Bangi: Zijue nchi tano zilizoruhusu uzalishaji wa bangi Afrika

Banghi

Chanzo cha picha, Ganjapreneur

Maelezo ya picha, Matumizi ya bangi kwa ajili ya dawa, imekuwa fursa ya kiuchumi kwa nchi nyingi za Afrika

Bangi ni zao haramu kisheria katika nchi nyingi dunaini, linapigwa marufuku kwa sababu ya athari zake kiafya, lakini yapo mataifa yanayoruhusu uzalishaji wa bangi kwa sababu ya matumizi ya dawa. Kuweka uwiano wa matumizi yake kiafya na matumizi ya starehe kunaleta ukakasi na mzozo wa kimajadiliano kati ya watafiti na watumiaji wa zao hilo duniani.

Ripoti ya mwaka 2019 kutoka Taasisi ya kimataifa inayoshughulika na masuala ya bangi Afrika (Africa Regional Hemp and Cannabis), zinaonyesha Afrika inachangia dola milioni $37.3 kwenye soko la dunia la bangi abayo ni sawa na asilimia 11%.

Kwa sasa dunia inashuhudia nchi nyingi zikiifanya bangi kuwa zao halali na kuanza kulimwa kwa wingi. Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia uhalifu na dawa za kulevya (UNODC), inasema kati ya mkwa 1995 mpaka 2005, nchini 19 kati ya 53 barani Afrika ziliripoti kuzalisha bangi au marijuana.

Morocco ni nchi ya hivi karibuni kutoka Afrika kuruhusu kilimo cha bangi kwa matumizi ya dawa na viwanda. Afrika Kusini, Ghana, Uganda ni nchi zenye uelekeo huo licha ya kuwa na sheria zinazokataza matumizi yake kwa starehe. Wajasiriamali wanasema zao hilo linaingiza fedha nyingi kwa sasa linapouzwa nje ya nchi. Unaweza kujiuliza kwa kiwango gani bangi ni fursa na nchi gani zimechukulia zao hilo kama fursa kubwa kiuchumi? BBC inakuletea orodha ya nchi 5 barani Afrika zilizoruhusu kilimo cha Bangi.

Morocco

Bangi

Chanzo cha picha, AFricaNews

Maelezo ya picha, Nchini Morocco bangi hulimwa zaidi kwenye maeneo ya milima

Wiki hii Bunge la Morocco limepitisha sheria ya kuruhusu bangi kulimwa nchini humo kwa matumizi ya dawa tu, ikiwa ni nchi ya hivi karibuni Afrika kufanya hivyo. Wabunge 119 walipiga kura ya kuunga mkono huku 48 wakikataa.

Morocco ndiye mzalishaji mkubwa wa zao hilo hata kabla haijawa sheria rasmi kwa sababu udhibiti wake haukuwa na nguvu kutokana na kutegemewa na sehemu kubwa ya wananchi. Kwa mfano eneo la Rif, lenye watu zadiya milioni 1, kilimo cha bangi kinasaidia familia kati ya 90,000 na 140,00.

Mwaka 2016, ripoti zinasema asilimia 80% ya mapato ya kiuchumi ya eneo hilo yalihusishwa na kilimo cha bangi. Huku Ripoti moja ya Marekani inakadiria kuwa Morroco kuingiza dola $23bn kila mwaka kutokana na zao la bangi. Na hicho ndicho hasa kilichowasukuma wabunge kulipitisha zao hilo ili lilimwe halali.

Rwanda

Bangi

Chanzo cha picha, Devidscourse

Maelezo ya picha, Mashamba mengi ya bangi hulimwa kisasa kwa lengo la kuzalisha zaidi kusafirishwa nje

Mwaka jana Rwanda, iliruhusu uzalishaji wa bangi kwa ajili ya matumizi ya dawa kwa kuuza nje na kuongeza mapato. Serikali ya Rwanda inasisitiza kwamba uzalishaji wa bangi utafanywa kwa watu waliopewa leseni maalumu kwa mfano maduka ya dawa, na kwamba matumizi ya kawaida ya starehe bado bangi ni kosa kisheria.

Sheria ya Rwanda inakataza matumizi ya bangi kwa starehe na ukikutwa unaweza kufungwa miaka mpaka miwili na kwa wale wauzaji wanaweza kufungwa mpaka kifungo cha miaka 20.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Green Party, Frank Habineza, aliwahi kunukuliwa akisema ni jambo zuri Rwanda kuruhusu uzalishaji wake lakini serikali ingeruhusu moja kwa moja kwa matumizi ya ndani ikiwemo ya dawa.

Lesotho

Bangi

Chanzo cha picha, KOHK

Hii ndiyo nchi ya kwanza kupewa leseni rasmi ya kimataifa na kusafirisha bangi kwenye soko la kimataifa kwa ajili ya utengenezaji wa dawa.

Mwaka 2008 Lesotho ilikuwa nchi ya kwanza kutoka Kusini mwa Afrika kuruhusu kisheria matumizi ya bangi, asilimia 70% ya soko la bangi Afrika Kusini, linashikiliwa na Lesotho.

Kampuni moja ya ndani ya uzalishaji wa bangi (MG Health) imeongeza uzalishaji wake sasa kutoka kilo 250 kwa mwezi mpaka kufikia mamia ya tani katika eneo linalofikia mita za mraba 16,000. Soko lake kubwa la bagni yake ni Ujerumani wanakotengeneza dawa.

Zimbabwe

Baada ya kuruhusu bangi kisheria mwaka 2019, Zimbabwe imeshuhudia zao hilo kuzalishwa mara tatu zaidi ya zao la tumbaku lililozoeleka. Zao la tumbaku kwa miaka mingi lilikuwa zao kuu la biashara linalouzwa nje ya nchi hiyo, ikiingizia dola milioni $444 mwaka kwa mujibu wa bodi ya tumbaku ya nchi hiyo.

Serikali nchi hiyo mpaka kufikia September mwaka jana ilikuwa tayari imetoa vibali 44 kwa wazalishaji wa bangi huku ikikadiriwa zao hilo litaiingizia nchi hiyo dola zinazofikia $1.25 mwaka huu.

Zambia

Bangi

Chanzo cha picha, MANGOKWETU

Maelezo ya picha, Bangi ni marufuku kwa nchi kama Tanzania, Polisi wamekuwa wakiendesha doria na kukamata wavuta bangi na wanaolima bangi

Bangi ni halali nchini Zambaia, imehalalishwa kisheria mwaka 2019 na ikielezwa imepitishwa kupunguza makali ya deni la taifa la nchi hiyo. Toka mwaka 2018 deni la taifa la nchi hiyo linaongezekwa kwa dola bilioni 10 kilwa mwaka.

Kiongozi wa upinzani nchini humo, Peter Sinkamba, ambaye alikuwa anasukuma zaidi zao hilo kuruhusiwa alisema, linatweza kuliingizia taifa hilo mpaka dola bilioni $36 kwa mwaka.

Nchini Zambia ukilipa dola $250,000 utapata leseni itakayokuwezesha kulima na kuuza nje bangi kwa matumizi ya dawa.

ONYO: Bangi hairuhusiwi katika baadhi ya nchi zikiwemo za Afrika Mashariki na ni kosa kisheria.