Je, Marekani inajiandaa kuchukua hatua gani dhidi ya Iran?

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Meli ya kubeba ndege ya Lincoln yenye uzito wa tani 100,000 inaelekea kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.
    • Author, Mehrnoush Pourziaei
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kutokana na kufungwa kwa intaneti, kuna taarifa chache zinazopatikana kutoka ndani ya Iran. Maandamano ya mitaani yanafikiriwa kupungua kwa kiasi kikubwa baada ya msako mkali wa serikali, lakini mvutano bado uko nje ya mipaka ya nchi hiyo, na baadhi ya wachambuzi wanaangazia uwezekano wa hatua za Marekani.

Maafisa wawili wakuu wa zamani kutoka Idara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, katika mahojiano na BBC Persian, wanasema bado Marekani inatafuta la kufanya.

Kulingana na tathmini yao, Idara za usalama na jeshi la Marekani zinakabiliana na maswali magumu. Moja, ni kutokuwa na uhakika kuhusu kitakachotokea baada ya shambulio la Marekani. Pili, kushindwa kwa Marekani kutabiri matokeo ya kisiasa kutokana na vitendo vyake vya kijeshi" katika eneo hilo. Ni baadhi tu ya maswali yanayowakabili washauri wa kijeshi wa Washington.

Wanasema kutokuwepo kwa waandamanaji mitaani na "kutokuwepo kwa ukandamizaji wa Tehran," hatua za kijeshi zitakuwa ngumu na zenye changamoto kwa Washington, ingawa mtindo wa kufanya maamuzi wa Donald Trump umeonyesha anaweza kubadilika wakati wowote.

Kutafuta jibu

l

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza Juni 21 kwamba vituo vya nyuklia vya Iran vilishambuliwa kwa amri yake.

Ijumaa, Januari 2, Pentagon ilikuwa katikati ya kukamilisha mpango wa uvamizi wa Ikulu ya rais wa Venezuela na kumkamata "Nicolas Maduro" ambapo ghafla jambo jingine muhimu liliwekwa kwenye ajenda.

Donald Trump alitangaza "silaha zilizojaa za Washington ziko tayari kuwaunga mkono waandamanaji wa Iran ikiwa serikali itawauwa.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, chini ya saa 36 baada ya taarifa ya Trump, rasimu ya kwanza ya mapendekezo ya jinsi ya kuishughulikia Iran ilikuwa kwenye dawati la rais wa Marekani.

Ni rasimu inayoangazia changamoto: Hakuna meli za kubeba ndege za Marekani katika maji ya eneo hilo. Ikiwa kutakuwa na shambulio lolote dhidi ya Iran na likafuatiwa na kulipiza kisasi kutoka Tehran, kikosi cha jeshi kilichopo katika Ghuba ya Uajemi hakitakuwa na ngao ya kujilinda ili kulinda kambi za Marekani na washirika wake dhidi ya makombora ya Iran.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mkutano huo ulimalizika Jumamosi usiku bila uamuzi wa mwisho, na chaguzi hiyo ikawekwa kando kwa muda.

Nilipomuuliza Mara Carlin, naibu waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani: Je, rais hakujua kwamba hakuna meli ya kubeba ndege katika Ghuba ya Uajemi, alijibu, "Rais mwenyewe huenda hakuzingatia hili sana, lakini nina uhakika wale wanaomshauri katika Idara ya Ulinzi wamesisitiza umuhimu wa hilo.”

Afisa mkuu wa zamani wa Pentagon, ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameiambia BBC, ikiwa rais anataka kuchukua hatua za kijeshi "kuwaunga mkono waandamanaji," swali la kwanza la Pentagon, si aina ya silaha, bali ni lengo la kisiasa la rais ni lipi.

"Je, ni kutuma ujumbe wa onyo kwa Tehran ili kupunguza ukandamizaji, au lengo ni kudhoofisha muundo wa usalama na hata kubadilisha utawala"?

Tatizo jingine ni kwamba washauri wa kijeshi wa rais wa Marekani wanajua kwamba yeye ni rais asiye wa kawaida ambaye si lazima afuate mifumo ya kawaida ya kisiasa huko Washington.

Naibu waziri huyo wa zamani wa ulinzi anataja tatizo jingine ambalo baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vimelielezea kama "utafutaji wa Trump wa chaguo la uhakika la asilimia 100."

"Sijawahi kuona chaguo la kijeshi ambalo limehakikishwa asilimia 100," anasema. "Daima kuna kiwango fulani cha hatari na hatari isiyoepukika."

Mashaka na hatari

l

Chanzo cha picha, Khamanei.ir

Maelezo ya picha, Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds, aliuawa Januari 3, 2020, kwa amri ya Donald Trump.

Mjadala wowote kuhusu "chaguo la kijeshi" huko Washington huibua suala la kulipiza kisasi kutoka Iran. Iran bado ina mamia ya makombora ya masafa marefu, na vituo kadhaa vya Marekani katika eneo hilo, vyenye karibu wanajeshi 30,000 wa Marekani, viko karibu, kulingana na afisa wa zamani wa Pentagon.

Anabainisha kuwa katika siku ambazo mazungumzo juu ya kufanya shambulio yalizidi kuwa makubwa, kutokuwepo kwa meli ya kubeba ndege katika eneo hilo likuwa ni jambo la hatari na la ajabu kwa baadhi, ikizingatiwa kwamba meli hiyo ya kubeba ndege na kikosi kazi kinachoambatana nayo kina jukumu muhimu katika ulinzi dhidi ya makombora na usimamizi wa migogoro.

Ushauri kwa rais huko Washington unashughulikia chaguzi mbalimbali, kuanzia hatua za kijeshi na mabadiliko ya utawala, vikwazo kwa meli za mafuta, mashambulizi ya mtandaoni, au operesheni ya siri ya ghafla, kama ile ya kumuondoa madarakani rais wa Venezuela.

Afisa huyo wa zamani wa Pentagon amesema ikiwa chaguo la mwisho ni shambulio "la kutisha" linalomlenga kiongozi wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, Iran inatarajiwa kutafuta jibu zito sana dhidi ya Marekani.

Jibu ambalo, bila mwavuli wa ulinzi wa makombora na mandalizi mazito, linaweza kuwa na gharama kubwa kwa vikosi vya Marekani.

Kwa upande mwingine, shambulio dogo kwenye majengo matupu au baadhi ya kambi za Basij au Wizara ya Ujasusi, linaweza kutuma ujumbe wa kisiasa kwa Tehran na wakati huo huo kupunguza uwezekano wa jibu kali la Iran, lakini halitabadilisha mambo kati ya waandamanaji na serikali

Ugumu wa kutabiri

l

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Mwaka 2003, Rais wa Marekani George Bush alitangaza kumalizika kwa Vita vya Iraq akiwa ndani ya meli ya kubeba ndege ya Lincoln, lakini vita hivyo vilidumu kwa miaka mingine saba na kusababisha vifo vya maelfu ya wanajeshi wa Marekani.

Katika majira ya kuchipua ya mwaka 2003, Rais wa Marekani George W. Bush alitangaza Vita vya Iraq kuwa vimemalizika kwa mafanikio, akiwa ndani ya meli ya kubeba ndege ya Lincoln. Lakini vita hivyo viliendelea kwa miaka mingine saba na kusababisha vifo vya maelfu ya wanajeshi wa Marekani.

Historia ya migogoro kati ya Iran na Marekani, iwe ni kuuawa kwa Qassem Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha IRGC, au wakati wa vita vya siku 12, imeonyesha kwamba Iran kwa ujumla imejaribu kutoa jibu la kulipiza kisasi au imeahidi kulipiza kisasi.

Kulingana na afisa wa zamani wa Pentagon, kutokana na kupungua kwa maandamano ya barabarani, Marekani inaweza kuendeleza sera ya shinikizo kwa kutishia rasilimali za mafuta za Iran ili kuirudisha Iran kwenye meza ya mazungumzo, badala ya kuchukua hatua moja kwa moja.

"Ikiwa watu hawapo mitaani, itakuwa vigumu sana kufanya shambulizi na hiyo ndio changamoto," anasema Mara Carlin.

"Kundi la meli za kubeba ndege huenda likawasili katika eneo hilo katikati ya wiki ijayo, na labda ikiwa mambo yanaonekana kuwa shwari na watu hawapo mitaani, meli zitakaa katika eneo hilo kama kizuizi."

Kinachoonekana kuwa na uhakika hadi sasa ni kwamba Donald Trump si wa kawaida katika maamuzi yake. Wakati wa vita vya siku 12, awali alisema Marekani haitashiriki katika shambulio dhidi ya Iran, lakini ghafla akaamuru shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.

Mwaka uliopita, kulingana na shirika la "Armed Conflict Events and Locations Database" (ACLED), Marekani imefanya mashambulizi 626 ya anga katika nchi mbalimbali duniani kote, ikiwa ni pamoja na Somalia, Iran, Yemen, Nigeria, Venezuela, Iraq na Syria, yote yalifanywa kwa idhini ya rais wa Marekani.

Mara Carlin anasema, kwa marais waliopita unajua wakati serikali iko tayari kutumia nguvu za kijeshi na wakati ambapo haitaki kutumia nguvu za kijeshi. Lakini kwa Rais Trump, kila kitu hakina uhakika na ni vigumu sana kutabiri."