Goma

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nangaa akiwa katika mkutano wa waandishi wa habari wa M23 mjini Goma

    Kiongozi wa muungano wa waasi wa Congo unaojumuisha kundi la M23, Corneille Nangaa, amesema kuwa mkataba kati ya Kinshasa na Washington kuhusu madini muhimu katika mkoa unaokumbwa na vita ni batili kisheria, wenye mapungufu makubwa, na hali yake inatia shaka kuhusu utekelezaji wake.

    Nangaa, anayesimamia Alliance Fleuve Congo (AFC), alikuwa akirejelea makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyosainiwa Washington Desemba 4, ambayo yangewezesha Marekani kupata ufikiaji mkubwa wa madini muhimu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ubadilishanaji wa uwekezaji na ushirikiano wa usalama.

    Katika mahojiano na Reuters mjini Goma Jumatatu, Nangaa alisema kuwa mpango huo una upungufu wa uwazi na mapungufu ya kisheria, akirejelea kile alichokiita “ukosefu wa uwazi katika mazungumzo” na “mapungufu ya taratibu, hasa ukiukwaji wa Katiba na sheria.”

    Ukosoaji wa Nangaa unaibua maswali zaidi kuhusu uwezekano wa uwekezaji wa Marekani mashariki mwa Congo, mkoa uliokumbwa na vita, mwaka mmoja baada ya M23 kuchukua Goma, mji mkubwa zaidi wa mkoa, katika shambulio la ghafla.

    Sehemu kubwa ya madini muhimu mashariki mwa Congo, ikiwa ni pamoja na coltan, ziko katika maeneo ambayo sasa yanashikiliwa na M23, ambayo imechukua eneo kuu la migodi kama Rubaya katika Kivu Kaskazini.

    Nangaa alisema kuwa maeneo ya migodi yaliyotolewa kwa Washington yanaweza baadaye kuwa chanzo cha migongano, kwa sababu tayari yanaweza kuwa yametolewa kwa washirika wengine.

    “Wamarekani wanaweza kuwa wamesaini mkataba huo, lakini wanapaswa kujua kuwa walisaini na utawala usio halali, na pia uliyo na ufisadi,” alisema.

    Kwa upande mwingine, Ikulu ya Congo ilikanusha shutuma za Nangaa, ikisema ushirikiano huo “uko ndani ya mamlaka ya kikatiba” ya rais na serikali waliochaguliwa.

    Ikulu ilisema hofu kuhusu migongano na wamiliki wa mikataba ya awali ni “makadirio tu”, na kwamba ushirikiano wowote utafuata mikataba halali na kanuni za madini za Congo.

    Serikali ya Congo imesema kuwa ushirikiano huu utawasilishwa kwa wabunge kwa ajili ya idhini mwezi Machi.

    “Tuna wingi thabiti bungeni, hivyo tunaamini tutapata idhini ya bunge,” alisema Makamu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi wa Taifa, Daniel Mukoko Samba, kwa Reuters huko Davos wiki iliyopita.

    Soma Pia:

  3. Uzalishaji wa bangi kwa matumizi ya tiba waruhusiwa nchini Brazil

    v

    Chanzo cha picha, Valeria Mongelli/Bloomberg via Getty Images

    Anvisa (Wakala wa Taifa wa Udhibiti wa Afya wa Brazil) imeruhusu rasmi, siku ya Jumatano (Januari 28), kilimo cha mmea wa Cannabis sativa nchini Brazil kwa matumizi ya tiba na utafiti wa kisayansi.

    Uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Mahakama ya Juu ya Haki (STJ), ambayo mwezi Novemba 2024 ilithibitisha uhalali wa uzalishaji wa bangi kwa madhumuni ya tiba na/au dawa pekee, kama sehemu ya kulinda haki ya afya.

    Kwa matumizi ya tiba, wakurugenzi wa Anvisa wameidhinisha kwa kauli moja kilimo cha katani ya viwandani (industrial hemp), aina maalumu ya Cannabis sativa yenye kiwango cha tetrahydrokannabinoli (THC) kisichozidi asilimia 0.3.

    THC ndiyo kiungo kikuu cha mmea kinachosababisha athari za kisaikolojia.

    Aina hii ya bangi haisababishi kulevya, lakini ina kiwango kikubwa cha cannabidiol (CBD), ambayo inathaminiwa kwa uwezo wake wa tiba katika kusaidia wagonjwa wenye wasiwasi (anxiety), maumivu sugu, kifafa, matatizo ya usingizi, pamoja na magonjwa mengine ya mfumo wa neva.

    Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa, uzalishaji utakuwa na mipaka kulingana na mahitaji ya dawa, na kampuni zitawajibika kutoa taarifa na sababu za kiasi kinachozalishwa, ikiwemo ukubwa wa ardhi (hekta) itakayotumika kwa kilimo.

    Kilimo hicho hakijaruhusiwa kwa umma kwa ujumla, bali kinaruhusiwa kwa kampuni na mashirika maalumu pekee, na hatua hii haijumuishi matumizi ya burudani ya bangi.

    Soma pia:

  4. China yawanyonga wanachama 11 wa genge la ulaghai la Myanmar

    Makumi ya wanachama wa mafia ya Ming walihukumiwa mnamo 2025

    Chanzo cha picha, CCTV

    Maelezo ya picha, Makumi ya wanachama wa mafia ya Ming walihukumiwa mnamo 2025

    China imewanyonga wanachama 11 wa familia maarufu iliyokuwa ikiendesha vituo vya ulaghai nchini Myanmar, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Mahakama ya mkoa wa Zhejiang iliwahukumu wanachama wa familia ya Ming mwezi Septemba mwaka jana kwa makosa mazito yaliyohusisha mauaji, kuwazuia watu kinyume cha sheria, ulaghai, pamoja na kuendesha nyumba za kamari haramu.

    Familia ya Ming ilikuwa miongoni mwa koo kadhaa zilizotawala mji wa Laukkaing, uliopo karibu na mpaka wa China.

    Chini ya utawala wao, mji huo uliokuwa maskini na usiotambulika uligeuzwa kuwa kitovu cha kasinon, nyumba za starehe za ngono na uhalifu wa kifedha.

    Milki yao ya ulaghai iliporomoka mwaka 2023 baada ya wanachama wake kukamatwa na kukabidhiwa kwa China na makundi ya kijeshi ya kikabila yaliyokuwa yameuteka mji wa Laukkaing katika muktadha wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Myanmar.

    Kwa miaka mingi, mitandao ya ulaghai nchini Myanmar imewanasa maelfu ya raia wa China, na pia bara la Afrika halijasazwa, ambao ni miongoni mwa mamia ya maelfu ya watu waliotekwa au kusafirishwa kwa nguvu hadi katika kambi hizo, ambako walilazimishwa kuwalaghai watu wa nchi za nje.

    Mwaka jana, mitandao ya kijamii nchini China ilitikiswa na habari za muigizaji mdogo aliyesafiri kwenda Thailand kwa kazi ya uigizaji lakini baadaye akalazimishwa kupelekwa katika kituo cha ulaghai Myanmar.

    Visa kama hivi vilizidisha hasira ya umma nchini China, huku Beijing kwa muda mrefu ikiishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar kudhibiti magenge ya ulaghai.

    Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya China, shughuli za ulaghai na kamari za genge la Ming zilipata zaidi ya yuan bilioni 10 (sawa na dola bilioni 1.4 za Marekani) kati ya mwaka 2015 na 2023.

    Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa zao mwezi Novemba. Mahakama ilisema uhalifu wa genge hilo ulisababisha vifo vya raia 14 wa China na kujeruhi watu wengine wengi.

    Soma Pia:

  5. Nyota wa Bollywood Arijit Singh atangaza kustaafu uimbaji katika filamu akiwa na miaka 38

    Arijit Singh ni mmoja wa waimbaji maarufu nchini India hivi sasa

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Arijit Singh ni mmoja wa waimbaji maarufu nchini India hivi sasa

    Mashabiki wa mwimbaji maarufu wa India, Arijit Singh, wameonyesha huzuni na heshima zao baada ya kutangaza kuwa hataimba tena nyimbo za filamu (playback singing), hatua inayofunga ukurasa muhimu katika muziki wa Bollywood wa kisasa.

    Baadhi ya mashabiki wamesema sauti yake ilikuwa “sauti ya huzuni na furaha zetu”, huku wengine wakisema ilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watu wengi.

    Katika sinema ya India, playback singing ni pale mwimbaji anaporekodi wimbo studio na waigizaji wanauigiza kwa kusawazisha midomo kwenye filamu.

    Arijit Singh amekuwa mmoja wa waimbaji wakuu katika mtindo huu, hasa kwa nyimbo za mapenzi na nyimbo zilizopendwa sana.

    Singh, mwenye umri wa miaka 38, alitangaza uamuzi wake kupitia Instagram siku ya Jumanne, akisema: “Ninaacha hapa. Ilikuwa safari nzuri.”

    Tangu hapo, mitandao ya kijamii imejaa ujumbe wa mashabiki wakikumbuka jinsi nyimbo zake zilivyokuwa sehemu ya utamaduni wa India.

    Hakueleza sababu ya kuacha kuimba kwa filamu, lakini taarifa zinasema atakamilisha miradi aliyokuwa ameanza, na ataendelea kutunga na kuimba muziki wake binafsi, nje ya filamu za kibiashara.

    Hatua hii imewashangaza wengi kwa sababu imetokea wakati bado yuko kilele cha mafanikio.

    Hivi karibuni, aliimba mbele ya umati mkubwa uliojaa katika Wembley Arena, London, jambo linalofikiwa na waimbaji wachache wa India.

    Licha ya umaarufu wake, Arijit Singh amejulikana kwa kuepuka maisha ya umaarufu kupita kiasi.

    Hatoi mahojiano mara kwa mara, hapendi matangazo makubwa, na huonekana hadharani kwa mavazi ya kawaida.

    Aliwahi kusema: “Nachukia kuwa mtu maarufu.”

    Mwaka 2013, aliimba wimbo “Tum Hi Ho” katika filamu Aashiqui 2, wimbo uliobadilisha mwelekeo wa muziki wa mapenzi Bollywood kwa kuleta hisia za ndani na unyenyekevu.

    Wimbo huo ulipendwa sana kote India, ukachezwa redioni, harusi na vipindi vya televisheni.

    Baadaye, Singh alisema alihisi kero kusikia sauti yake kila mahali, na akaanza kupunguza idadi ya nyimbo alizokuwa akiimba.

    Licha ya yote, wengi wanaamini kuwa sauti ya Arijit Singh itaendelea kuishi na kuathiri muziki wa India kwa muda mrefu ujao.

    Soma Pia:

  6. Wademocrat wapendekeza masharti magumu ili kudhibiti vitendo vya ICE

    g

    Chanzo cha picha, US Immigration and Customs Enforcement

    Wademocrat katika Baraza la Seneti wametoa orodha ya matwakwa yanayokusudia kudhibiti vitendo vya maafisa wa uhamiaji wanaohusika na msako dhidi ya wahamiaji haramu ICE, matakwa ambayo maseneta hao wanasema sharti yafungamanishwe na mswada wa fedha kwa ajili ya wizara ya usalama wa ndani.

    Miongoni mwa matakwa hayo ni kuwapiga marufuku maafisa hao wa ICE kuvaa barakoa na doria kali za kushtukiza na badala yake wahitaji waranti, hati ya upekuzi, wa kumkamata mtu kutoka kwa Jaji.

    Kiongozi wa wademocrat kwenye seneti Chuck Schumer amesema matakwa yao sharti yazingatiwe akisema

    ''Tunataka barakoa zivuliwe na Kamera wanazovaa mwilini ziwashwe,maafisa wa uhamiaji wanapaswa kukatazwa kuvaa barakoa, lazima kamera zao ziwashwe na walazimike kubeba vitambulisho vinavyostahili.Hakuna tena maafisa wasiojulikana,hakuna tena operesheni za kisirisiri na iwapo warepublican watapinga,ni kwamba wanachagua vurugu badala ya kuwepo utaratibu,hivyo ndivyo ilivyo''

    Unaweza Kusoma Pia:

  7. Je, unafahamu uwezo wa Jeshi la Iran Revolutionary Guard ?

    Jeshi la IGRC linakadiriwa kuwa na wanajeshi 150,000

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Jeshi la IGRC linakadiriwa kuwa na wanajeshi 150,000

    IRGC (Islamic Revolutionary Guard Corps) ni jeshi maalumu la Iran lililoanzishwa mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.

    Kazi yake ni nini?

    • Kulinda utawala wa Kiislamu wa Iran.

    • Kumtii moja kwa moja Kiongozi Mkuu wa Iran, si serikali ya kawaida.

    • Kudhibiti usalama wa ndani na nje ya nchi.

    IRGC hufanya nini?

    • Ina jeshi lake, anga, majini na idara ya ujasusi

    • Inaendesha operesheni nje ya Iran kupitia kikosi chake kinachoitwa Quds Force

    • Inahusishwa na kusaidia makundi yenye silaha katika nchi kama Syria, Iraq, Lebanon na Yemen

    • Ina ushawishi mkubwa katika siasa na uchumi wa Iran.

    Kwa nini inapingwa?

    Nchi za Magharibi zinaishutumu IRGC kwa:

    • Kusaidia ugaidi

    • Kukandamiza haki za binadamu

    • Kuchochea migogoro katika Mashariki ya Kati.

    Kwa sababu hizo:

    • Marekani tayari imeliorodhesha IRGC kama kundi la kigaidi.

    • Umoja wa Ulaya unajadili kufanya uamuzi huo huo.

    Utawala wa rais Donald Trump umedai kwamba wapiganaji wa Quds pia wanatumiwa na Iran kama njia mojawapo ya kuwasaidia magaidi katika eneo la mshariki yakati-ikiwemo kundi la Hezbollah nchini Lebanon pamoja na kundi la Palestina Islamic Jihad -kwa kuwapatia fedha , mafunzo, silaha na vifaa.

    Wapiganaji wa Quds pia wametuhumiwa na Marekani kwa kupanga njama kutekeleza mashambulio ya kigiaidi , moja kwa moja ama kupitia washirika wake katika mabara matano kati ya saba.

    Wapiganaji wa Quds walidai kuhusika katika njama ya kumuua balozi wa Saudia nchini Marekani kwa kulipua mgahawa mjini Georgetown.

    Na mwaka uliopita , mahakama nchini Ujerumani ilimuhukumu mwanachama wa wapiganaji wa Quds kwa kumpeleleza kiongozi wa kundi la Ujerumani na Isra na watu wakaribu.

    Unaweza pia Kusoma:

  8. Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano kuitangaza IRGC kuwa kundi la kigaidi

    ff

    Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

    Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano ya kuitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kuwa kundi la kigaidi.

    Baada ya Uhispania na Ufaransa kuunga mkono hatua hiyo, pamoja na utayari wa Italia na Ujerumani ambazo hapo awali zilikuwa zimeunga mkono wazo hilo ndani ya Umoja wa Ulaya, inaonekana kuwa wabunge wa Bunge la Ulaya wamekubaliana kuidhinisha uamuzi huo.

    Siku ya Jumatano, Januari 28, Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Wiki hii, Ulaya ina fursa na wajibu wa kihistoria wa kulitangaza rasmi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la utawala wa Iran kuwa kundi la kigaidi.”

    Kabla ya kauli hiyo, mbunge wa Bunge la Ulaya, Hannah Neumann, alikuwa ametangaza kukubali kwa Uhispania na akaandika kwenye mtandao wa X:

    “Sasa kinachobaki ni Ufaransa.” Baadaye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alitangaza kuwa Paris inaunga mkono uamuzi huo.

    Inatarajiwa kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya watapiga kura leo, Alhamisi, Januari 29, kuhusu kuweka vikwazo vipya dhidi ya watu wanaokiuka haki za binadamu na kampuni 10 zinazohusishwa na utengenezaji wa ndege zisizo na rubani (drones) za Iran.

    Awali wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alisema angependekeza IRGC iongezwe katika orodha ya makundi ya kigaidi ya Umoja wa Ulaya.

    Kufuatia kauli hiyo, Iran ilimwita balozi wa Italia mjini Tehran kwenda Wizara ya Mambo ya Nje kulalamikia hatua hiyo.

  9. Ndege yaanguka Colombia, watu wote 15 waliokuwemo wafariki dunia

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ndege ya abiria imeanguka kaskazini mwa Colombia, na kuwaua watu wote 15 waliokuwemo, shirika la ndege la serikali la nchi hiyo, Satena, limethibitisha.

    Katika taarifa, shirika hilo lilisema ndege yake aina ya Beechcraft 1900'', ilipata ajali mbaya,” lakini halikutoa maelezo zaidi.

    Mabaki ya ndege hiyo sasa yamepatikana katika eneo la milima.

    Orodha rasmi ya abiria inajumuisha mbunge Diógenes Quintero Amaya na Carlos Salcedo, mgombea katika uchaguzi ujao wa bunge.

    Awali, Satena ilisema mawasiliano na ndege hiyo yalikatika dakika 11 kabla ya muda uliopangwa wa kutua katika mji wa Ocaña, karibu na mpaka wa Venezuela, saa 12:05 kwa saa za eneo (17:05 GMT) siku ya Jumatano.

    Kwa mujibu wa shirika la ndege, Safari ya NSE 8849 iliondoka katika mji wa Cúcuta, takribani kilomita 100 (maili 62) kaskazini-mashariki mwa Ocaña, ikiwa imebeba abiria 13 na wahudumu wawili wa ndege.

    Operesheni ya utafutaji miili imeanzishwa katika eneo la milima, na namba ya simu ya dharura imewekwa kwa ajili ya ndugu wa waliokuwemo ndani ya ndege.

    Akizungumza na chombo cha habari cha ndani, Semana, gavana wa Norte de Santander, William Villamizar, alisema miili saba imepatikana.

    Taarifa ya kuthibitisha kifo cha Quintero imeshirikiwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, ikimuelezea kama “mtu ambaye katika maisha yake yote aliwahudumia wale waliokuwa na uhitaji mkubwa zaidi.”

    Quintero alikuwa akishikilia kiti kimoja kati ya viti 16 katika bunge la Colombia vilivyotengwa kuwakilisha waathirika wa mgogoro kati ya jeshi la waasi wa Kimaaandiko ya Marx, Vikosi vya Mapinduzi vya Silaha vya Colombia (FARC), na serikali ya Colombia.

    Soma pia:

  10. Iran yasema itajibu mapigo hadi Tel Aviv iwapo Marekani itathubutu kuishambulia

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imetangaza kuwa imejumuisha mji wa Tel Aviv katika orodha ya maeneo itakayoshambulia iwapo itashambuliwa na Marekani au washirika wake, ikionya kuwa itajibu kwa haraka, kwa shambulilo lisilo na kifani. Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Tehran, Washington na Israel ukiendelea kuongezeka.

    Onyo hilo limetolewa na mshauri mkuu wa kiongozi wa juu wa Iran, Ali Shamkhani, ambaye alisema kuwa shambulio lolote la kijeshi la Marekani litachukuliwa kama tangazo la vita. Alisisitiza kuwa dhana ya “shambulio dogo” haipo na kwamba Iran italenga mshambuliaji ambaye ni Marekani pamoja na mji wa Tel Aviv.

    Jeshi la Iran na walinzi wa mapinduzi pia wamesema wako tayari kwa hali zote za kivita. Msemaji wa walinzi wa mapinduzi, Ali Mohammad Naeini, alionya kuwa uzoefu wa vita vya awali umeonyesha kushindwa kijeshi dhidi ya Iran, akisisitiza kuwa majeshi ya Iran ndiyo yataamua mwisho wa mapambano.

    Wakati huo huo, Marekani imeongeza kwa kiasi kikubwa uwepo wake wa kijeshi Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na kupeleka meli kubwa ya kivita ikiongozwa na manowari ya kubeba ndege ya Abraham Lincoln. Hatua hiyo imechochea hofu ya uwezekano wa shambulio la mapema kutoka Washington.

    Rais Donald Trump ameionya Iran kwamba "muda unakwisha" wa kujadili makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia kufuatia ongezeko la vikosi vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba.

    Kwa upande wmignien Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema serikali ya Iran iko dhaifu kuliko wakati mwingine wowote na huenda ikakabiliwa na maandamano mapya ya wananchi, huku akibainisha kuwa haijulikani ni nani atachukua nafasi ya Kiongozi wa juu iwapo angeondolewa madarakani.

    Kwa upande wake, Iran imekanusha madai ya udhaifu wa ndani, ikieleza kuwa maandamano ya hivi karibuni ni njama za kigeni. Serikali ya Tehran imesisitiza kuwa itatetea mamlaka, uhuru na mfumo wake kwa nguvu zote endapo itakabiliwa na shambulio lolote la kijeshi.

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya habari za moja kwa moja leo Alhamisi Januari 29, 2025